Asaka mumewe aliyepotea kufutia mgogoro wa ardhi
MIRIAM Ndunge Muya, 43, hana amani tena baada ya mumewe kupotea siku 21 zilizopita kufuatia mzozo wa ardhi.
Mumewe Nicholas Alex Otieno, 47, aliondoka nyumbani kwao Mlolongo Phase IV mnamo Agosti 7, 2025 kwenda hospitalini kwa matibabu ya jeraha la kichwa na hajarudi tena.Alikuwa amejeruhiwa katika makabiliano baina ya wakazi na wahuni waliodaiwa kuingilia mgogoro wa ardhi ya jamii.
Aliketi kwa huzuni nje ya ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Athi River, akiwa amembeba bintiye wa miaka mitatu.Bi Ndunge alikuwa amepiga kambi hapo kwa zaidi ya saa sita tulipompata.
Lengo lake lilikuwa wazi kutafuta majibu kuhusu aliko mumewe aliyepotea, Bw Nicholas Alex Otieno, mwenye umri wa miaka 47, ambaye alitoweka siku 21 zilizopita.Bi Ndunge alisema kuwa mumewe aliondoka nyumbani kwao eneo la Mlolongo Phase IV Mulinge mnamo Agosti 7, 2025 kuelekea hospitali ya karibu kutafuta matibabu ya jeraha la kichwa.
Alisema siku ya awali, mumewe alikuwa amejeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya wakazi na genge la wahuni waliodaiwa kuingilia mgogoro wa umiliki wa ardhi ya jamii.Akiwa amevaa sweta la kijani kibichi, suruali nyeusi na viatu vya plastiki vya wazi, Bw Otieno ambaye hufanya kazi za vibarua katika maeneo ya ujenzi ili kutunza familia yake, alimuaga binti yao wa mwisho kabla ya kuondoka lakini hakurudi tena nyumbani kama ilivyo kawaida.
Majira ya saa kumi na mbili jioni, Bi Ndunge alikosa subira na akampigia simu mumewe. Ingawa aliahidi kurudi baadaye, alisema alionekana kuwa katika hali ya wasiwasi.“Nilipopiga simu, alizungumza kwa kifupi na kwa haraka. Alionekana kuwa katika hali ya taharuki na alikuwa akipumua kwa kasi.
Alisema kuna mtu (bila kutaja jina) alimpa kazi ya muda kwenye jaa la karibu na mtaa wetu,” alisema Bi Ndunge huku machozi yakimtoka na sauti yake ikitetemeka,
“Ilikuwa jioni sana na nikahisi kuna tatizo. Nilijaribu kumpigia tena lakini hakupokea simu zangu.”Haijulikani ikiwa Bw Otieno alifika hospitalini kutibiwa kabla ya kutoweka. Mahali alipokuwa kuanzia saa tatu asubuhi alipoondoka nyumbani hadi saa kumi na mbili jioni alipozungumza na mkewe kwa simu bado ni kitendawili.
Mnamo Agosti 9, 2025, Bi Ndunge aliandikisha ripoti ya kupotea kwa mtu kupitia OB 22 katika Kituo cha Polisi cha Mavoko SNP, bila kujua alikuwa ameanza safari ndefu ya kutafuta majibu yasiyopatikana kutoka kwa jamaa, vituo vya polisi, hospitali na mochari – kuhusu aliko mumewe!
“Kwa msaada wa marafiki na jamaa, tumemtafuta kila mahali lakini hatujafanikiwa. Nimepitia usiku wa upweke nikisubiri mlango kugongwa na mume wangu, ni uchungu sana,” aliongeza.Akimtaja mumewe kama mtu mchangamfu asiye na marafiki wengi wanaojulikana, alieleza hofu kuwa huenda wahuni waliomjeruhi siku moja kabla ya kutoweka kwake ndio walihusika na huenda wanamzuilia kwa siri.
“Nahofia maisha yangu na ya binti yangu. Naomba maafisa wa usalama wanisaidie kumtafuta mume wangu. Kama alitekwa, naomba aachiliwe,” aliomba kwa sauti ya majonzi.Bi Ndunge alipokuwa amepiga kambi kwenye ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Athi River, Bw Odidi Otieno, siku ya Alhamisi, kiongozi huyo alikataa kuzungumza na wanahabari kuhusu suala hilo.
Aidha, wakazi waliokuwa wameandamana na Bi Ndunge walizuiwa kuingia katika jengo la DCC na maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami, hali iliyokaribia kuibua kizaazaa.
Hata hivyo, mzee wa kijiji wa Mlolongo Phase IV Mulinge Scheme, Bw Paul Ndunda, aliiambia Taifa Leo kwamba huenda Bw Otieno alikuwa mwathiriwa wa mgogoro wa umiliki wa ardhi kati ya wakazi na genge la wahuni ambao wamekuwa wakiwatisha kwa takriban miaka miwili sasa.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Athi River Mashariki, Bw Anderson Mbae, alisema ofisi yake inafahamu kuhusu ripoti ya mtu aliyepotea na kwamba uchunguzi unaendelea chini ya usimamizi wa mashirika mbalimbali yanayoongozwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
“Maafisa wa usalama wanafanya kazi usiku na mchana kutatua fumbo hili la kutoweka kwa Bw Otieno. Ni mapema mno kubashiri sababu,” alisema Bw Mbae, akiwasihi jamaa na marafiki kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia katika uchunguzi.