Afya na Jamii

Kuandaa kabeji uifurahie kama vile unavyofurahia nyama!

January 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA PAULINE ONGAJI

Msimu wa sikukuu umekamilika kumaanisha kwamba uhalisi wa maisha umeanza kuwarejelea wengi. Mojawapo ya mambo ambayo yamekuwa yakijadiliwa hasa humu nchini ni chakula ambacho kitawafaa wengi wakati huu wa kiangazi.

Kwa mara kadhaa, mboga za kabeji zimetajwa kama chakula nafuu kitakachowafaa wengi wakati huu. Mboga hizi zina viwango vya juu vya kemikali za antioxidants kama vile vitamini C, mbali na kuimarisha hali ya kinga mwilini.

Lakini tatizo ni kwamba sio wengi wanaojua jinsi ya kupika chakula hiki. Ikiwa wewe ni mmoja wao, mbinu hizi zitakupa uandalizi mzuri wa mboga hizi.

Kupika kitoweo cha kabeji

Pasha mafuta katika chungu kikubwa huku kiwango cha moto kikiwa ni cha kati. Ongeza robo ya kabeji iliyokatwa kwa vipande vikubwa na uendelee kukoroga kwa kipindi cha kila baada ya dakika tano. Ongeza supu ya kuku au mboga, chumvi, pilipili na uache mboga zitokote. Funika chungu kisha upunguze kiwango cha moto na mboga ziendelee kuiva taratibu kwa kati ya dakika 15 na 20. Nyunyizia siki au juisi ya ndimu juu kisha ukoroge na kuandaa pamoja na ugali, chapati au wali.

Kupika kabeji kwa mvuke

Weka kifaa malum cha mvuke kwenye chungu kikubwa. Ongeza maji ya kutosha kujaza sehemu ya chini ya chungu lakini uhakikishe kwamba hayafikii kifaa cha mapishi ya mvuke. Chemsha maji. Ongeza kabeji juu ya kifaa cha mapishi ya mvuke kisha ufunike na uache mboga ziendelee kuiva kwa kati ya dakika 10 na 12. Koleza kwa chumvi, pilipili na viungo vingine kisha uandae.

Kukaanga kabeji kwa mafuta

Pasha mafuta kwenye chungu kikubwa huku kiwango cha moto kikiwa cha juu. Ongeza kabeji na endelee kupika huku ukiendelea kukoroga kila baada ya dakika 7 na 10. Koleza kwa chumvi, pilipili na viungo vingine upendavyo kisha uandae mara moja. Unaweza imarisha ladha ya chakula hiki kwa kuongeza viungo vingine kama vile kitunguu saumu, tangawizi, mafuta ya simsim au mchuzi wa soya.

Kuchemsha kabeji

Jaza chungu kwa maji ya chumvi kisha uchemshe. Ongeza kabeji zilizokatwa kwa vipande vikubwa. Funika na uache mboga ziendelee kuchemka kwa kati ya dakika 15 na 20 na upinduea mara moja pekee. Ondoa maji hayo kisha urejeshe chungu motoni kwa kati ya dakika 2 na 3 hadi unyevu uliosalia ukauke. Ongeza siagi na ukoleze kabla ya kuandaa.

Kuoka kabeji

Pasha oveni moto huku kiwango cha joto kikiwa nyuzi 128. Katakata kabeji kwa vipande vikubwa. Nyunyiza mafuta kwenye sinia la kuoka kisha upange vipande vya kabeji juu yake. Koleza kwa chumvi, pilipili na viungo vingine upendavyo. Oka kwa kati ya dakika 25 na 35 hadi kabeji zibadili rangi na kuwa hudhurungi. Pindua na uandae.