Familia zahangaishwa na ‘ugonjwa’ wa wazee kupotea jijini
NA FRIDAH OKACHI
IMEBAINIKA kwamba baadhi ya wazee, waume kwa wake, hukumbwa na matatizo ya kusahau njia wanapokuwa wametoka nyumbani kuenda sokoni na ama maeneo ya burudani au ya umma kwa shughuli mbalimbali.
Shirika moja linalofahamika kama Kenyan Aged Require Information, Knowledge, and Advancement almaarufu Karika, na ambalo linaloshughulikia maslahi ya wakongwe jijini Nairobi, hupokea wakongwe zaidi ya watano kila siku.
Wengi wao wakikosa kufahamu wanakotoka na majina ya waangalizi wao.
Msimamizi wa Karika, Elijah Mwega, aliambia Taifa Leo kwamba wazee hao hufikishwa katika ofisi za shirika ama na wasimamizi wa serikali au wapitanjia ili kuwasaidia kurudi nyumbani.
“Wale ambao mimi hupokea ni kutoka kwa machifu. Kuna wale wanaopelekwe katika vituo vya polisi na kwa kuwa hapa tunayo makao ya kuwastiri, wanaletwa hapa kuishi tunapoanza kutafuta familia zao,” akasema Bw Mwega.
Kulingana na msimamizi huyo, wanakabiliwa na changamoto kupata habari kutoka kwa wakongwe hao kwa sababu baadhi yao hugeuka na kuwa wakali.
“Huwa vigumu kutafuta jamaa wao kwa wale ambao hawana stakabadhi yoyote ya utambulisho. Ili kupata maelezo kamili sisi huhakikisha wanafurahia kula chakula kizuri na pia tunawapa sehemu nzuri ya kulala,” akaeleza afisa huyo.
Familia ya Judy Waceke yenye makazi yake katika wadi ya Waithaka jijini Nairobi, hulazimika kufunga lango la kutoka nje wanapoenda katika shughuli zao za kikazi ili kuzuia mama yao kupotea kila wakati.
Pia, wameungana kama jamii kuhakikisha kila mmoja wao anatoa kiasi kidogo cha pesa kumwajiri mjakazi wa kumwangalia mama yao siku ya Jumapili.
Bi Waceke aliambia Taifa Leo kwamba mamake mzazi amepotea zaidi ya mara sita. Alisema mzazi wake amepotea zaidi ya mara sita.
“Tunajaribbu kadri ya uwezo wetu, lakini huchoshwa anapopotea kwa sababu kumtafuta huwa ni kibarua kigumu. Akipata fursa ya kutoka, hatafahamu ni njia ipi alitumia hivyo kurudi huwa ni bahati nasibu. Lakini majirani wanaomfahamu wakati mwingine humrejesha hapa,” akasema Bi Waceke.
Kilomita 100 kutoka katika sehemu anakoishi Bi Waceke, familia ya Bi Alice Wangui inamtafuta baba mzazi aliyepotea miezi sita iliyopita.
Bi Wangui aliambia Taifa Leo kwamba babake amekuwa na matatizo ya kusahau njia kwa muda mrefu.
“Tumemtafuta kila mahali bila kumpata. Kwenye mitandao ya kijamii tumepakia picha zake, angalau akionekana hata kaunti nyingine waweze kuwasiliana nasi,” alidokeza Bi Wangui.
Wakati mwingine, wazazi wanaoachwa wakiwa upwekeni, huanza kuwa na fikra za kujitoa uhai wakihisi kuwa wanatengwa na kutelekezwa.
Utafiti unaonyesha kuwa kadri umri unavyozidi kusonga, ndivyo akili ya binadamu huwa katika uwezekano mkubwa wa kuwa na kumbukumbu ya chini.
Wakati mwingine hali hii husababisha ugonjwa wa ‘dementia’. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria ugonjwa huo hutatiza watu 1,827 na kusababisha vifo kwa asilimia 0.65
Kenya inaorodheshwa nambari 76 duniani kwa ugonjwa huo.