Makala

Maadui wa elimu? Wenye matatu walaumiwa kwa kupandisha nauli

May 16th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

WADAU katika sekta za elimu, usalama na biashara wameteta kuhusu hatua za wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma kuwa na mazoea ya kulenga wanafunzi na nauli za juu shule zikifungwa na kufunguliwa.

Wakati wanafunzi wanapoelekea nyumbani baada ya muhula kuisha, wakifungua na pia katika safari za likizo ndogo, magari hayo hupandisha nauli kwa hata asilimia 200.

“Sielewi ni tamaa, ulafi au utundu tu wa madereva na makondakta,” akasema Kamishna wa Mombasa Bw Mbogo Mathioya.

Bw Mathioya alisema mtu aliyekomaa kiumri na anajua nafasi ya watoto katika jamii, hafai kuwalenga wanafunzi na nauli za juu.

Aidha, Bw Mathioya aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu “japo unaweza ukasema kwamba wanafunzi hao huwa na wazazi ambao wanawafadhili na eti kwamba sio wanafunzi hulengwa, lakini taswira ni kwamba mazoea yao kupandisha nauli kiholela huifanya elimu kuwa na gharama za juu”.

Mshirikishi wa Muungano wa Walimu wa Murang’a Kusini Bw John Njata alisema kwamba kuna wazazi ambao hungojea mshikemshike wa usafiri wa wanafunzi upungue kwa kuchelewesha watoto wao nyumbani.

Alisema kwamba watoto wengi huchelewa kufungua shule wazazi wao wakingojea nauli za kawaida zirejelewe hali ambayo huwapata wanafunzi hao wakikaa nyumbani kwa wiki moja zaidi.

“Katika hali hii, mwanafunzi akifika shuleni huwa amechelewa na hata wakati mwingine huwa amebaki nyuma kielimu,” akasema Bw Njata.

Pale ambapo wazazi huwa hawana budi kuchukua mikopo au kugeuka kuwa ombaomba ni siku ya kufunga shule kwa kuwa ni lazima mtoto afike nyumbani.

Bw Njata aliwataka wahudumu wa matatu wakome kiujiangazia kama watu ambao huwa na kinyongo na wanafunzi wakipata elimu hivyo basi kuzindua njama za kuwatatiza ndio wakae nyumbani katika lindi la ujinga.

“Kuna taswira kwamba wengi walio katika biashara za matatu wakiwa wahudumu au wawekezaji ni wale ambao hawakuenda mbali sana kielimu na hivyo basi huwa na kisasi dhidi ya elimu ya watoto wa wenyewe,” akadai Bw Njata.

Msanii Kareh B ambaye hivi majuzi alimpoteza mtoto wake katika ajali ya barabarani alopokuwa akisafiri usiku kurejea nyumbani baada ya shule kufungwa alisema kwamba “hakuna ukatili mkuu kama wa kuweka pesa mbele kuliko maisha na kesho njema ya mtoto”.

“Mtoto wangu alipakiwa kwa basi usiku wa manane kwa kuwa wahudumu walikuwa wakikimbizana na pesa na kisha usimamizi wa shule aliyokuwa akisomea ulikuwa mshirika wa mchezo huo wa pesa… matokeo ni kwamba mtoto wangu hakuwahi kufika nyumbani, aliaga dunia na nishamzika,” alilalama Kareh B.

Mwanakamati katika muungano wa Wamilki Matatu Nchini Bw Micah Kariuki alisema kwamba ni hali ya kibiashara kwa kuwa “hata sisi huwa na watoto na huwa wanalipishwa nauli hizo za juu na matatu hizo zetu”.

Alisema kile huchangia nauli hizo za juu sio ukatili au ulafi bali ni msukumo wa kibiashara ambao kwa kawaida, hujitokeza katika kila safu ya harakati za uchumaji wa mali.

“Mkilalamika kutuhusu, msisahau kusema hata wauzaji wa sare za shule, wauzaji wa vitabu na wauzaji wa viatu pia huongeza bei zao shule zikifunguliwa. Msisahau kwamba hata wakati wa msimu wa Krisimasi, maduka ya nguo za watoto huongeza bei. Biashara hizo zote humilikiwa na wazazi wa watoto ao hao. La mno, msisahau ya kwamba wakati biashara iko chini na kwa steji hakuna abiria, ninyi hupiga bei shoka kwa zaidi ya asilimia 30,” akajitetea Bw Kariuki.

Lakini Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi alisema kwamba kuleta mijadala ya kani za kiuchumi katika masuala ya watoto, ni kupotosha mada kuu ya hali ilivyo.

Alisema taifa hili linafaa likome ule ulafi na tamaa kwa kuwa hata hali sio mbaya vile kama inavyosemwa lakini tabia za baadhi ya Wakenya kukimbizana na faida zilizopitiliza ndio hutatiza uchumi wa wengi kufinyika kimfuko.

“Tulikuwa katika zile enzi zetu za miaka ya sabini hadi tisini (1970s hadi 1990s) tukichunga masilahi ya watoto. Dereva aliyekuwa akibeba wanafunzi hata angejitolea kuwafikisha watoto hadi shuleni bila ada za nyongeza badala ya kuwaweka kwa steji. Watoto walikuwa wa kila mzazi mtaani na masilahi yao yalikuwa yakichungwa kikamilifu. Leo hii hata wamiliki wa magari ya kibinafsi hawajitolei kubeba wanafunzi waliokwama kwa steji,” akasema Bw Murungi.

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya aliambia Taifa Leo kwa njia ya ujumbe wa WhatsApp kwamba “utapata mzazi ana gari lililo na nafasi nyingine 10 na amebeba mtoto wake pekee akimpeleka shuleni”.

“Barabarani anawaacha watoto wanaoelekea katika shule iyo hiyo anayompeleka huyo mtoto wake kwa kuwa hao sio wake. Tuko na shida katika hizi bongo zetu na tunajidhania kuwa wangwana,” akasema gavana Natembeya.

Bw Natembeya alisema “hata tupenyeze ubunifu gani wa usomi na ujeuri katika huo mjadala, hali katika ukweli mtupu ni kwamba kufanya biashara na watoto ni ulafi ulio na ukatili kuliko shambulio la fisi”.

[email protected]