Habari za Kaunti

Kifo cha ‘Sniper’: Maafisa wapekua kwa Mwangaza

January 6th, 2024 2 min read

NA GITONGA MARETE

MAAFISA wanaoweka zingatio katika kuchunguza uhalifu wa mauaji, walifika katika makazi ya Gavana wa Meru Kawira Mwangaza mnamo Jumamosi ambapo wamechukua sampuli kusaidia katika uchunguzi wa kifo cha bloga Daniel Muthiani almaarufu ‘Sniper’.

Maafisa hao wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) waliweka utepe wa kuzingira makazi hayo yaliyo katika mtaa wa kifahari wa Milimani, Meru.

Mkurugenzi wa kuchunguza uhalifu wa mauaji Martin Nyaguto aliwaongoza maafisa hao kuzuru kila sehemu ya makazi hayo kufanya upekuzi wao.

Maafisa wameonekana wakiingia na kutoka kwa makazi hayo, japo DCI haikufichua ni aina gani ya ushahidi ambao walikuwa wakitafuta.

Mshirikishi wa DCI kanda ya Mashariki Bw Lenny Kisaka amesema makachero walikuwa wakitafuta ushahidi ambao utakuwa wa umuhimu mkubwa wanapoendelea kuchunguza mauaji ya bloga huyo ambayo yalishtua nchi nzima.

Bw Kisaka amesema watafanya upelelezi katika sehemu nyinginezo.

“Tunafanya uchunguzi kuhusu mauajin ya mtu aliyefahamika kama ‘Sniper’ na tumekuwa katika sehemu mbalimbali. Tuna timu ya wataalamu kutoka nyanja mbalimbali wenye uwezo wa juu kufanya uchunguzi wa kisayansi,” Bw Kisaka amewaambia wanahabari.

Katibu wa Kaunti ya Meru Dkt Kiambi Athiru amekuwepo wakati wa shughuli hiyo akisema “nimeletwa kusaidia” timu ya makachero kufika katika sehemu mbalimbali ambazo walitaka kuzifikia.

Upekuaji huu unajiri siku mbili tu baada ya makachero kumkamata kaka ya gavana, Bw Murangiri Kenneth Guantai ambaye anazuiliwa na kuhojiwa jijini Nairobi kuhusiana na mauaji hayo ya kinyama.

Vitengo vya uchunguzi viliomba kuendelea kumzuilia, pamoja na washukiwa wengine watano, kwa siku 21 kukamilisha uchunguzi.

Ombi liliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu ya Kiambu mnamo Ijumaa kwamba Mbw Kenneth Mutua Matiri, Fredrick Muriuki Kiugu, Frankline Kimathi, Timothy Kinoti, na Guantai wazuiliwe kwa siku 21 katika kituo cha polisi cha Muthaiga hadi uchunguzi ukamilike.

Bw Guantai  ni mmojawapo wa maafisa wa usalama wa gavana Mwangaza, naye Bw Matiri ni afisa wa itifaki katika ofisi ya gavana.

DCI, katika ombi lake, inadai, washukiwa walimuita Muthiani kwa mtego wa kifo chake, kwa kisingizio kwamba walitaka akutane na Bi Mwangaza.

Mshukiwa mwingine ni Bw Vincent Murithi Kirimi ambaye inadaiwa ndiye alikuwa wa kwanza kumpigia Muthiani simu.

Kikao cha kusikiliza ombi hilo kinatarajiwa Jumatatu.

Muthiani, almaarufu ‘Sniper’, alitoweka mnamo Desemba 2, 2023, lakini baadaye mwili wake ukapatikana katika kichaka karibu na kingo za Mto Mutonga katika kaunti jirani ya Tharaka Nithi mnamo Desemba 16, 2023.