Hakuna ushahidi kuthibitisha bangi huathiri nguvu za kiume, ripoti yasema
NA CECIL ODONGO
DHANA kuwa bangi inachangia ukosefu wa nguvu za kiume huenda ikatokomea baada ya utafiti wa hivi punde kuonyesha kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha hoja hiyo.
Hii ni baada ya utafiti uliochapishwa kwenye International Journal of Impotence wiki hii kusema dawa hiyo ya kulevya haichangii mwanaume kukosa kuwika kitandani wakati wa tendo la ndoa. Ukosefu wa nguvu za kiume huwasababishia wanaume wengi msongo wa mawazo ndiposa ni vyema matibabu yakumbatiwe kuutibu.
Takwimu kutoka kwa mashirika mbambali za kiafya zimekisia kuwa idadi ya wanaume ambao wanakabiliwa na ukosefu wa nguvu za kiume huenda ikafikia watu milioni 322 kufikia mnamo 2025. Jinsi umri wa mwanaume hupanda ndivyo pia yupo katika hatari ya kutatizwa na ukosefu wa nguvu za kiume.
Ingawa hivyo, utafiti umeonyesha kuwa bangi haivurugi homoni za kiume ambazo huchochea mahaba kwa mwanaume. Wanasayansi waliozamia utafiti huo walibaini kuwa kemikali ambazo zinatokana na uvutaji bangi, hazikuwa na athari zozote katika kuundwa kwa mbegu za kiume au uume kukosa kudumisha ashiki wakati wa mapenzi.
Hata hivyo, utafiti zaidi unastahili kufanywa, kupata iwapo kuna uhusiano wowote ambao utafiti wa sasa haukuvumbua iwapo bangi inaathiri homoni za kiume. Hapo ndipo, mikakati ya kuzuia na kutibu ukosefu wa nguvu za kiume, itakumbatiwa.
Tafiti za awali zimeonyesha kuwa bangi ina kemikali inayofahamika kama maarufu kama delta-9-tetrahydrocannabinol (THC) ambayo husababisha homoni za kiume kushindwa kudumisha ashiki wakati wa tendo la ndoa.
Hii ni kwa sababu tafiti za awali zilibaini kuwa kemikali zinazotokana na bangi huvuruga homoni za akilini na huchangia kuathiri udhabiti wa uume wakati wa tendo la ndoa.