Makala

2018: Mwaka wa kondomu feki madukani

December 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na CAROLYNE AGOSA

MWAKA wa 2018 umekuwa mwaka ambao kondomu ziligonga vichwa vya habari huku visa vya mipira feki, duni au chache vikiripotiwa mara kadha na baadhi kuishia kortini.

Siku chache tu kabla ya Siku ya Wapendanao Februari 14, shirika la Population Services Kenya (PSK) lilitoa tahadhari ya kuwepo kwa kondomu feki madukani.

Shirika hilo la afya ambalo husambaza kondomu za Trust nchini lilionya kuhusu kondomu zake feki zilizokuwa zikiuziwa wananchi, hususan aina ya Trust Studded.

Kwenye tangazo magazetini kwa siku tatu mfululizo, shirika hilo liliwaomba wateja kuwa waangalifu mno kuthibitisha “alama za uhakika za kondomu za Trust Studded” wanaponunua mipira hiyo ya mapenzi.

“Angalia alama za ubora kwenye pakiti zetu kuhakikisha unanunua kondomu za sawa za Trust. Usihadaiwe,” PS Kenya ilisema katika tangazo hilo na kutoa maelezo kuhusu alama hizo.

Miezi kadha baadaye, na siku moja tu kabla maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Ulimwenguni Desemba 1, Wizara ya Afya ilitoa tahadhari kuhusu matumizi ya kondomu za Fiesta baada ya mipira hiyo kupatikana kuwa na mashimo.

Uchunguzi uliofanywa na Bodi ya Dawa na Sumu (PPB) ambayo ndiyo hudhibiti dawa na bidhaa za matibabu ulipata kuwa, kondomu hizo za wanaume hazikuwa na unene unaohitajika.

Kasoro zilipatikana hususan katika mipira ya Fiesta Stamina na Fiesta Big Black wakati PPB ikiendesha uchunguzi wake wa mara kwa mara kubaini ubora wa bidhaa sokoni.

“Bodi ya Dawa na Sumu ilifanya uchunguzi uliojumuisha bidhaa za Fiesta Stamina na Fiesta Big Black zinazotengenezwa na kampuni ya Cupid Limited. Bidhaa za Fiesta Stamina zilikosa kutimiza kipimo cha kutokuwa na mashimo, huku Fiesta Big Black zikikosa kutimiza kipimo cha unene,” ilisema barua ya bodi hiyo iliyoandikwa Novemba 20, 2018.

Kampuni ya Cupid Limited ambayo ndiyo hutengeneza mipira hiyo, kuiondoa sokoni.

“Unaagizwa kuondoa sokoni mara moja bidhaa zilizoathiriwa. Vile vile, unatakiwa kuwasilisha utaratibu wa jinsi utakavyoondoa bidhaa hizo katika siku mbili za kupokea barua hii,” ilieleza.

Kondomu za Fiesta huundwa na kampuni hiyo ya kimataifa yenye makao yake nchini India kabla kusambazwa katika mataifa zaidi ya 40 kote ulimwenguni.

Kando na mipira feki na duni kuripotiwa, kisa kingine kilichoibuka 2018 ni kesi ya mwanamume aliyedai kwamba kondomu ambazo alikuwa akitumia wakati akishiriki ngono nje ya ndoa zilikuwa duni kwani aliambukizwa maradhi ya zinaa.

Aidha, mkazi huyo wa Nairobi alidai kuwa baadhi ya wanawake alioshiriki nao mapenzi waliishia kushika mimba.

Katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu mwezi Julai, Williamson Nyakweba Omworo alisema kwa karibu miezi 10 alikuwa akiramba asali kama kawaida kabla kugundua kondomu za Zoom alizotumia hazikuwa bora.

Mwanamume huyo aliomba korti kumpa fidia ya matibabu akisema kuwa baada ya kuambukizwa maradhi ya zinaa mke alimtoroka, alipoteza kazi yake, na kusongwa na mawazo.

Omworo alishtaki kampuni ya Beta Healthcare inayosambaza kondomu hizo, Shirika la Ubora wa Bidhaa (Kebs) na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kwa kuruhusu uuzaji wa mipira hiyo aliyoamini kuwa mibovu.

Mwanamume huyo aliomba kortini kumpa fidia ya matibabu na masaibu ambayo amepitia akisema kuwa baada ya kuambukizwa maradhi ya zinaa mke alimtoroka, alipoteza kazi yake, na kusongwa na mawazo.

Kondomu zilizo na kasoro ni hatari kwani zinapotoboka ama kulegea hukosa kuwapa wapenzi ulinzi wanaohitaji kuzuia mimba na vile vile maambukizi ya maradhi ya zinaa ikiwemo HIV.

Walaghai wamefanikiwa kunakili bidhaa mbalimbali za kondomu ikiwemo Durex.

Mnamo 2013, genge kubwa la kimataifa la watengenezaji kondomu bandia lilitibuliwa nchini China baada ya takriban mipira milioni tano feki kunaswa wakati washuki,wa wakijitayarisha kuisafirisha kuelekea mataifa ya nje, kama ilivyoripoti shirika ABC News.

Visa vya uhaba wa kondomu pia viliripotiwa nchini, hususan katika mji wa Achers Post katika kaunti ya Samburu kwenye barabara kuu ya Isiolo-Moyale.

Mji huo umeshuhudia ukuaji mkubwa kwani ni kitovu cha usafiri kuelekea Kaunti ya Marsabit na pia mji wa Moyale katika mpaka wa Kenya na Ethiopia.

Vile vile, kambi za kijeshi za Kenya na Uingereza pia zimechangia ukuaji huu pamoja na hifadhi za wanyamapori katika kaunti za Samburu na Isiolo.

Ukuaji huu umevutia biashara mbalimbaloi ikiwemo ukahaba.

Msimu wa sherehe za Krismasi ulipoanza Desemba ripoti ziliibuka kwamba baadhi ya wakazi walidai kondomu za wanaume zilikuwa haba mno kiasi cha kuwalazimu wengine kutumia tena mipira hiyo.

Aidha, wengine aliamua kutumia karatasi za plastiki kama kinga ya magonjwa ya zinaa.