Habari za Kaunti

Lamu: Wanaowapa wendawazimu taka kutupa ovyo mjini waonywa

February 2nd, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MANISPAA ya kisiwa cha Lamu imeanzisha msako wa wakazi ambao wanadaiwa kuwabebesha wendawazimu na watu wenye matatizo ya kiakili mifuko iliyojaa taka kuenda kuwatupia.

Meneja wa Manispaa ya Lamu Abdulswamad Abdalla anasema wengi wamekuwa wakifanya hivyo kama njia mojawapo ya kuepuka gharama inayofungamana na utupaji taka mjini.

Katika mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake Alhamisi, Bw Abdalla alisema ipo haja ya wakazi kutii sheria zinazofungamana na ukusanyaji na utupaji taka zilizowekwa mjini, akisisitiza kuwa wanaokaidi sheria hizo watakiona cha mtema kuni.

Bw Abdalla aliweka wazi kuwa hatua ya kuwapa wendawazimu magunia yaliyojaa taka kwenda kutupa imeishia kuwacha taka hizo zikitupwa kwenye maeneo yasiyostahili.

“Kumpa mpungufu wa akili au mwendawazimu taka kuenda kuzitupa huko ni kukosa kuwajibika. Tumeweka mikakati kabambe, ikiwemo kujenga vibirika kwenye baadhi ya mitaa ili watu wakusanye taka huko. Tingatinga zetu za kukusanya taka pia zimekuwa zikizunguka kila mtaa kukusanya taka. Sioni sababu ya watu kuishia kuwapa taka wendawazimu. Tunachunguza na tukikupata tutakuchukulia hatua,” akasema Bw Abdalla.

Meneja wa Manispaa ya Lamu Abdulswamad Abdalla. Amewaonya wanaowapa wendawazimu taka kuenda kuzitupa kisiwani Lamu akisema hatua hiyo huishia taka kutupwa pasipofaa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Afisa huyo alisema serikali ya kaunti, kupitia kwa gavana, Issa Timamy na ofisi yake imejizatiti vilivyo kuurembesha mji wa kale wa Lamu na ule wa Shella, ambayo yote ni ngome za watalii wanaozuru eneo hilo.

“Tuna mpango kwamba hivi karibuni tutatundika mikebe maalum ya kukusanyia taka kwenye barabara, vichochoro na vishoroba vya miji yote mikuu ya Lamu, ikiwemo mji wa kale wa Lamu, Shella, Mpeketoni, Hindi, Witu, Mokowe, Faza, Kizingitini, Kiunga na kwingineko. Azma hii inalenga kuinua hadhi na usafi wa miji yetu,” akasema Bw Abdalla.

Afisa huyo pia amewaonya wale wenye hulka ya kuamka usiku wa manane na kubeba taka kuzirusha kwenye ufuo au ndani ya Bahari Hindi mjini Lamu.

Alisema kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya viumbe hai baharini.

Kauli yake inajiri wakati ambapo wanamazingira wamekuwa wakijitokeza kila mara kuwarai wananchi kuepuka kutupa taka za plastiki baharini kuzuia uchafuzi wa mazingira ya viumbe wa baharini.