Habari za Kitaifa

Kijana aliyetoweka wakati wa maandamano apatikana ndani ya choo amekufa


MWANAMUME ambaye alitoweka wakati wa maandamano dhidi ya serikali Julai 17 katika Kaunti ya Nairobi alipatikana ndani ya choo akiwa amekufa.

Mwili wa Frankline Ondwari, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, ulipatikana ukiwa umening’inia ndani ya choo ambacho hakitumiki katika mtaa wa Ngumo.

Marehemu Ondari ambaye atazikwa Jumatano hii alipatikana siku moja tu baada ya gazeti la Daily Nation kuchapisha habari kuhusu kutoweka kwake.

Siku ambayo alitoweka, Bw Ondwari aliwaambia wanafamilia wake kuwa alikuwa amekamatwa na alikuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, Nairobi.

Mamake Dyline Sabina kwenye mahojiano na Taifa Leo awali alisema kuwa mwanawe alikuwa amekamatwa na alipopiga simu ilipokelewa na mtu ambaye alijitambulisha kama afisa wa polisi.

Mtu huyo alimwambia kuma mahabusu hawaruhusiwi kuwa na simu.

Uchunguzi uliofanyiwa mwili wake na mwanapatholojia huru ambaye alipewa kazi hiyo na familia ulionyesha kuwa Bw Ondwari alinyongwa. Taifa Leo pia ina picha ambazo zilipigwa kwenye choo ambacho mwili wake ulipatikana.

Bi Sabina alieleza Taifa Leo kuwa baada ya kuongea na mtu huyo aliyejitambulisha kama afisa, mmoja wa marafiki wa mwanawe alimpigia simu na kusema polisi walikuwa wakiitisha Sh3,000 ili wamwachilie Bw Ondwari. Alituma pesa hizo kwa nambari ya simu ya mwanawe.

Edith Nyangarisa, dadake marehemu Ondwari alisema aliongea na nduguye siku ambayo alitoweka na hata akamwambia alikuwa kwenye mchakato wa kuachiliwa na polisi.

“Alisema atanipigia akifika nyumbani kwa sababu walikuwa wakielekea kumwachilia,” akasema Bi Nyangarisa.

Emmanuel Inyiega, rafiki wa karibu wa marehemu alisema Bw Ondwari aliacha simu yake kwa rafikiye katika barabara ya Kirinyaga, Nairobi ambako aliacha ikipata chaji.

“Nilienda katika kituo cha polisi na nikaambiwa ameachiliwa. Hata baada ya kumkosa nilirejea katika kituo hicho na nikaambiwa hakuwa huko,” akasema Bw Inyiega.

Kwa wiki mbili familia ya Bw Ondwari ilimsaka sehemu mbalimbali lakini hawakumpata. Walimtafuta katika vituo mbalimbali vya polisi, mochari, hospitali na walipiga ripoti kuhusu kutoweka kwake katika kituo cha polisi cha Kasarani.

Mara ya mwisho Bw Ondwari alikuwa na mamake ni mnamo Disemba 2023 nyumbani kwao Keumbu, Kaunti ya Kisii. Amerejelewa kama mtu mtulivu ambaye alipenda sana kujumuika na marafiki.

Familia ya Purity Njeri ambaye alitoweka mnamo Julai 11 bado haijampata huku mamake Ruth Nduta kutoka Gatanga Kaunti ya Murang’a akisema hajui kama mwanawe yuko hai.

Shelmith Nyawira Njiru, mwanamke ambaye alitoweka Julai 17, 2024 naye alipatikana Uganda ambapo inadaiwa alitelekezwa na watu waliokuwa wamemteka nyara.