• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:03 PM
Kama mwanamke, kuota kwa nywele kwenye kidevu kwanipa taabu!

Kama mwanamke, kuota kwa nywele kwenye kidevu kwanipa taabu!

Mpendwa Daktari,

Mimi ni mwanamke na nakumbwa na shida ya kujithamini, kutokana na tatizo la nywele kuota miguuni, kwenye mapaja, mikononi, na katika sehemu inayozingira kidevu changu. Nimekuwa nikitumia wembe kunyoa lakini mbinu hii husababisha mkwaruzo. Pia, siwezi kumudu kufanyiwa utaribu wa kuondoa nywele wa electrolysis. Nifanyeje?
Naomi, Mombasa

Mpendwa Naomi,

Tatizo la nywele kuota kupindukia katika sehemu ambapo kwa kawaida huwa chache au hazipo kabisa (kama vile uso, kidevu na kifua kwa wanawake, kwenye tumbo na mgongo) inafahamika kama hirsutism.

Kwa kawaida nywele katika sehemu hii huwa nyeusi kupindukia, nyingi na ngumu. Tatizo hili huathiri takriban kati ya asilimia 5 na 10 ya wanawake.

Wakati mwingine, hali hii yaweza tokana na matatizo ya kihomoni na hivyo kuongeza viwango vya androgen, kwa mfano, polycystic ovarian syndrome (PCOS), au matatizo mengine yanayoathiri tezi adrenali.

Pia, kuna baadhi ya dawa ambazo huchochea nywele kuota kupindukia, kama vile dawa za steroid, phenytoin (zinazotumika kudhibiti kifafa), minoxidil (zinazotumika kukabiliana na shinikizo la damu), cyclosporine (zinazotumika kuzima nguvu za kingamwili). Pia shida hii yaweza chipuka baada ya kukatikiwa.

Ili kutibu hirsutism, litakuwa jambo la muhimu kuchunguza iwapo kuna matatizo mengine yanayoisababisha na kuyakabili.

Litakuwa jambo la busara kumuona daktari ili viwango vyako vya homoni na hasa androgen, vichunguzwe. Hapa pia kuna chunguzi zingine zitakazofanywa kama vile ultrasound au CT scan ili kukagua ovari na tezi adrenali. Hata hivyo, kuna wakati ambapo hata baada ya kudhibiti baadhi ya hali hizi, nywele hizo zitaendelea kuota.

Mbinu zisizodumu za kuondoa nywele kama vile kuonyoa, kufanya waxing au kutumia krimu za kuondoa nywele, zitakusaidia.

Krimu za Eflornithine hydrochloride (kwa mfano Vaniqa) zaweza pakwa ili kupunguza kasi ya nywele kuota, japo hazisitishi shida hii.

Unaweza mtembelea mtaalamu wa ngozi ili ufanyiwe utaratibu wa kudumu wa kuondoa nywele kwa kutumia laser/photoepilation, japo ni ghali.

Kupunguza viwango vya homoni za androgen mwilini kwaweza fanywa kwa kupunguza uzani ikiwa una uzani mzito, kudumisha lishe bora na kufanya mazoezi kila wakati.

Pia, hali hii yaweza kabiliwa kwa kutumia baadhi ya dawa kama vile mchanganyiko wa tembe za kupanga uzazi na spironolactone.

Unapaswa kutumia dawa hizi kwa angalau miezi sita (6) kabla ya kaunza kutambua mabadiliko kwani huchukua muda kabla ya nywele mpya kuota.

  • Tags

You can share this post!

Ruto kutafuta mtu mwingine baada ya Kemosi kukataa kazi ya...

Leteni hao majeruhi Bayern tuwape dozi, Arsenal sasa...

T L