Habari

Mahakimu wasiadhibiwe kwa kufanya kazi yao – Jaji

August 31st, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAJAJI na mahakimu hawafai kuadhibiwa kwa kutekeleza majukumu yao, Mahakama Kuu imeamua.

Jaji Byram Ongaya alitoa uamuzi huo alipomrudisha kazini hakimu mkazi wa Kiambu Bryan Khaemba aliyesimamishwa kazi kwa kutoa agizo Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mkewe Susan wasikamatwe.

Kwa mujibu wa uamuzi huo hakuna hakimu ama jaji atakayesimamishwa kazi au kuchukuliwa hatua ya kinidhamu kwa kutekeleza jukumu lake kisheria.

Chama cha Mahakimu na Majaji nchini (KMJA) kilifurahishwa na uamuzi huo wa Ijumaa jioni na kusema ulitia moyo na sasa mahakimu na majaji watafanyakazi yao pasipo woga kwa vile sheria inawatetea.

Katibu mkuu wa KMJA, Derrick Kuto, alisema uamuzi huo ulipokewa kwa furaha na umeimarisha utendakazi wa mahakimu na majaji.

Katika uamuzi wa kihistoria uliosomwa kwa zaidi ya saa nne, mahakama iliamuru Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kupitia Mwanasheria Mkuu ifanyie marekebisho sheria zake kuepuka ukandamizaji wa haki za mahakimu na majaji.

Jaji Ongaya alisema ni kitendo cha kudunisha kabisa na kuvunja moyo wa hakimu ama jaji kutimuliwa kwa kufanya kazi aliyoajiriwa kuifanya.

“Sheria za JSC zifanyiwe marekebisho ndipo mahakimu na majaji wasiwe wanateswa na kudhulumiwa kwa kufanya kazi yao,” alisema Jaji Ongaya.

Alisema sheria za JSC hazitoi mwelekeo wa utendaji kazi wa mahakimu na kulitaka bunge lifanyie marekebisho baadhi ya sheria zinazothibiti utenda kazi wa mahakimu.

Aamuru arudi kazini

Jaji Ongaya alifutilia mbali uamuzi wa kusimamishwa kazi Bw Khaemba na kuamuru arudi kazini kufikia Septemba 9, 2019.

Pia aliamuru alipwe mishahara yake yote na marupurupu kabla ya Novemba 1, 2019.

Hakimu huyo alisimamishwa kazi na Jaji Mkuu David Maraga kwa kutoa maagizo ya kutokamatwa kwa Bw Waititu, mkewe Susan na washukiwa wengine kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Hata hivyo, Jaji Ongaya alimtetea Jaji Maraga akisema hakuwa na kinyongo wala hila au husuda akimsimamisha kazi Bw Khaemba kwa vile alikuwa akitekeleza kazi yake kama kiongozi wa idara ya mahakama.

Alisema kuwa haki za Bw Khaemba zilikandamizwa kwa kuagizwa akae nyumbani bila kupokea mshahara ama marupurupu yoyote ila hakuwa amefutwa kazi.

Katika barua aliyopokea Juni 13 , 2019, Bw Khaemba aliamriwa aende nyumbani kusubiri uamuzi wa jopo la kuchunguza mienendo yake.

“Sheria ya JSC inasema hakimu ama jaji akisimamishwa kazi anatakiwa kupewa asilimia fulani ya mshahara wake pamoja na marupurupu ya hospitali,” alisema Jaji Ongaya.

Jaji huyo alisema JSC haijatenga kiwango cha pesa ambazo hakimu au jaji aliyesimamishwa kazi anapasa kuwa akipokea.

“Jaji Mkuu Maraga alichukua hatua ya ghafla alipopokea taarifa kwamba Bw Khaemba hakuwa kazini alipotoa maagizo katika ombi alilowasilisha Bw Waititu kupinga hatua ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka,” alisema Jaji Ongaya.