Hali zinazochangia saratani kuzuka upya hata baada ya ‘kupona’
MWAKA wa 2011, Bi Judy Wanyoike alianza kupata maumivu ya mgongo na kutokwa na damu ukeni, dalili ambazo hapo awali hakuweza kuzifafanua.
Hali hii iliendelea kwa miezi kadhaa hadi mwaka wa 2012 alipoambiwa kuwa alikuwa na saratani ya shingo ya kizazi.
“Nilikua nimeenda kwenye semina ya kanisa ya wiki moja huko Naivasha, ambapo mojawapo ya shughuli ilikuwa uchunguzi wa Pap Smear,” akumbuka.
Kwa mshangao wake, madaktari waligundua hitilafu wakati wa uchunguzi huo, na bila kupoteza muda akashauriwa kwenda katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta KNH kwa vipimo zaidi.
“Baadaye ilithibitishwa kuwa nilikuwa na saratani ya lango la uzazi ya hatua ya 2B.”
Ili kukabiliana na hali hii, Bi Wanyoike alifanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi, utaratibu uliondamana na matibabu ya tibakemia, tibaredio na utaratibu wa brachytherapy, ambapo baadaye alianza kupata nafuu.
Hata hivyo, mwaka wa 2019, kansa hii ilirudi. “Singeweza kwenda haja kubwa,” asema.
Kufika Septemba mwaka huo, hali yake ilikuwa imezidi kuwa mbaya kiasi kwamba hakuweza hata kupitisha hewa tumboni.
“Uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa nilikuwa na uvimbe, ambao ulitolewa kupitia upasuaji na kuonyesha kwamba ulikuwa na kansa.”
Bi Wanyoike alianza matibabu ya tibakemia na tibaredio ambapo mwezi Aprili mwaka wa 2020, alikamilisha taratibu hizi zote.
Lakini masaibu yake hayakuwa yamekwisha, kwani tena mwaka wa 2022, alianza kupata maumivu ya mgongo ambayo yalikuwa yamesambaa hadi shingoni.
“Nililazimika kufanyiwa tena vipindi vinne vya tibakemia na uchunguzi wa PET scan mwezi Agosti mwaka huu.”
Kulingana na wataalam, uwezekano wa kansa ya lango la kizazi kurudi hutegemea hatua ya saratani, aina ya matibabu, na hali ya mgonjwa.
“Kansa hurudi pale seli za kansa zinapobaki mwilini baada ya matibabu na kuanza kukua tena,” aeleza Dkt Catherine Nyongesa, mtaalamu wa matibabu ya kansa jijini Nairobi.
Sababu kuu ya kansa kurejea, asema, ni seli ndogo za saratani kubaki mwilini baada ya taratibu kama vile upasuaji, tibaredio na tibakemia.
Aidha, iwapo kansa itagundulika ikiwa tayari iko katika hatua ya juu, basi hatari yake kurejea huongezeka.
“Wakati huu, uwezekano wa maradhi haya kusambaa kwenye tishu au tezi za limfu huwa uko juu,”aeleza Dkt Nyongesa.
Tafiti za kitabibu zinaonyesha kuwa katika hatua za awali (Stage I) za kansa, uwezekano wa kansa ya lango la uzazi kurejea huwa kati ya asilimia 5 na 15, na mara nyingi hujirudia katika kipindi cha kati ya miaka 2 na 3 baada ya matibabu.
Kwa upande mwingine, aina hii ya kansa ikitambulika katika hatua ya pili au ya tatu (Stage II–III), uwezekano wa kurejea huongezeka na kuwa kati ya asilimia 30 na 40, huku iwapo ugonjwa huu utagundulika katika hatua za mwisho (Stage IV), hatari ya kurejea tena huwa imeongezeka pakubwa na kufikia asilimia 50.
“Katika hatua hii, ni vigumu kuondoa saratani yote kabisa,” aeleza Dkt Nyongesa.
Kulingana na Dkt Nyongesa, tatizo ni kwamba wanawake wengi huchelewa kwenda kufanyiwa uchunguzi, kumaanisha kwamba maradhi haya yanapogundulika, tayari huwa yamesambaa.
“Kwa bahati mbaya, hakuna ishara za mapema za maradhi haya, kumaanisha kuwa sio rahisi kwa mgonjwa kutambua kuwa ana tatizo. Tatizo ni kwamba wanawake wengi huenda hospitalini wakiwa wamechelewa ambapo mara nyingi kansa hii huwa imeenea katika sehemu zingine, na hivyo kufanya iwe ngumu kupokea matibabu na kuokoa maisha ya mgonjwa,” aeleza Dkt Nyongesa.
Takwimu zinaonyesha kwamba hapa nchini ni asilimia ndogo ya wanawake wanaogundulika kuwa na kansa ya lango la uzazi mapema na kufanyiwa matibabu kabla ya mambo kuwa mabaya.
Lakini pia kulingana na wataalam, maambukizi sugu ya HPV (hasa aina 16 na 18) yanaweza kuchangia kansa kuzuka tena, au ikiwa baadhi ya seli sugu za kansa ambazo hazikuangamizwa kupitia tibakemia na mionzi, zilisalia.
Kando na hayo, maradhi haya yanaweza kurejea ikiwa mfumo wa kingamwili ni dhaifu, au kulingana na mtindo wa maisha kama vile vutaji sigara, lishe duni, msongo wa mawazo na kutofuatilia matibabu ipaswavyo.
Kulingana na Dkt Nyongesa, dalili zinazoweza kuashiria kurejea kwa kansa ni pamoja na maumivu ya nyonga au mgongo, kutokwa na damu au ute usio wa kawaida, ugumu wa kwenda haja ndogo au kubwa, kuumwa miguu au miguu kuvimba, na kupungua uzani bila sababu.
Njia bora ya kudhibiti maradhi haya, Dkt Nyongesa asema, ni kufanya utambuzi wa mapema ambao hasa hufanywa kupitia uchunguzi wa pap smear unaosaidia madaktari kugundua vidonda au seli zisizo za kawaida kwenye lango la uzazi, na ambazo zaweza tibiwa kabla ya kugeuka na kuwa na uwezo wa kusababisha kansa.
Kulingana na mtaalam huyu, kupimwa ndio mbinu ya kutambua maradhi haya kwani yaweza saidia kuzuia aina nyingi za kansa ya lango la uzazi kwa kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye seli za lango la uzazi ili ziweze kutibiwa.