Kinachofanya wanaume kuamua ‘kufa kimende’ wakikumbwa na changamoto za kimaisha
WANAUME wamekuwa wakilemewa na matatizo ya msongo wa kiakili kutokana na changamoto za kikazi na kifamilia.
Hata hivyo, imebainika kuwa wengi wao huchelea kufichua matatizo yao kwa wenzao kazini au watu wa familia zao.
Hii ndio maana Sera kuhusu Afya ya Kiakili Nchini ya 2015 hadi 2030 inawahitaji waajiri kutekeleza mipango ya kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na hali zinazoweza kuwasababishia msongo wa kiakili.
Nao watetezi wa haki za afya ya kiakili wanasisitiza kuwa wanandoa ndio wanafaa kutoa usaidizi wa kwanza kwa waathiriwa.
Mara nyingi Chris* hujipata akikabiliana na mahitaji yake ya kitaaluma na haja ya kupata utulivu.
Mwanamume huyu, mwenye tajriba ya miaka 14 katika taaluma ya mawasiliano, anaona ni vugumu kwake kumjulisha mkewe kuhusu matatizo ya kiakili yanayomzonga.
“Kila mara bosi wangu hunilazimu kufanyakazi nyingi ambayo ingefanywa siku itakayofuata,” anasema Chris, ambaye anaongoza kitengo cha mawasiliano katika kampuni moja ya Uhusiano wa Mwema.
“Nahitajika kufika afisini saa mbili asubuhi (8.00am) na kuondoka saa kumi na moja jioni (5.00pm), lakini mimi hufika nyumba saa tano za usiku baada ya kufanyakazi kwa saa zaidi,” anaongeza.
Siasa za ofisini na kukosewa heshima na wadogo wake kazini huzidisha matatizo yake.
Kikosi chake kinapokosa kutimiza malengo yake ya kila mwezi kutokana na sababu zisizoepukwa kama vile kuugua kwa wafanyakazi na washindani kutwaa wateja—bosi wake humzomea mbele ya wadogo wake.
“Mwanzoni, nilimpigia siku mke wangu kumweleza masaibu yangu, lakini alifanya mambo kuwa mabaya zaidi,” Chris anaeleza.
“Mke wangu angetaka kufahamishwa kuhusu mahusiano yangu kazini na kutisha kuwakabili wafanyakazi wenzangu.” anaongeza.
Kwa hivyo, baada ya kuhisi kuwa mkewe hangemsaidia, Chris aliamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine ambaye alimtaja kama anayejali na kuelewa.
“Kuhusu mke wangu, ni heri nife kimya kimya badala ya kumweleza yanayonizonga,” anakiri.
“Badala ya kunipa usaidizi, hunifanya kuhisi kama ninayelengwa kwa kulemewa na msongo wa kikazi,” Chris naongeza.
Anayoyapitia Chris sio ya kipekee.
George* meneja katika benki moja inayokabiliwa na changamoto nyingi, anakabiliwa na presha nyingi hata zaidi.
“Sharti nielezee kuhusu mikopo isiyolipwa na idadi ndogo ya wateja wanaochukua mikopo mipya, haswa uchumi wa nchi unapopitia wakati mgumu,” anasema.
“Hali hii inachangiwa na maswala ambayo siwezi kuyadhibiti, ilhali mimi ndiye hulaumiwa,” George anasema.
Hii ndio maana George huamua kusakata densi za Kikalenjin na kuimba kwa sauti ya juu wakati wa ibada kanisa.
Nyakati zingine hujiliwaza kwa kutizama mechi ya kandanda ya ligi kuu ya Uingereza haswa timu ya Arsenal inapocheza.
Kulingana na Wizara ya Afya, karibu asilimia 25 ya wagonjwa wanaotibiwa na kwenda nyumbani na hadi asilimia 40 ya wanaolazwa katika vituo vya afya wanaugua magonjwa ya akili yanayohusishwa na mfadhaiko, matumizi wa dawa za kulevya, na wasiwasi.
“Nimeshughulikia visa ambapo majibu ya mke yalizidisha matatizo ya akili ya mume, na hatimaye kupelekea kufutwa kazi,” anasema Fanuel Demesi, mchungaji katika Kanisa la Friends International Center, ambaye mara nyingi huwashauri wanaume.
“Tunawahimiza wanandoa kusikiliza wenzao na kutoa usaidizi unaohitajika. Wanaume pia ni wanadamu na wanahitaji faraja na mwongozo wakati wa magumu.”
Mwanasaikolojia Daniel Kariuki anaonya wanaopuuza mafadhaiko unaokumba wanaume kutokana na kazi zao.
“Wanapokuwa chini ya shinikizo, wanaume wengi huwakashifu wale walio karibu nao: wake zao au watoto,” anaeleza. ”
Afya ya akili ni suala muhimu ambalo haliwezi kupuuzwa. Uelewa na ushauri ni muhimu,” asema.