Familia nyingi Afrika zakumbana na masaibu tele zikisaka huduma za afya
NA PAULINE ONGAJI
KATIKA kijiji cha Jimbo, Kata ya Lukore, Kaunti ya Kwale, Bi Faith Kioko,26, anajiandaa kumpeleka mwanawe, mwenye umri wa miaka saba katika kliniki.
Mwanawe Bi Kioko hawezi kujifanyia chochote, na hivyo ni jukumu la mama huyu kumuosha, kumvisha, kumlisha, kumsaidia kwenda haja, kumbeba na hata kumpindua anapolala.
Tatizo lilianza mtoto huyu akiwa na miezi sita ambapo alianza kuwa na kifafa.
“Pia, niligundua kwamba alikuwa analala sana,” aeleza Bi Kioko.
Kulingana na Bi Kioko, ukaguzi wa daktari uliofanywa Agosti 2018, ulionyesha kwamba mwanawe alikuwa na matatizo ya kusikia, kuzungumza, kusimama, na hata kutembea, huku akionyesha ishara za maradhi ya usonji.
Kutokana na hali hii lazima mtoto huyu amuone daktari mara moja kwa mwezi, na mtaalam wa tibamaungo mara mbili katika kipindi hiki.
Huduma hizi yeye hupokea katika hospitali ya Rufaa ya Msambweni, zaidi ya kilomita 30 kutoka nyumbani kwao, na hivyo kila wakati huu unapowadia, lazima Bi Kioko ajiandae kwa safari.
“Lazima nimuandae kisha nimbebe kwa takriban kilomita moja, kuelekea katika sehemu ambayo sisi husubiri gari, ambapo safari huwa mara mbili kwa mwezi,” aeleza.
Gari wanalotumia kwa safari hii ni aina ya probox, ambapo licha ya hali ya mtoto huyu, lazima wamkunje ili kuruhusu abiria wengine waingie.
Kisha kuna gharama ya usafiri ambapo kila ziara hospitalini, lazima awe na Sh700 za nauli.
Kisha kuna ada ya kliniki ya kumuona daktari kila mwezi, mbali na dawa ambazo anatumia.
“Ili kukabiliana na kifafa, daktari alipendekeza awe anatumia dawa fulani ambapo kwa mwezi yeye hutumia chupa mbili, na hii hutugharimu pesa nyingi,” aeleza.
Mahitaji
Kulingana na Bi Kioko, imekuwa changamoto kukidhi mahitaji ya mtoto huyu.
“Hii imekuwa changamoto kubwa kwa familia yetu hasa ikizingatiwa kwamba sina jira na nawategemea wazazi wangu ambao ni wakulima.”
Haya ni masaibu yanayokumba familia nyingi zinazosaka huduma za afya hasa katika maeneo ya mashambani, sio tu humu nchini, bali barani Afrika.Udadisi uliokusanywa kati ya Novemba 2020 na Machi 2021, kuhusu hali ya huduma nafuu ya afya kwa wote barani ulionyesha kwamba ni asilimia 48 pekee ya idadi ya watu barani wanapokea huduma za afya wanazohitaji huku hali ikiwa mbaya hata zaidi kwa wale wanaoishi katika maeneo ya mashambani.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, raia wengi wa Afrika hawapokei huduma za afya kama inavyofaa kutokana na ugawaji duni wa rasilimali katika sekta ya afya.
Utafiti unaonyesha kwamba kwa sasa mataifa ya Afrika hutumia kati ya $8 na $129 kwa kila mtu kwa afya, ikilinganishwa na mataifa tajiri ambayo hutumia zaidi ya $4,000.
Hii ni kwa kutokana na masuala mbali mbali kama vile kiwango cha chini cha jumla ya pato la taifa (GDP) na kiwango cha chini cha ukusanyaji thabiti wa ushuru.
Kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamesababisha sekta ya afya kupuuzwa barani inapowadia wakati wa kuitengea fedha.
Uongozi mbaya
Kulingana na Prof Francis Omaswa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afya ulimwenguni barani Afrika (ACHEST), Afrika imekumbwa na changamoto ya uongozi mbaya, suala ambalo limetatiza tu sio sekta ya afya, bali maendeleo kwa ujumla.
“Aidha, umaskini umekuwa changamoto katika bara hili huku idadi ya watu ikiendelea kuongezeka,” aeleza Prof Omaswa.
Kulingana na mtaalam huyu, aidha, mataifa mengi ya Afrika, Kenya ikiwa miongoni mwayo, hutegemea ufadhili kutoka nje ili kuendesha asilimia kubwa ya bajeti ya huduma za afya.
“Hii imesababisha mataifa mengi kushindwa kujitegemea katika sekta hii,” aeleza.
Ili Afrika itimize ndoto ya raia wake kufikia huduma za afya kwa urahisi, Prof Senait Fisseha, mkurugenzi wa miradi ya kimataifa katika hazina ya The Susan Thompson Buffet Foundation, asema lazima uongozi wa nchi hizi uwe tayari kuwekeza katika sekta ya afya.
Kulingana na Prof Omaswa, ndoto hii itatimizwa tu iwapo suala la uongozi litaangaziwa.
“Aidha, suluhisho ni kuzungumza na viongozi wa nchi za Afrika na kuwarai kuwekeza zaidi sio tu katika afya, bali pia utafiti. Tatizo ni kwamba viongozi wengi barani huchukulia huduma ya afya kuwa mzigo, ilhali yaweza kuwa uwekezaji mkubwa.”