Makala

Mapenzi yanoga tena kwa wanandoa baada ya kazi za mikoko kurejeshwa

February 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

MIAKA sita tangu marufuku ya kukata mikoko ilipoondolewa na serikali ya Kaunti ya Lamu, mapenzi miongoni mwa wanandoa waliokuwa wametalikiana punde waume wao walipopoteza ajira kufuatia marufuku hiyo sasa yamenoga.

Mnamo Februari 24,2018, serikali kuu kupitia kwa wakati huo, Naibu wa Rais, William Ruto, ilitangaza marufuku ya kukata miti, ikiwemo mikoko kote nchini.

Hatua hiyo ilichukuliwa kama njia mojawapo ya kutunza mazingira na kuhifadhi misitu na maeneo ya chemichemi yaliyokuwa kwenye hatari ya kuangamia kufuatia ukataji kwa wingi wa misitu uliokuwa ukiendelezwa na Wakenya kote nchini.

Tangazo hilo lilikuwa kama kisirani, hasa kwa familia nyingi za Lamu ambazo kitega uchumi chao cha kipekee ni kukata miti ya mikoko, kuuza na kujipatia mtaji wa kukimu maisha yao.

Sekta ya mikoko, Kaunti ya Lamu imeajiri zaidi ya familia 30,000 za eneo hilo, nyingi ya hizo zikiwa ni zile zipatikanazo visiwa vya Lamu, Ndau, Mkokoni, Manda, Matondoni, Kipungani, Kiwayu, Kiunga na viungani mwake.

Marufuku hiyo ilidumu kwa karibu mwaka mmoja, kipindi ambacho kilishuhudia ndoa nyingi zikivunjika na familia kusambaratika si haba.

Sehemu mojawapo ya msitu wa mikoko Lamu.
Picha|Kalume Kazungu

Wanaume wengi kitumbua kiliingia mchanga punde marufuku ya mikoko ilipoamriwa kwani walipoteza wake zao waliowatoroka kwa kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.

Kuna wanaume wengine ambao pia walitoroka wake zao na watoto, hivyo kuachia majukumu yote akina mama, hasa baada ya kushindwa kustahimili kelele za kila siku majumbani kutoka kwa mabibi zao kutokana na kufeli kufadhili mahitaji ya nyumba kwa kukosa kazi.

Kwa jumla, wanaume walipoteza vipenzi vyao vya rohoni ilhali wanawake kwa upande mwingine wakiachiwa majukumu yote ya kulisha familia wanaume wakitelekeza majukumu ya nyumbani.

Yaani, kila upande kulisheheni msongo wa mawazo.

Cha kufurahisha hata hivyo ni kwamba licha ya yote kutukia, mwanga wa matumaini ulirejea mwaka mmoja baadaye pale serikali kuu kupitia kwa Afisa Mkuu wa Masuala ya Uhifadhi katika Shirika la Huduma za Misitu nchini (KFS), Bi Muthoni Munyasia alipozuru Lamu mnamo Februari 19,2019, ambapo alitangaza kuondolewa kwa marufuku ya kukata mikoko kote Lamu.

Bi Munyasia aidha aliweka wazi mikakati ya serikali itakayohakikisha wakazi wa Lamu wanavuna mikoko katika hali endelevu na yenye kunawirisha msitu wa mikoko licha ya ukataji utakaoendelea.

Tangazo hilo lilileta raha kwa wakazi wengi wa Lamu, ikiwemo vijana, akina baba na akina mama kwani walijua fika kuwa angalau kazi au vibarua vyao vya kukata na kuuza mikoko kukimu mahitaji ya kimaisha vimerejea.

Katika mahojiano na Taifa Leo Ijumaa, Mwenyekiti wa Miungano ya Kijamii ya Kukata na Kuhifadhi Mikoko, Kaunti ya Lamu, Bw Abdulrahman Aboud, alikiri kuwa tangu marufuku hiyo kuondolewa Lamu karibu miaka sita iliyopita, wapenzi wengi waliokuwa awali wameachana walirudiana na kusameheana, hivyo kunogesha huba si haba.

Bw Aboud aliishukuru serikali kuu kwa kuwaamini wakazi wa Lamu na kuwaondolea marufuku ya kukata mikoko, akiitaja hatua hiyo kuwa kikombozi cha ndoa nyingi zilizokuwa tayari zimesambaratika.

Alieleza kuwa mikoko ni rasilimali muhimu kwa jamii ya Lamu kwani mja akitaka kujenga, kutengeneza boti na mashua au fanicha za kurembesha sebule lazima atumie mikoko.

Kulingana na Bw Aboud, mikoko ndio kusema kwa jamii ya Lamu akisisitiza kuwa uvunaji wa mikoko ni biashara iliyoajiri maelfu ya familia Lamu.

“Ni biashara iliyoanza tangu jadi wakati wa mababu zetu. Kupiga marufuku biashara hiyo kulimaanisha familia zote zaidi ya 30,000 zinazotegemea biashara ya mikoko ziliachishwa kazi. Hii ilileta migogoro mingi kwa familia, hivyo wanandoa wengi wakaishia kuachana. Watoto nao walihangaika. Twashukuru tangu marufuku kuondolewa, walioachana walirudiana kuendeleza maisha. Mambo kwa sasa ni nywee. Migogoro kati ya bwana na bibi nyumbani imepungua pakubwa,” akasema Bw Aboud.

Bi Husna Lali, mmoja wa wawekezaji wakuu katika biashara ya mikoko kisiwani Lamu, alisema ni kupitia kitega uchumi hicho ambapo wameweza kujipatia fedha za kusomeshea watoto, kulipia kodi ya nyumba, matibabu, chakula na mahitaji mengine ya maisha.

Bi Husna Lali, mmoja wa wanabiashara wawekezaji wakuu wa biashara ya mikoko kisiwani Lamu. Picha|Kalume Kazungu

Bi Lali alikiri kuwa mwaka mmoja wa marufuku ya mikoko ulikuwa jehanamu kwao kwani mambo mengi, ikiwemo masomo ya watoto wao yalisimama.

Anasema kwa sasa maisha ni raha mustarehe kwani biashara inazidi kunoga kila kukicha.

“Kupitia ukataji na uuzaji mikoko, sisi tumefaulu kujipanga vilivyo kimaisha. Unajua kukicha utafika bandarini kuuza mikoko na kupata mtaji wa kujikimu,” akasema Bi Lali.

Ahmed Omar, mmoja wa vijana ambaye aliyejiajiri kupitia mikoko anawasihi vijana wenza kujituma maishani badala ya kusubiri kazi za kuajiriwa.

“Mimi nimesoma na niko na digrii yangu. Badala ya kusubiri kuajiriwa, nimejiingiza mzimamzima kwenye biashara ya mikoko na ni mwaka wa tatu sasa. Biashara ni nzuri. Ni kujituma,” akasema Bw Omar.

Wanajamii wa Lamu tangu jadi wamesifika kwa kuendeleza hulka ya kuhifadhi mazingira, hasa mikoko, ikiwemo kuendeleza mara kwa mara upanzi wa miche ya mikoko kila wanapovuna miti hiyo.

Ikumbukwe kuwa kati ya asilimia 100 ya msitu wa mikoko nchini, karibu asilimia 65 hupatikana kaunti ya Lamu.