2018: Je, mabadiliko ya hali ya anga yaliongeza bei ya mafuta?
Na BERNARDINE MUTANU
Miezi kadhaa iliyopita, serikali iliweka ushuru wa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta na kusababisha bei ya mafuta nchini kupanda kwa kiwango kikubwa.
Ilikuwa changamoto kwa wananchi hasa watumiaji wa mafuta ya taa wengi wao ambao wanaishi chini ya dola kwa siku.
Lakini baada ya wananchi kulia sana, serikali iliamua kupunguza ushuru huo hadi asilimia nane.
Licha ya hatua hiyo, mafuta yamekuwa yakiongezeka hatua kwa hatua katika muda wa miezi kadhaa iliyopita.
Katika muda wa mwaka mmoja, bei ya mafuta imekuwa karibu maradufu. Kwa mfano katika Novemba 15 na Desemba 14, 2017, bei ya mafuta taa Nairobi ilikuwa ni Sh71.23 ilhali bei hiyo ilikuwa ni Sh111.83 muda huo 2018, zaidi ya uwezo wa wananchi wengi.
Mjini Mombasa, bei ya mafuta taa kati ya Novemba 15 na Desemba 14, 2018 ilikuwa ni Sh109.20 ikilinganishwa na Sh68.46 kipindi hicho 2017.
Licha ya kuwa kuna mambo mengi ambayo yamehusishwa na ongezeko la bei ya mafuta ikiwemo bei katika soko la kimataifa na mfumko wa bei ya bidhaa, Kenya inaendelea kuhamia katika matumizi ya kawi inayoweza kufanya upya ingawa pole pole.
Hatua hii ni kwa lengo la kupunguza gesi zenye kuleta joto jingi ardhini kuambatana na makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusiana na kupunguza utoaji wa gesi hizo ambazo nidioksidi ya kaboni, oksaidi ya shura (nitrous Oxide) na methani.
Katika wavuti wake, ERC imesema, “Huku Kenya ikilenga kubadilisha uchumi wake kutoka kilimo hadi utengenezaji wa bidhaa na utoaji huduma ambazo ni sekta zinahitaji sana matumizi ya kawi, utoaji wa kawi safi, ambaye wengi wanaweza kupata na inayoweza kutegemewa ni muhimu.”
Hata hivyo, wakati wa mahojiano na Taifa Leo, Mkurugenzi Mkuu wa ERC Pavel Robert Oimeke alisema ongezeko la bei ya mafuta linatokana na ongezeko la bei ya mafuta ambayo hayajasafishwa.
“Bei ya mafuta yasiyo safi iliongezeka kutoka Sh5,570 kwa pipa Septemba 2017 hadi Sh7,825 kufikia Mei 2018. Zaidi, ushuru (VAT) uliongezewa kwa petroli, dizeli na mafuta taa kutoka Septemba 1, 2018,” alisema.
Aliongeza kuwa ukweli kwamba bei ya mafuta taa imeongezeka kwa kiwango cha juu zaidi ni kwa sababu ya kuongezewa kwa ‘ushuru wa kuchanganywa’ kupitia kwa Mswada wa Fedha 2018. Ingawa bei ya mafuta nchini mara nyingi hutegemea mahitaji na uzalishaji ulimwenguni, kudhibitiwa kwa bei ya mafuta huenda likawa ni suala la mabadiliko ya anga kulingana na wataalamu.
Matumizi ya mafuta kwa magari, jenereta na meli hutoa gesi za kuleta joto, moja dioksidi ya kaboni ambayo kulingana na shirika la kupima hali ya hewa ulimwenguni (WMO) iliongezeka kwa kiwango kikubwa sana.
Kutokana na hilo, joto ardhini linazidi kuwa jingi na ndio maana kumekuwa na kuyeyuka kwa mabahari na mabadiliko ya hali ya anga.