Afya na Jamii

Kashfa ya uuzaji wa mbegu hatari za kiume yafichuliwa

Na MERCY CHELANGAT December 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RIPOTI mpya ya uchunguzi iliyotolewa na EBU Investigative Journalism Network imefichua kashfa kubwa barani Ulaya ambako mbegu za uzazi kutoka kwa mfadhili mmoja aliyekuwa na mabadiliko hatari ya kijenetiki yanayosababisha saratani zilitumika kuwazalisha angalau watoto 197.

Tukio hilo limeibua maswali mazito kuhusu ukosefu wa kanuni za kimataifa zinazosimamia sekta ya utoaji wa mbegu za uzazi duniani.

Mfadhili huyo alikuwa na mabadiliko katika jeni yanayohusishwa na ugonjwa unaoongeza hatari ya kupata saratani katika umri mdogo.

Kwa bahati mbaya, mabadiliko hayo hayakuwa yakichunguzwa kwa kawaida wakati mfadhili alianza kutoa mbegu mwaka 2005.

Kati ya watoto 67 wa mwanzo waliopatikana, 23 walibeba jeni hizo na 10 waligunduliwa na saratani. Mbegu hizo zilisambazwa na hifadhi ya mbegu za wanaume Denmark, kwa kliniki katika angalau nchi 14.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa mbegu za mfadhili huyo zilitumika zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa katika baadhi ya nchi.

Kukosekana kwa sheria za kimataifa kuhusu idadi ya watoto kwa mfadhili mmoja kumeruhusu idadi kubwa ya mbegu kuvuka mipaka ya kitaifa.

Kwa mfano, nchini Ubelgiji ambako kiwango ni familia sita, mbegu hizo zilitumika kuunda takribani familia 38.

Huku Kenya, utoaji wa mbegu za uzazi unaongezeka kutokana na uelewa kuhusu matibabu ya utasa, pamoja na fidia ya kifedha kwa wafadhili. Wanawake wengi wanaojitegemea kiuchumi pia wanachagua kupata watoto bila ndoa, hali inayoongeza mahitaji ya mbegu.

Changamoto za kiuchumi pia zimewafanya vijana kuchukulia utoaji wa mbegu kama chanzo cha kipato, huku malipo yakianzia Sh40,000 hadi Sh100,000 kwa mchango mmoja.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, daktari mtaalamu wa utafiti wa matibabu, Dkt Ahmed Kalebi, anasema mabadiliko ya kijenetiki ni mabadiliko ya kudumu katika DNA yanayoweza kurithishwa kupitia mbegu au yai.

Anaeleza kuwa baadhi ya magonjwa hurithiwa lakini hujitokeza mtu akiwa mkubwa, hivyo mfadhili anaweza kuonekana mzima wakati wa kuchangia.

Kwa sasa, Kenya haina sheria maalum ya kusimamia teknolojia ya uzazi wa kusaidiwa (ART), hivyo hakuna masharti ya lazima ya uchunguzi wa vinasaba kwa wafadhili au idadi ya watoto anayetoa mbegu anaweza kuchangia.

Kliniki nyingi hufuata viwango vya kimataifa kwa hiari. Hata hivyo, Mswada wa ART wa 2022, uliofanyiwa marekebisho yake Novemba 1, 2025, unalenga kuweka mfumo wa kisheria, kudhibiti idadi ya watoto hadi 10 kwa mfadhili, na kuanzisha mamlaka ya kitaifa ya kusimamia sekta hiyo.

Iwapo utapitishwa, uswada huo utaanzisha sajili ya kitaifa ya wafadhili, kliniki na watoto waliozaliwa kupitia ART, kuhakikisha uchunguzi wa vinasaba unafanywa, na kulinda familia dhidi ya hatari za kijenetiki.

Dkt Kalebi anasema hatua hizo zitasaidia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usalama wa uzazi wa kusaidiwa nchini Kenya.