Na NA COLLINS OMULO May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga ameshikilia kuwa sharti wabunge waruhusu mswada wa kuhalalisha Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF) uidhinishwe na wananchi katika kura ya maamuzi la sivyo pesa za hazina hiyo zisalimishwe kwa serikali za kaunti.

Huku akiunga mkono pendekezo hilo kutoka kwa maseneta, kiongozi huyo wa ODM waliwataka wabunge kujikita katika majukumu yao matatu yaliyoko kwenye katiba na wakome kuingilia majukumu ya serikali.

Majukumu hayo matatu ni; utengenezaji wa sheria, kuhakikisha utendakezi wa serikali na uwasilishaji matakwa ya wapiga kura katika serikali.

Akiongea Alhamisi, Mei 22, 2025 baada ya kufanya kikao cha faragha na maseneta, Bw Odinga alisisitiza kuwa wabunge hawafai kusimamia fedha za hazina ya ustawi wa maeneo bunge yao.

Alisema jinsi ambavyo, Seneti imejikita katika wajibu wake, Bunge la Kitaifa linapasa kufanya hivyo, akisema hatua yao na kusimamia NG-CDF inajumu kanuni ya kikatiba ya utengano wa mamlaka kati ya nguzo za serikali.

“Kazi ya wabunge ni kutoa uwakilishi, uhakiki wa utendakazi wa serikali na utungaji wa sheria na haya ndio majukumu wanayopasa kushughulika nayo,” akasema.

Bw Odinga amekuwa amekuwa akisisitiza kuwa juhudi za sasa zinazoendeshwa na wabunge kuifanya hazina hiyo itambuliwe na Katiba haina maana.

Amelikashifu Bunge la Kitaifa kwa kuvuka mipaka ya majukumu yake na kuonekana kuhujumu ugatuzi kwa kutwaa majukumu ya serikali za kaunti.

Bw Odinga alionya kwamba kwa kuendelea kudhibiti fedha za maendeleo wabunge wanashiriki mgongano wa kimasilahi hali inayohujumu kuwajibika kwao.

Kiongozi huyo wa ODM alisema haiwezekani kwa wabunge kuhakiki utendakazi wa serikali ya kitaifa ikiwa watasimamia utekelezaji wa miradi hiyo hiyo wanayopasa kuhakiki.

“Hazina ya NG-CDF ni njia mojawapo ambayo wabunge wanatumia kuingilia majukumu ya serikali za kaunti. Wabunge hawafai kujenga barabara, hospitali na shule,” Bw Odinga akasema.

“Mwendeshe vikao vingi vya ushirikishaji maoni ya umma, mtakavyopenda lakini hatimaye sharti mswada huo uwasilishwe kwa kura ya maamuzi na mtapoteza. Ndio tunataka basari, lakini utoaji wa basari ufanywe na serikali za kaunti,” akaongeza.

Hazina ya NG-CDF ilianzishwa kama njia moja ya kupambana na umasiki na kuchochea maendeleo katikati ngazi za mashinani.

Hazina hiyo hutengewa asilimia 2.5 ya jumla ya mapato yanayokusanywa na serikali ya kitaifa kila mwaka.

Ilivyo sasa kila moja ya maeneo bunge 290 hupokea angalau Sh130 milioni kila mwaka.

Maeneo bunge yenye idadi kubwa ya watu na yale yaliyoko maeneo yenye kiwango kikubwa cha umasikini hupokea mgao mkubwa wa pesa za hazina hiyo.

Bw Odinga alisema juhudi za kufikia malengo ya ugatuzi zimekuwa ngumu kwa utekelezaji wake umekumbwa na changamoto nyingi ndani ya miaka 12 iliyopita.

“Bado kina shida za hapa na pale lakini tunaweza kuzishughulikia kwa kutoa nafasi kwa serikali za kaunti kutekeleza majumu yao. Ugatuzi ni safari na kwa pamoja sharti tusafiri pamoja tukiwa na matumaini kuwa tutafaulu,”  akaeleza.

Bw Odinga pia alitaka Bunge la Seneti lipewa mamlaka zaidi ili liweze kutekeleza majukumu sawa na yanayotekelezwa na mabunge ya seneti katika nchi zingine, haswa Amerika.

“Seneti inapasa kutekeleza wajibu ipasavyo na hivyo inapasa kuongezwa mamlaka. Mamlaka ya Seneti ya Kenya yanapasa kuwa sawa na yale ya Seneti ya Amerika,” Bw Odinga akaeleza.

Naibu Kiongozi wa ODM na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kuwa Bw Odinga amejitolea kulinda ugatuzi, licha ya kwamba wabunge na serikali ya kitaifa zimekuwa zikijuhumu utendakazi wa serikali za kaunti.

Bw Osotsi alisema maseneta wamekubaliana kuachilia Hazina ya Seneti kuhusu Uhakiki wa Utendakazi wa Serikali za Kaunti (SOF) kwani wabunge wanapania kuitumia kuwahonga (maseneta) kupitisha mswada wa kuhalalisha NG-CDF.

“Wabunge wanatumia hazina iliyopendekezwa ya SOF kuwahonga maseneta wapitishe hazina ya NG-CDF inayokiuka katiba. Njia ya kipekee ya kuhalalisha hazina hii ya kuwasilisha Mswada huo katika kura ya maamuzi. Hii kwa sababu unaenda kinyume na malengo ya katiba na muundo wa uongozi,” akasema Bw Osotsi.

Naye Seneta wa Kirinyaga James Murango aliunga mkono kauli ya Bw Osotsi akishikilia kuwa hazina ya NG-CDF inakiuka Katiba.

“Aidha, tunataka Seneti ipewe mamlaka zaidi kama vile ya kupitisha Mswada wa Fedha na kuidhinisha Bajeti ya Kitaifa. Hii ni kwa sababu masuala yote ya kifedha yanahusu kaunti,” Bw Murango akaeleza.