• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mapapai: Matunda yenye ushindani mkuu sokoni kipindi hiki cha corona

Mapapai: Matunda yenye ushindani mkuu sokoni kipindi hiki cha corona

Na SAMMY WAWERU

UGONJWA wa Covid-19 na ambao ni janga la kimataifa umejiri na mafunzo mengi kwa taifa la Kenya na ulimwengu kwa jumla.

Uchumi wa nchi nyingi umeathirika kwa kiwango kikubwa. Sekta mbalimbali zimeyumbishwa na makali ya corona, idadi ya juu ya wafanyakazi wakipoteza nafasi za ajira.

Licha ya mahangaiko yanayoendelea kushuhudiwa, gurudumu la maisha sharti lisukumwe.

Ni bayana lazima watu wale na wanywe, ili kuzima makali ya njaa. Aidha, sekta ya kilimo imekuwa tegemeo kuu kipindi hiki cha nyakati ngumu, na ambayo imedhihirisha ni nguzo kuu ya uchumi na maendeleo.

Kando na kuhakikisha kuna bidhaa za kutosha za kula, sekta ya kilimo imekuwa mwajiri wa wengi hasa walioathirika kwa kupoteza kazi.

Kuna walioingilia shughuli za kilimo na wengine kuwa wafanyabiashara wauzaji wa mazao.

Chaguo la mimea bora kulima ni muhimu, katika mdahalo huu. Huku madaktari na wataalamu wa masuala ya afya wakihimiza watu kukumbatia chakula chenye virutubisho vya kutosha ili kuuhami mwili kwa kinga imara dhidi ya virusi vya corona, matunda yanajumuishwa kwenye orodha hii.

Mapapai ni kati ya matunda yanayopendekezwa kipindi hiki cha corona. Isitoshe, ni chakula murwa kwa watoto hasa wanaoendelea kunyonya.

Huku soko lake likiwa mithili ya dhahabu, Loise Ndung’u ambaye ni mkulima wa mimea mseto Kaunti ya Murang’a, anakiri mapapai yana faida chungu nzima kimapato.

Loise Ndung’u mkulima wa mapapai Kaunti ya Murang’a. Picha/ Sammy Waweru

Alianza kuyakuza miaka kadha iliyopita.

“Mapapai ni kati ya matunda yenye ushindani mkuu sokoni,” Loise anasema.

Anaendelea kueleza kwamba kipindi hiki watu wanahimizwa kula matunda kwa wingi, soko la mapapai limenoga. “Mapapai ni matunda yenye virutubisho anuwai, mwororo na yasiyo na asidi, hivyo basi ni kipenzi cha wengi,” anafafanua mkulima huyo.

Harrison Kinyanjui ni mkulima wa mapapai Thika, na anakiri soko lake linaendelea kuimarika. “Mwaka huu, 2020, matunda haya yamekuwa na ushindani mkuu sokoni. Sijaweza kutosheleza mahitaji ya wanunuzi wangu,” Kinyanjui anaiambia Taifa Leo.

Cha kutia moyo katika uzalishaji wa mapapai ni kwamba hayana ugumu kuyakuza. Muhimu zaidi ni mkulima kuwa na chanzo cha maji ya kutosha, kwa kuwa yananarishwa na maji.

“Kilimo cha matunda kinafanikishwa na kuwepo kwa maji ya kutosha,” anasisitiza Angela Mutegi, mtaalamu wa masuala ya kilimo. Mahitaji mengine muhimu ni matunzo kwa njia ya fatalaiza na mbolea, na vilevile palizi kuondoa kwekwe na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu.

Jinsia ya mipapai ya kike shambani inapaswa kuwa zaidi ya asilimia 95, kulingana na maelezo ya mtaalamu Angela. “Idadi ya mipapai ya kiume iwe takriban asilimia tano ili kusaidia katika uchavushaji mtambuka (cross pollination),” anashauri mdau huyo.

Kwa kuzingatia vipimo faafu kitaalamu, ekari moja inasitiri zaidi ya mipapai 900. Aidha, mapapai yanachukua karibu miezi saba na chini ya mwaka mmoja pekee kukomaa, kuanza kuvuna, baada ya shughuli za upanzi.

Hata ingawa kiwango cha mavuno kinategemea matunzo na yalivyonawiri, wataalamu wa kilimo wakihoji mpapai mmoja kwa mwaka huzaa kati ya matunda 75 – 150, kiuzani yakikadiriwa kuwa kati ya tani 35 – 50, sawa na kilo 35, 000 – 50, 000.

Mapapai yananunuliwa kwa kilo, kilo moja ikiwa kati ya Sh40 – 100.

Kulingana na Loise Ndung’u, mkulima, chaguo la aina ya mbegu ya mipapai pia ni hoja ya busara kuzingatia. “Ni muhimu mkulima achague mbegu bora, kwa kufanya utafiti wa kutosha kupitia wakulima waliobobea katika ukuzaji wa mapapai na pia wataalamu wa kilimo,” anashauri.

Mapapai aina ya Solo-Sunrise Hybrid yanasemekana kuwa bora, kutokana na uhalisia wake. Wakulima wanaoyakuza wanasema yana ladha ya kipekee, inayoyafanya kuwa na ushindani mkuu sokoni.

Kimsingi, ukuzaji wa mapapai una faida tele kimapato, wakulima wakihimizwa kuyatathmini na kuyalima kwa wingi ili kukithi kiu cha wateja.

You can share this post!

COVID-19: Visa vipya 390

Tovuti ya IEBC yakwama watu wakiomba kazi