Afya na Jamii

KINAYA: Baada ya zogo la Duale na Kibagendi, natamani mawaziri na wabunge wazichape tu!

October 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATI ya wabunge na mawaziri, unamwamini nani? Ati hujui? Au huna hakika? Hata mimi. Ni sawa na kuniuliza kati ya mbwa koko na fisi, wa kuaminiwa mfupa ni nani.

Hata wewe unajua fika kuwa mwisho wa siku, mfupa utatafunwa tu. Tofauti ni kasi ya kuutafuna. Kimsingi, huwezi kumtuma yeyote kati yao kumfikishia mtu mfupa.

Hawakutupaka mafuta kwa mgongo wa chupa waliponena wahenga kuwa mbuzi na ng’ombe wamoja, kondoo mtu wa kando.

Mimi nawe watu wa kando, wabunge na mawaziri wamoja, ndiyo maana sisisimki nikiona vioja vyao.

Wana hulka ya wezi wa Nairobi, ambao hukuibia, kisha wanakimbia huku wakipiga mayowe na kuwaelekeza watu wamnase mwizi, kumbe kaiba wao.

Hilo likijiri mtaani, mwenzako huegemea ukuta na kuwatazama washamba wakiingizwa mjini kishenzi!

Hivi, kama mimi, umewahi kutamani watu wazichape hadharani, ushangilie kwa kuwa hakuna anayelima kwenu? Huo ni msemo wa kikwetu, na hutumiwa ugomvi unapotokea kati ya watu ambao huna huruma nao.

Wakitaka kulana maini, kung’oana macho au hata kukatana masikio, kwako ni sawa tu, miereka yao haili kwako kamwe. Hisia za aina hiyo ni ithibati kuwa umechoka kuhadaiwa.

Ukifuatilia ugomvi wao, aghalabu unaachwa ukijiuliza ni yupi msema kweli, unaishia kujijibu: hata mimi sijui, wote ni washukiwa ambao bado hawajapatikana na hatia.

Juzi nimemuona Waziri wa Afya, Aden Duale, akikaribia kuzichapa na Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, kuhusu matatizo ya bima ya afya nchini – SHA.

Nilikodoa macho ili niwaone vizuri, huku nikiomba kimoyomoyo wakabane koo na kuchaniana magwanda ili niburudike.

Wakenya wa kawaida tumeteseka siku nyingi, na watesi wetu tunawajua: wabunge na utendaji, yaani ofisi ya rais.

Kibagendi alidai Duale ni mwizi sugu wa hela za SHA. Duale naye, kwa kiburi cha ibilisi, akamjibu kwa madai kwamba mbunge huyo ni mmiliki wa hospitali binafsi inayonufaika kwa pesa za SHA.

Moyoni nilijiambia Duale hasemi kweli, nikatamani azabwe kibao cha uso aone vimulimuli, lakini Kibagendi akaniangusha.

Unawezaje kusingiziwa mbele ya kamera za runinga za kitaifa kisha umwache mtu hivyo?

Si angemzaba mtu kofi kisha akariri ile sheria inayoruhusu wabunge kukosa adabu wakiwa bungeni? Alimwacha vipi? Kwani yeye si mwanamume kamili? Ningekuwa hapo ningemhimiza afanye kitu.

Ona sasa, tayari nilikuwa nimeanza kumpendelea Kibagendi, kisha nikamkumbuka aliyekuwa spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, akieleza ulivyo ulafi wa wabunge, eti wanadai ‘ahsante’ zao kwa watu wanaofika mbele yao.

Niliishia kusema kuwa vita vya mbuzi na ng’ombe siviwezi, nikachukua jembe na kuelekea shambani.

[email protected]