Habari za Kitaifa

Korti ilivyosambaratisha njama za polisi kumnyaka Wanjigi

Na RICHARD MUNGUTI August 10th, 2024 1 min read

MAHAKAMA kuu imezima Polisi kumkamata na kumshtaki kiongozi wa Chama cha kisiasa cha Safina Jimi Wanjigi.

Na wakati huo huo Jaji Bahati Mwamuye aliwaagiza polisi wamwachilie mara moja Wanjigi endapo walifaulu kumkamata baada ya kupiga kambi katika makazi yake katika mtaa wa kifahari Muthaiga usiku wa Agosti 8,2024.

Jaji Mwamuye alitoa maagizo hayo baada ya Wanjigi kuwasilisha ombi katika mahakama kuu akiomba korti isambaratishe hatua za polisi za kumkamata na kumshtaki kwa kumili silaha hatari.

Wakili Nelson Osiemo aliwasilisha kesi dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin akisema “wametisha kumkamata Wanjigi.”

Bw Osiemo alieleza mahakama kwamba polisi walimwandama Wanjigi kutoka kati kati mwa jiji Agosti 8 baada ya kushiriki katika maandamano ya Nane Nane hadi katika makazi yake mtaani Muthaiga.

“Polisi walidai kwamba walipata grunedi nne zikiwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba yake,” Bw Osiemo alimweleza Jaji Mwamuye.

Wakili huyo alisema “Jimi Wanjigi kamwe hajui chochote kuhusu grunedi nne zilizokuwa kwenye gari lililokuwa nje ya makazi yake.”

Mahakama ilielezwa Wanjigi anahofia polisi watamkamata na kumzuilia kwa makosa asiyoyajua.

Bw Osiemo alisema hati za mlalamishi zitakandamizwa endapo mahakama haitazima hatua ya polisi kumshika.

Akitoa uamuzi Jaji Mwamuye alisema ametathmini kwamba huenda haki za mlalamishi (wanjigi) zikakandamizwa iwapo polisi watamkamata na kumzuilia bila kumweleza sababu.

Jaji huyo aliamuru kesi hiyo itajwe Agosti 16, 2024 kwa maagizo zaidi.