Makala

Mwanafunzi wa kike aliyevunjika uti wa mgongo ahitaji usaidizi wa dharura

May 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAFUNZI wa kike mjini Thika anahitaji usaidizi baada ya kuvunjika uti wa mgongo wake.

Binti Rachael Wanjiku, 11, anahisi maumivu makali kutokana na uti wake wa mgongo kuvunjika mwaka wa 2017 alipokuwa akicheza na mwanafunzi mwenzake.

Imedaiwa mwenzake alimsukuma wakiwa nje wakicheza na kwa ghafla alianguka kwa mgongo wake ambapo alijeruhiwa vibaya.

Mamake mwanafunzi huyo, Bi Virginia Mukami, anakiri kwamba mwanawe huyo – Wanjiku – amekuwa akihisi uchungu kila mara ambapo hata hawezi kujifanyia kazi yoyote mwenyewe.

Alizidi kueleza ya kwamba baada ya kupata majeraha hayo, mwanawe amekosa kuenda shule kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

“Nilimpeleka kwa hospitali ya kibinafisi jijini Nairobi ambapo walipata ya kwamba uti wake wa mgongo uliathirika vibaya na anahitaji upasuaji unaohitaji Sh2.5 milioni nchini India. Mimi hata kazi za nyumba ya kufulia watu nguo niliacha ili kumshughulikia mwana wangu. Maisha yanaendelea kuwa magumu kwa sababu bado ninahitaji kumpatia chakula na sina namna,” anasema Bi Mukami.

Ripoti ya daktari ilieleza kuwa uti wake wa mgongo ulikuwa tayari umelegea ambapo viungo vyake ya mikono na miguu haviwezi tekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Kwa hivyo, ninahitaji kutafuta wahisani ili wanisaidie niweze kumpeleka binti yangu hospitalini kwa ajili ya kupewa matibabu. Ninasononeka kila mara hata nashindwa la kufanya,” anasema Bi Mukami hata anashindwa kujizuia kububujikwa na machozi ya uchungu wa mzazi.

Mwanafunzi huyo anasema anahisi maumivu makali hata hawezi jifanyia kazi yoyote ile.

“Sijahudhuria shule kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Mimi nilikuwa katika darasa la tano nilipoumia na sasa ninatamani kurejea shuleni lakini siwezi,” anasema Wanjiku, huku akionekana kweli anayepata maumivu mengi.

Mfanyabiashara anayehusika na ususi Bw Humphrey Njenga ndiye alikuwa mstari wa mbele kuangazia masaibu ya mwanafunzi huyo baada ya hali yake kumulikwa na mitandao ya kijamii.

“Mimi niliguswa pakubwa na ndipo nikafanya hima nifuate vyombo vya habari kutafuta usaidizi,” akasema Bw Njenga na kuongeza jambo hilo ni la dharura na kila mmoja aliyeguswa ana haki ya kujitolea kuona ya kwamba msichana huyo anapata nafuu na kurejea shuleni.

Yeyote anayetaka kutoa mchango wake anastahili kutumia Paybill No 334061.

Tayari baadhi ya watu walioguswa na suala hili wanaendelea kutoa michango yao.