Habari za Kitaifa

Madereva wa teksi wafurahia nyongeza ya malipo

Na FRIDAH OKACHI August 24th, 2024 1 min read

KAMPUNI ya teksi inayotumia apu, Pan-African Super, imeongeza malipo kwa madereva kwa asilimia 15.

Hatua hii inalenga kuwawezesha madereva kukabili gharama ya juu ya maisha.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, madereva wa teksi kidijitali wamekuwa katika migomo ya mara kwa mara, wakilalamikia malipo duni kutoka kwa kampuni hiyo.

Migomo hiyo imeshinikiza Little ya Pan-African Super kuongeza viwango vya nauli kwa asilimia 15, ili kuwasaidia madereva kukabiliana na changamoto za kiuchumi wanazokumbana nazo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Little Bw Kamal Budhabhatti, alisema viwango hivyo vitawezesha madereva kupata mshahara unaostahili na pia kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, rahisi na salama.

“Tumesikiliza maombi yao na kujali malalamishi yaliyotolewa. Uamuzi huo, utawezesha madereva wetu kufurahia wanapotoa huduma za usafiri.  Tunaamini ni muhimu kuwasaidia wanaotumia mtandao wetu,” alisema Bw Budhabhatti.

Kulingana na mkurugenzi huyo, Asilimia hiyo 15, itakuwa na athari kwa wateja wa usafiri.

“Ongezeko hilo linamaanisha wateja wetu watalipia zaidi ikilinganishwa na hapo awali. Lakini, pia itahakikisha kutolewa kwa huduma bora zaidi na zinazotegemewa. Dereva mwenye furaha siku zote atatoa huduma bora,” aliongeza Bw Budhabhatti.

Hatua hiyo ilipokelewa vyema na madereva, wakisema matatizo yao kama vile kulipa kodi ya nyumba na familia yatapungua.

Teksi ikisubiri mteja. PICHA | FRIDAH OKACHI

Madereva wafurahi

Mwenyekiti wa wahudumu wa teksi Kaunti ya Nairobi Alutalala Wycliffe, alisema viwango hivyo ni vya nafuu na yenye matumaini kwa kuboresha kazi yao.

“Asilimia 15 inamaanisha kuwa kampuni hiyo imeongeza Sh40 kwa kiwango cha chini cha malipo kutoka kwa mteja. Awali kiwango cha chini kilikuwa Sh180, hivi sasa mteja atalipa Sh220,” alisema Bw Alutalala.

Bw Alutalala alisema baadhi ya madereva walikuwa wakiwaomba wateja wao kuwaongezea malipo, tukio ambalo linawakera.

“Wakati mwingine tulilazimika kuuliza wateja, bei ya malipo kwenye apu yao ni ngapi. Ukiambiwa, unamwomba kubatilisha ombi,” aliongeza.