Makala

MBURU: Kutunza mazingira kutasaidia kulkuza amani duniani

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

Siku ya Amani Ulimwenguni, ni siku yenye umuhimu mkubwa katika kuhakikisha kuwa watu na mataifa yanaishi kwa uwiano.

Maadhimisho ya siku hii ambayo hufanywa kila Septemba 21, yalibuniwa na Umoja wa Mataifa (UN) ili kuhakikisha kuwa dunia inaishi kwa amani, na kuwa masuala tofauti yanayoweza kuvuruga amani yanaangaziwa na kutatuliwa.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, suala la kutunza hali ya hewa kama mbinu ya kutafuta amani ndiyo ajenda kuu.

Ukweli ni kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa yakisababisha mizozo baina ya jamii na nchi, kimataifa na hata Kenya haijasazwa.

Maelfu ya Wakazi kutoka msitu wa Mau walitimuliwa kuhakikisha chemichemi za maji zinahifadhiwa.Hii ni moja wapo ya miradi iliyowekwa kuhakikisha kuwa misitu inahifadhiwa nchini.

Kwa njia rahisi, hali ya hewa inapochafuliwa ama kuharibiwa, watu wanakosa mahitaji ya kimsingi kama hewa safi, maji, chakula na lishe bora. Hali hii husababisha watu kuanza kung’ang’ania palipo na ubora wa mahitaji haya, wakiishia kuvurugana, kupigana na hali inapozidi hata kuuana.

Hivyo, ni vyema kwa Wakenya wote kesho kujiunga na ulimwengu kuhubiri kuhusu umuhimu wa kuyatunza mazingira na hali ya hewa, kwani ukweli ni kuwa hatua hiyo mwishowe huchangia kuleta amani katika jamii.

Kando na kukosekana kwa amani kutokana na mazingira wanamoishi watu, tumeshuhudia visa vya watu kulazimika kuhama makwao kutokana na hali ya mabadiliko ya hali ya anga, hasa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko ama maporomoko ya ardhi, ama kiangazi kikali.

Washikadau katika sekta mbalimbali, hasa ya kulinda mazingira wanafaa kutumia siku ya kesho kuwaelimisha na kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kutunza hali ya hewa.

Utakuwa wakati muafaka kuhusisha wanafunzi mashuleni, mashirika mbalimbali na zaidi ya yote kuwaelimisha watu wasiofahamu kuhusu umuhimu wa nkutunza mazingira kwani wengi wanaathirika na hali ya kutojua.

Serikali sasa inafaa kuweka mikakati thabiti pamoja na sera za kuwezesha utunzaji wa mazingira na kulinda hali ya hewa, kama mbinu ya kuboresha siku za usoni na kutafuta amani.

Hatuwezi kuendelea kushuhudia visa vya watu, jamii ama mataifa kuzozana na kupigana, kwa mizozo inayoweza kuzuiwa, kama kwa kutunza mazingira.

Mwisho, wakati tunatunza mazingira na hali ya hewa kwa ajili ya amani, tuendelee kushikilia misingi mingine ya kukuza amani kama kuwajali majirani zetu, kupendana na kusaidiana panapokuwa na tatizo.