Magari ya umeme yanapunguza uharibifu wa mazingira na vifo, ripoti ya WHO yaonyesha
NA PAULINE ONGAJI
NYUMBANI kwake katika mtaa wa Kawangware, Kaunti ya Nairobi, Bw Chris*, anajiandaa kuelekea kazini, ambapo anahudumu kama manamba katika kituo cha magari ya umma cha Congo.
Ni wiki kadhaa tangu baba huyu wa watoto wawili afanye kazi, kwani alikuwa akipokea matibabu kutokana na maradhi ya pumu.
Mwezi Januari, Bw Chris aligundulika kuwa na ugonjwa huu, shida ambayo hakuwa nayo awali. “Nilipoenda hospitalini, daktari aliniuliza iwapo mimi ni mvutaji sigara, vile vile aina ya kawi ninayotumia katika mapishi nyumbani kwangu.”
Bwana huyu asema kwamba hajawahi vuta sigara maishani mwake, na kwamba nyumbani kwake, ni gesi ambayo imekuwa ikitumika katika mapishi jikoni.
Hata hivyo, asema kwamba ilikuwa baada ya kumwambia daktari kuhusu kazi anayofanya, ndipo kichocheo cha ugonjwa wake kilitambuliwa.
“Kwa zaidi ya miaka kumi nimekuwa nikifanya kazi kama kondakta wa magari ya umma, ambapo majukumu yangu huwa ni kuita abiria na kuhakikisha kwamba mabasi yamejaa kabla ya kwenda jijini.”
Kwa hivyo, mara nyingi Bw Chris asema, yeye huwa wazi kwa moshi wa magari mchana kutwa. “Nilipomfichulia daktari haya aliniambia kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba shida hii ilitokana na hewa chafu ya moshi wa magari, ambayo nimekuwa nikipumua hasa nikiwa kazini,” aeleza.
Kulingana na wataalam wa kiafya, ugonjwa wa pumu ni mojawapo ya maradhi yanayosababishwa na hewa chafu hasa kutokana na moshi wa gari zinazotumia mafuta yanayochimbwa au visukuku, yaani fossil fuels kwa Kiingereza.
Kulingana na Mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira (UNEP), sekta ya uchukuzi wa umma jijini Nairobi huchangia kufikia asilimia 60 ya vichafuzi hewa.
Utafiti wa UNEP uliopima viwango vya vichafuzi hewa
Utafiti wa UNEP uliopima viwango vya vichafuzi hewa kwenye barabara jijini Nairobi, ulionyesha kwamba wakazi wa eneo hili wako wazi kwa chembechembe ndogo za matini hewani, zaidi ya viwango vinavyopendekezwa na shirika la WHO.
Wataalam wanasema kwamba sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya vyanzo vya uchafuzi wa hewa hapa Kenya, kwa sababu sekta hii huhusisha hasa magari makuukuu yanayotumia kawi zinazochimbwa.
“Magari haya huzalisha vichafuzi hewa hatari kama vile chembechembe ndogo za mata hewani (PM 22.5 na PM 10), gesi za nitrogen oxide, carbon monoxide, miongoni mwa vichafuzi vingine,” aeleza Bw Sammy Simiyu, mtaalam wa afya ya umma.
Kulingana na Bw Simiyu, vichafuzi hivi vina athari kubwa kwa afya. “Baadhi ya maradhi ambayo yamehusishwa na hewa chafu ya magari haya, ni pamoja na kansa, magonjwa ya moyo na maambukizi ya mfumo wa kupumua kama vile ugonjwa wa pumu na maradhi sugu yanayoathiri njia ya kupumia kwenye mapafu yaani chronic obstructive pulmonary disease (COPD) kwa Kimombo, ambayo husababisha uharibifu kwa mapafu na kuchochea kansa ya mapafu.
Utafiti wa Shirika la Afya Duniani WHO, unaonyesha kwamba uchafuzi wa hewa mijini hasa kutoka kwa magari haya, unahusishwa na zaidi ya vifo milioni 1.3 duniani kila mwaka.
Mwezi Novemba mwaka jana, ripoti ya Clean Air Fund ilionyesha kwamba Nairobi ni mojawapo ya miji sita barani Afrika, ambayo imeathirika pakubwa na uchafuzi wa hewa, na hivyo kusababisha vifo vingi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, mwaka wa 2022, uchafuzi wa hewa ulisababisha zaidi ya vifo 56,400 vya mapema katika miji sita mikuu barani, ikiwa ni pamoja na Nairobi, Accra, Cairo, Johannesburg, Lagos na Yaoundé.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linaonyesha kwamba uchafuzi wa hewa huchangia takriban vifo milioni saba ulimwenguni kila mwaka.
Aidha, shirika la WHO linakadiria kwamba asilimia 80 ya maradhi yasiyoambukizwa hutokana na sababu ambazo zaweza kuzuiwa, kama vile kemikali hatari za kimazingira, ikiwa ni pamoja na vichafuzi hewa.
Kulingana na wataalam, mojawapo ya mbinu za kupunguza uchafuzi wa hewa ni kwa motokaa za sekta ya uchukuzi kama vile mabasi, kutumia kawi mbadala kama vile umeme.
Magari ya kieletroniki yana uwezo wa kupuguza uchafuzi wa hewa
Tafiti kadhaa zinaonyesha kwamba magari ya kieletroniki yana uwezo wa kupuguza uchafuzi wa hewa kutokana na gesi ya kaboni, vile vile kuimarisha ubora wa hewa.
Na ndiposa kwa miaka sasa kumekuwa na wito kwamba motokaa zinazotumia kawi za visukuku kupunguzwa barabarani, na zile za umeme kuongezwa.
Hapa nchini, mwaka jana kampuni ya Roam inayohusika na kuunda magari na pikipiki za umeme, ilizindua basi ya umeme ya usafiri wa umma.
Kulingana na Bw Dennis Wakaba, afisa mtendaji wa mauzo wa kampuni hiyo hapa nchini, mabasi haya yatasaidia kushusha matumizi ya kawi za visukukuu, na hivyo kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochafua hewa.
Kulingana na Shirika la Nishati Duniani IEA, mwaka wa 2022, zaidi ya magari milioni 26 ya umeme yalikuwa barabarani, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 60 ya jinsi mambo yalivyokuwa mwaka wa 2021, na zaidi ya mara tano kuliko idadi ilivyokuwa mwaka wa 2018.
Gari za umeme zimethibitishwa kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa njia mbalimbali. Kwa mfano, hazitoi gesi hatari zinazopitia kwenye bomba la hewa chafu ya gari kama zile zinazotumia kawi za visukukuu, zikiwepo Carbon Monoxide (CO), Nitrogen Oxides (NOx), Hydrocarbons (HC), na chembechembe ndogo za matini hewani (PM) ambazo huchangia pakubwa uchafuzi wa hewa nje ya majengo.
Lakini kumekuwa na wasiwasi kuhusu magari haya, huku masuala kadha wa kadha yakiibuka kuhusu ikiwa matumizi yake yatawezekana au iwapo hii ni ndoto tu.
Gharama ya kununua mafuta
“Japo imenipunguzia gharama ya kununua mafuta, na ni kweli kwamba magari haya hayachafui hewa, kupata vituo vya kuweka nguvu za umeme na muda wa kufanya hivyo ni changamoto. Pia, mwendo wa kuendesha gari likiwa limejaa nguvu za umeme pia ni changamoto,” aelezea Oscar*, mwendeshaji teksi jijini Nairobi, ambaye amekuwa akitumia gari la umeme kwa miaka miwili sasa.
Kando na hayo, wataalam katika sekta hii pia wameangazia gharama za juu za mwanzo wakati wa kununua gari la umeme, vile vile kununua betri ni ghali mno.
Lakini licha ya changamoto hizi, wataalam wanashawishika kwamba gari za umeme ndio suluhisho kuu la kukabiliana na tatizo la uchafuzi wa hewa unaotokana na magari.
Kulingana na Bw Simiyu, athari za uchafuzi wa hewa kwa afya ya binadamu, mazingira na uchumi ni kubwa, kumaanisha kwamba serikali, sekta za kibinafsi na raia, sharti wachukue hatua kupunguza uzalishaji hewa chafu na kuimarisha ubora wa viwango vya hewa.
“Mojawapo ya njia za kufanya hivyo ni kupunguza uzalishaji hewa chafu kupitia magari.”