Afya na Jamii

AFYA: Mimi ni mwanamume, hali ya matiti yangu kuwa makubwa inanitatiza sana

Na PAULINE ONGAJI October 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Daktari,

Mimi ni mwanamume wa miaka 45 na nimekuwa na tatizo la matiti yangu kuwa makubwa kupindukia. Je, haya ni maradhi na napaswa kufanya nini kukabiliana na tatizo hili?

Jerry, Nairobi

Hali ambapo matiti ya mwanamume yanakua makubwa inafahamika kama gynaecomastia.

Kwa kawaida hali hii hutokea kukiwa na tishu zaidi ya matiti katika sehemu inayozingira chuchu na hivyo kusababisha matiti kuwa makubwa.

Hali hii yaweza athiri matiti yote na wakati mwingine huenda titi au matiti yaliyoathirika, yakakumbwa na maumivu.

Sababu kuu ya hali hii ni kutokuwepo kwa usawa baina ya homoni za oestrogen na testosterone. Kwa kawaida, wanaume huwa na viwango vya chini vya oestrogen, suala linalosababisha tishu za matiti kukua. Viwango vya juu vya testosterone huzuia oestrogen zisichochee matiti kukua.

Kwa hivyo kutokuwa kwa ulingano baina ya homoni hizi kwaweza sababisha hali hiyo ya gynaecomastia.

Wakati mwingi, kinachosababisha tatizo hili hakijulikani, na huenda likafifia baada ya muda, japo kwa baadhi ya watu huendelea.

Huenda gynaecomastia pia ikatokana na uzani mzito (kiwango zaidi cha oestrogen kinazalishwa), katika umri wa kubalehe ambapo kuna mabadiliko ya viwango vya homoni, katika umri wa uzee kutokana na kupungua kwa viwango vya testosterone, matumizi ya pombe, sigara, mihadarati, baadhi ya dawa za kimatibabu, maradhi ya figo au ini, matatizo ya kijenetiki, uvimbe kwenye korodani, tezi za adrenalini au pituitari.

Ili kudhibiti hali hii litakuwa jambo la busara kwenda kwa daktari ili sehemu hiyo ifanyiwe uchunguzi. Hii itasaidia kubaini iwapo kuna matatizo mengine.

Ikiwa itathibitishwa kwamba hakuna usawa wa homoni, basi utapewa dawa. Aidha, waweza kufanyiwa upasuaji kuondoa tishu ya ziada kwenye matiti endapo dawa utakazopewa hazitasaidia kuleta mabadiliko. Ikiwa kuna maradhi mengine, basi utatibiwa.