Habari za Kitaifa

Majangili wameangamiza watu 300, maafisa wa usalama wakilaumiwa ‘kukodisha’ silaha – Ripoti  

Na STEVE OTIENO September 7th, 2024 2 min read

MAJANGILI na wezi wa mifugo wamehusika na vifo vya zaidi ya watu 300, kujeruhi maelfu na kuharibu mali ya mamilioni ya pesa katika uvamizi ambao wamekuwa wakitekeleza katika kaunti kadhaa tangu 2023, utafiti mpya unaonyesha.

Ripoti hii yenye kichwa ‘Kudhibiti Wimbi Hatari La Wizi Wa Mifugo Na Ujangili Nchini Kenya,’ iliyoandaliwa na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC), inaonyesha kuwa kuna kupungua kwa thamani ya maisha ya binadamu na wimbi jipya la ujangili na wizi wa mifugo ikilinganishwa na siku za nyuma.

Utafiti huo ulifanywa katika kaunti 13 za Baringo, Elgeyo Marakwet, Isiolo, Kitui, Laikipia, Marsabit, Meru, Samburu, Turkana, Pokot Magharibi, Tana River, Kisumu na Nandi.

Kila kaunti ilionekana kuwa na changamoto za kipekee zinazoiathiri kuhusiana na tishio la ujangili na wizi wa mifugo.

Uovu huu unaendelea kuathiri mamilioni ya Wakenya, wengi wao wanaoishi katika maeneo kame Kaskazini mwa nchi licha ya mabilioni ya pesa kutengwa na serikali kukabiliana nao.

Tofauti na siku za nyuma ambapo nia ya wizi wa mifugo kwa kiasi kikubwa ilikuwa, ‘mtindo wa kitamaduni uliopangwa’ imegeuza kuwa biashara na ‘uhalifu uliopangwa,’ ripoti hiyo inaeleza.

Pia, kuna kuongezeka kwa silaha haramu ndogo ndogo ambazo zikiambatana na kiwango cha juu cha kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa vijana katika maeneo ya wafugaji, mazingira magumu ya kiuchumi na umaskini, vinachangia kuzidisha hali ambayo tayari ni mbaya katika kaunti zilizoathiriwa.

“Wauzaji wakuu wa bunduki zinazotumiwa katika wizi wa mifugo na mashambulizi ya majangili waliripotiwa kuwa wasambazaji wa silaha katika mpaka wa Kenya, wakifuatwa na wafanyabiashara wandani na wanasiasa,” utafiti unasema.

Kwa kiasi kikubwa, visa vinavyoendelea vya ujangili na wizi wa mifugo vimehusishwa na ufisadi na ukosefu wa uadilifu miongoni mwa maafisa wa umma.

Kituo cha Kikanda cha kuthibiti Silaha Ndogo Ndogo kinahusisha ongezeko la silaha ndogo ndogo kutoka nchi jirani na ufisadi unaotekelezwa na mashirika ya usalama mpakani.

Maafisa fisadi wa usalama pia wanatuhumiwa kuendeleza uhalifu huo kwa “kukodisha silaha zao kwa wezi wa mifugo, huku wanajeshi wa Kenya na Ethiopia na maafisa wa polisi wakishutumiwa kwa kutoa silaha zao kwa wapiganaji wafanye uvamizi,” sehemu ya ripoti hiyo inasema.

Maafisa hao wanafanya hivyo kwa lengo la kujipatia fedha za haraka kwa kutumia silaha wanazozipata kihalali kama wanavyofanya baadhi ya Polisi wa Akiba wa Kitaifa wanaotumwa katika maeneo haya kuwa wa kwanza kudumisha usalama kwa kukabiliana na majangili na wezi wa mifugo.

Maendeleo ya kiteknolojia pia yamefanya wahalifu hao kubadilisha mbinu, hali na sasa wanatumia simu zao za mkononi kupanga, kuvamia na kuharibu miundombinu iliyojengwa, ikiwemo shule.