ODONGO: Wazee wasitumiwe kuwalazimishia raia viongozi
Na CECIL ODONGO
MTINDO wazee au watu mashuhuri katika jamii kuwatawaza viongozi wa kisiasa kama wasemaji wa jamii zao unafaa kutupiliwa mbali, na badala yake wananchi waruhusiwe wajiamulie kiongozi wanayemtaka kupitia kura wakati wa uchaguzi.
Kauli hii imetokana na kuzuka kwa mjadala mkali kuhusu mkutano wa kuamua mustakabali wa kisiasa wa jamii ya Abaluhya, ambao umepangiwa kufanyika Januari 18 katika Kaunti ya Kakamega.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu) Francis Atwoli, ambaye anadhamini mkutano huo, amejipata akiungwa mkono au kupingwa na wanasiasa, ikikisiwa kwamba jamii hiyo pia itatoa kauli yake kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).
Ingawa hivyo, ni vyema kutambua kwamba Bw Atwoli aliongoza mkutano kama huo Disemba 31, 2016, ambapo Kinara wa ANC Musalia Mudavadi alitajwa kama msemaji wa jamii hiyo.
Kwa mtazamo wangu, haifai kamwe kwa wazee au viongozi wenye ushawishi watumie mamlaka yao kuwalazimishia raia kiongozi.
Japo, Bw Atwoli pia ana uhuru wa kuandaa mkutano huo na kumtaja msemaji mpya, huenda atakayetajwa akawa na kibarua kigumu kuunganisha jamii hiyo ambayo imekuwa ikigawanya kura zake kwa wawaniaji mbalimbali wa urais.
Si Magharibi pekee ambako mtindo huo huenda usishabikiwe, kwa kuwa hata maeneo mengine, kutawazwa kwa viongozi fulani kumekosa kuvutia uungwaji mkono miongoni mwa raia.
Kwa mfano miaka miwili iliyopita, Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati alitawazwa kama mzee na msemaji wa jamii ya Abagusii lakini licha ya kujizolea umaarufu miongoni mwa wafuasi wa ODM jijini, mbunge huyo hajafaulu kudhibiti jamii yake kisiasa kama waziri wa zamani Simeon Nyachae enzi zake.
Katika eneo la Nyanza, aliyekuwa mbunge wa Rongo na waziri mwenye ushawishi mkubwa katika utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi, Bw Dalmas Otieno alitawazwa na baadhi ya wazee kama msemaji wa jamii ya Waluo lakini hilo halikumsaidia kumpiga kumbo Bw Odinga ambaye bado ni maarufu sana eneo hilo.
Eneo la Pwani nalo halijakuwa na msemaji kamili tangu kufariki kwa Waziri wa Utalii Karisa Maitha mnamo mwaka wa 2004. Licha ya magavana Ali Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi(Kilifi) kutawazwa wazee wa Mijikenda, ushawishi wao wa kisiasa eneo hilo umekuwa ukitegemea siasa za Bw Odinga na chama cha ODM.
Hata Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto hawakujipa umaarufu wanaojivunia kwa sasa kutokana na kutawazwa.