Ada zinazolemaza kilimo nchini
SERIKALI za ugatuzi zinaendelea kupata shinikizo kupunguza au hata kuondoa ada zinazotoza kwa pembejeo za kilimo na mazao ya shambani kati ya kaunti.
Sekta ya kibinafsi na wadauhusika katika sekta ya kilimo, wanahoji ada hizo maarufu kama cess ndizo zinachochea kiwango cha gharama ya chakula kuwa ghali.
Aidha, wanalalamika kuwa kando na kusababisha mfumko wa bei ya chakula, malipo hayo yanayotozwa kwenye mpaka wa kila kaunti kusafirisha bidhaa umefanya biashara kuwa ngumu kwa wauzaji wa mbegu, fatalaiza na wasambazaji wa mazao ya shambani kuelekea mijini.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Mtandao wa Wakulima Kenya, kwa Kiingereza ndio, Agriculture Sector Network (ASNET) Agatha Thuo, suala hilo lisipoangaziwa huenda litalemaza ukuaji wa sekta kilimo nchini.
“Mfumo wa sasa kutoza ‘ushuru’ kwa pembejeo na mazao ya kilimo yanaposafirishwa kutoka kaunti moja hadi nyingine, unadhoofisha uzalishaji, uwekezaji na kulemaza sekta ya kilimo,” Agatha anaonya.
Cess, ni malipo ambayo wasafirishaji wa pembejeo za kilimo na mazao kutoka shambani hulipishwa kuyavukisha kutoka kaunti moja hadi nyingine.
Ada hizo, ASNET na wadauhusika wengine kwenye utandawazi wa kilimo, hata ingawa wanaunga mkono ukusanyaji ushuru kuboresha uchumi, wanahoji si halali kisheria.
Kila kaunti ina ada zake ambazo ni tofauti na ya zingine, huku jinsi zinavyotozwa na kusimamiwa zikiibua maswali kwani kuna baadhi ya maafisa wanaokosa mfumo maalum wa risiti kuwajibika. Agatha anasema, “Imekuwa changamoto ya muda mrefu.”
Agatha anaelezea tofauti hizo kwa kutumia takwimu zilizokusanywa na ASNET kutoka kaunti mbalimbali.
Kwa mfano, gunia la mahindi yaliyokaushwa lenye uzito wa kilo 90 hutozwa cess ya Sh90 katika Kaunti ya Kericho, ikilinganishwa na Sh50 katika Kaunti ya Trans Nzoia.
“Gunia kama hilo la viazi linaweza kutozwa Sh50 katika kaunti moja na kiasi kikubwa zaidi katika kaunti nyingine,” anadokeza.
Kwa upande wa vitunguu, wafanyabiashara hulipa karibu Sh100 kwa kila gunia katika Kaunti ya Narok, ikilinganishwa na Sh30 katika Kaunti jirani ya Kajiado.
“Tofauti hizi zinamaanisha kwamba ninapokuwa mnunuzi wa mazao, ninahamishia gharama hizi kwa mkulima, na matokeo yake mkulima hupata malipo madogo,” anateta.
‘Ushuru’ huo, ambao wakosoaji wanasema hauna msingi thabiti kisheria, umeendelea kutozwa tangu mwaka 2013 kufuatia kuanza kwa serikali za ugatuzi baada ya kupitishwa kwa Katiba ya 2010.
Hata ingawa imegatuliwa, sekta ya kilimo na maendeleo ya mifugo inaendelea kupokea mgao kutoka kwa serikali ya kitaifa.
“Suala la ada zinazotozwa pembejeo na mazao ya kilimo linahitaji kutathminiwa kwa umakini mkubwa. Kama sekta binafsi, tunaunga mkono juhudi za serikali kuongeza uzalishaji wa kilimo, lakini pia ni lazima tushughulikie changamoto ambazo hazitalemaza uzalishaji,” Agatha akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.
ASNET ni muungano wa kilimo unaojumuisha wadau kutoka sekta binafsi pamoja na taasisi nyingine, zikiwemo zile za serikali, kwa lengo la kuratibu, kushawishi sera na kubadilisha sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuleta ushindani unaofaa na uwekezaji.
Muungano huo umejaribu kushinikiza Baraza la Magavana (CoG) kutathmini suala la cess, Agatha akinukuu Kifungu cha 209 cha Katiba kinachobainisha mamlaka ya ukusanyaji wa mapato ya serikali ya kitaifa na kaunti, akisisitiza kuwa ingawa kaunti zina haki ya kukusanya mapato, namna ushuru huu unavyotekelezwa kwa sasa una athari hasi kwa wakulima, wafanyabiashara na walaji.
ASNET inapendekeza cess itozwe mara moja katika eneo la uzalishaji, na mapato hayo yatumike kuboresha miundombinu ya kilimo.