Bunge yageuka paradiso ya walafi
HATUA ya wabunge na maseneta kujiongezea posho zao za usafiri kupitia marekebisho ya marupurupu kwa kima cha jumula cha Sh4.4 bilioni imesawiri bunge kama paradiso la walaghai wanaojijali huku raia wakiendelea kuteseka kutokana na gharama ya juu ya maisha.
Habari hizi ziliwasha moto wa hasira na kejeli mitandaoni huku raia wakiwataja wabunge kama matapeli wakuu wanaotumia mamlaka yao ya uwakilishi kujinufaisha.
Katika kile kinachoonekana kuwa sehemu ya mchakato wa kisiasa ulioendeshwa kimya kimya, hakuna taasisi ya umma iliyojitokeza kueleza kilichoendelea. Na hata zaidi, wananchi waliokuwa na uelewa finyu au waliokata tamaa walitetea hatua hiyo kwa kusema marekebisho hayo si nyongeza ya mishahara.
Lakini kwa mtumiaji mmoja wa mtandao wa X (zamani Twitter) aliyekuwa na hasira, hili sio jambo la mzaha.
“Wabunge wetu wanaongeza posho huku bei ya unga ikipanda kila wiki. Hii Kenya si ya wananchi tena, ni paradiso ya matapeli wa kisiasa!” aliandika @Biko_Mkenya.
Mtumiaji mwingine wa Facebook aliandika:“Sisi wa Ugunja hatujui hata mbunge wetu ni nani kwa sasa, lakini maisha yanaendelea tu. Hawa watu hawafai.” – Maureen Atieno via Facebook.
Wachambuzi wa siasa na wataalamu wa utawala wanakubaliana na raia kuwa katika mfumo wa ugatuzi, viti vya Wawakilishi wa Wadi, Mbunge, Seneta na Mwakilishi wa Wanawake zimepoteza maana na umuhimu wake nchini.
“Hali imekuwa mbaya chini ya utawala wa sasa, Viti hivi havina maana kwa mwananchi wa kawaida. Hizi ni nyadhifa ambazo zimegeuzwa kuwa ngazi za kujitajirisha, sio kutetea raia na kufanya serikali iwajibike,” asema mchambuzi wa siasa Joseph Kiilu.
Anasema badala ya kutekeleza majukumu yao baada ya kuchaguliwa, wanasiasa wengi hujiingiza katika miradi ya binafsi na vita vya kuwania minofu.
“Wakati umefika tuanze kuzungumza kwa uwazi: mabunge ya kaunti na kitaifa yamekuwa paradiso ya matapeli. Nyadhifa za kuchaguliwa zimegeuzwa kuwa fursa za kufanya biashara na kulaghai raia badala ya majukwaa ya kuhudumia umma,” aeleza Kiilu na na kuongeza kuwa hii ndiyo sababu bunge limetekwa na serikali kuu.
Kuanzia Aprili 1, 2025, Wabunge wanatarajiwa kupokea nyongeza ya posho ya Sh 366,011 kwa mwezi kama sehemu ya malipo mapya ya kusafiri kwa magari yao kila mwezi. Hatua hii imeibua hasira mitandaoni huku Wakenya wakijiuliza ni vigezo gani vilivyotumika kuidhinisha ongezeko hilo katika taifa linalopambana na matatizo ya kiuchumi.
“Kila Mbunge sasa atapata mshahara wa ziada wa Sh366,000 kuanzia Aprili 1, 2025, kama posho kila mwezi. Hii inamaanisha mzigo wa Sh4.4 bilioni kwa mlipa ushuru kila mwaka, juu ya mshahara wao wa Sh739,600 uliowekwa na SRC,” alisema Moe, mchanganuzi wa masuala ya kiuchumi akiandika katika X.
Hasira ya umma imeendelea kuelekezwa kwa Bunge kwa kutoonyesha huruma kwa hali ya uchumi wa mwananchi wa kawaida, huku gharama ya maisha ikiwa juu, bei ya bidhaa za kimsingi ikipanda kila mara, na huduma za umma zikiwa duni.
“Hakuna hela ya kulipa madaktari, hakuna hela za elimu, lakini kuna hela za kufidia wabunge kwa safari katika maeneo wanayowakilisha? Kenya ni kama mtaa wa wadosi wachache.” – @KenyaFurious.
Hatua ya wabunge inajiri wakati ambao serikali imekiri kuwa itabidi kukopa zaidi ili kulipa madeni hali ambayo inafanya ongezeko la posho kwa wabunge kuonekana kama dharau kwa mwananchi wa kawaida.
“Tunaelekea kwenye shimo la madeni, lakini wabunge wanakula marupurupu ya kusafiri kama hawajui magari yanatumia mafuta ya wananchi,” aliandika @MillyWanjiru kwenye Facebook.
Kilio cha raia kimechangiwa zaidi na ukweli kwamba ahadi za Rais William Ruto za kupunguza matumizi ya serikali, hasa kupunguza idadi ya washauri wake, zimeonekana kuwa maneno matupu. Badala ya kupungua, idadi hiyo imeongezeka, na hivyo kuongeza mzigo kwa mlipa ushuru.
Aidha, sekta muhimu kama afya na elimu zimekuwa zikisuasua. Mfumo wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) umefeli kutoa huduma bora huku walimu wakuu wa shule wakikosa mgao kutoka serikalini.
Wakati huo huo, madaktari wanagenzi bado hawajaajiriwa licha ya makubaliano ya pamoja (CBA) yaliyotiwa saini. Serikali inadai haina fedha za kuwalipa.
“Wabunge wanapata mileage ya milioni, sisi madaktari tunaambiwa hakuna hela. Afya ya mwananchi sio muhimu kwao,” alilalamika daktari mmoja kupitia mtandao wa Telegram.