Afya na Jamii

Kila sigara unayovuta, unapunguza uhai kwa dakika 19.5 – Utafiti

Na CECIL ODONGO January 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KWA kila sigara ambayo huvutwa, mtu hupunguza uhai wake ulimwenguni kwa dakika 19.5, Watafiti wamebaini.

Utafiti wa Taasisi ya Mafunzo ya London ulibaini kuwa wanaume hupunguza uhai wao kwa dakika 17 kutokana na kila sigara wanayovuta. Hatari hiyo hiyo ipo kwa wanawake ambao hupoteza dakika 22 kwa kila sigara wanayovuta.

Huu utafiti unaonyesha kuwa wanaovuta sigara wanajiweka hatarini zaidi ikizingatiwa kuwa tafiti za hapo awali zilikuwa zimeweka idadi ya dakika ambazo wanapunguza uhai wao kuwa 11 pekee kwa wanaume na wanawake.

Kwa kuwa kila pakiti ya sigara huwa ina sigara 20 hii ina maana kuwa ukivuta sigara zote basi umepunguza uhai wako hapa duniani kwa muda wa saa saba.

Vilevile utafiti huo ulianika hatari ambayo ipo kwa kuvuta hata sigara moja pekee kwa siku.

Kwa mwanaume, kuvuta sigara mara moja kwa siku kwa muda wa miaka 10 hupunguza uhai wako kwa dakika 62,050 ambazo zinaweza kufasiriwa kama siku 43.

Takwimu hizo ni juu kwa wanawake ambao utafiti huo umeonyesha kuwa maisha yao yatafupishwa kwa dakika 80,300 au siku 56.

“Kuvuta sigara ni ghali na pia kuna athari ambazo huishia kwa mauti kwa binadamu. Utafiti huu unaonyesha wazi hatari iliyoko katika kuvuta sigara na njia pekee ya kujikwamua ni kuwacha matumizi hayo,” ikasema utafiti huo.

“Utafiti huo unaonyesha watu hupoteza dakika 20 ya uhai wao kwa kila sigara ambayo wanavuta. Kadri mtu anavyoendelea kuvuta sigara ndivyo anapunguza uhai wake na jinsi anavyokomesha tabia hiyo ndivyo anarefusha uhai wake,” ikaongeza utafiti huo.

Kando na kupunguza siku za uhai, uvutaji wa sigara pia huandamana na magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari, kupoteza fikra na magonjwa hatari ya mapafu.