Maradhi ya selimundu yanavyotesa mamilioni Afrika
NA PAULINE ONGAJI
AKIWA na miezi minane, Bi Eunice Awino, mkazi wa Kaunti ya Nairobi, aligunduliwa kuwa na maradhi ya selimundu, na tokea wakati huo, maisha yake yalibadilika yakawa magumu.
Katika maisha yake, anasema kwamba muda wake mwingi ameutumia hospitalini akipokea matibabu, suala ambalo mbali na kumuathiri kisaikolojia na kimwili, lilikuwa pigo kwa masomo yake.
“Nikiwa mwanafunzi, mara nyingi ningekuwa mgonjwa na kulazwa hospitalini hata kwa mwezi moja, hivyo ilikuwa changamoto kushindana na wenzangu,” aeleza.
Hata hivyo, mzigo mkubwa hata zaidi ulikuwa wa kifedha kwa familia yake.
“Ili kudhibiti hali hii, lazima nitumie dawa. Kwa sasa mimi hutumia zaidi ya aina sita za dawa. Aidha, sharti niende hospitalini kukaguliwa angalau kila baada ya miezi mitatu,” aeleza Bi Awino.
Vilevile, chakula chake kilikuwa maalum ambapo sharti lazime kingejumuisha mboga na matunda, ambapo hii pia ilikuwa gharama kwa wazazi wake.
Hii ndio taswira inayowakumba wagonjwa wengi wa maradhi ya selimundu hapa barani Afrika, huku tafiti zikionyesha kwamba ugonjwa huu unaendelea kuwa kero kwa wengi hasa hapa Afrika.
Selimundu ni kikundi cha matatizo yanayosababisha seli nyekundu za damu kubadilika na kuchukua umbo la mundu.
Seli hizi hufa mapema, na hivyo kusababisha uhaba wa seli nyekundu za damu zenye afya (anemia ya selimundu), kisha kuziba mtiririko wa damu, na hatimaye kusababisha maumivu.
Wataalamu wa masuala ya afya wanahofia kwamba mzigo wa ugonjwa wa selimundu unaendelea kuwa mzito hapa Afrika, na endapo hatua zinazohitajika hazitachukuliwa, huenda maradhi haya yakalemaza kabisa mifumo ya afya ya wengi hapa barani.
Ndiposa katika kongamano la kwanza kuhusu Mkakati wa PEN-Plus kuangazia maradhi yasiyoambukizwa barani (ICPPA), majuma mawili yaliyopita nchini Tanzania, wataalamu wa afya walielezea hofu kwamba bara hili linaendelea kukodolea macho hatari.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), miongoni mwa watu milioni 120 wanaoishi na maradhi ya selimundu ulimwenguni, zaidi ya asilimia 66 yao wanaishi barani Afrika.
Aidha, kati ya asilimia 75 na asilimia 85 ya watu hawa ni watoto wanaozaliwa barani Afrika. Asilimia hii ni sawa na watoto 240,000.
Nchini Kenya, inakadiriwa kwamba watoto 6,000 huzaliwa wakiwa na maradhi ya selimundu kila mwaka, ambapo wataalamu wanahoji kwamba huenda idadi hii ikaongezeka kufikia mwaka wa 2050.
Barani Afrika, vifo 38,403 kutokana na maradhi ya selimundu, vilirekodiwa mwaka wa 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26, kutoka mwaka wa 2000, huku mzigo huu ukitokana na uwekezaji duni katika jitihada za kukabilia maradhi haya.
Kwa mujibu wa Dkt Jane Hankins, kutoka Idara ya Himatolojia katika hospitali ya utafiti ya watoto ya St Jude Children’s Research Hospital nchini Amerika, mojawapo ya mbinu za kupiga vita maradhi haya ni kuwepo kwa vituo vya kutosha vya kupima ugonjwa huu hasa miongoni mwa watoto wanaozaliwa.
Lakini Dkt Hankins asema kwamba mataifa ya Afrika yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa vituo hivi. Kulingana naye, kutokuwepo kwa mfumo maalum wa kuchunguza maradhi haya miongoni mwa watoto barani Afrika ni kizingiti kikuu katika matibabu ya ugonjwa huu.
“Matatizo mengi ya kiafya yanayohusishwa na maradhi haya huathiri hasa watoto chini ya miaka mitano, na hivyo utambuzi wa mapema ni muhimu ili kuanzisha matibabu mapema, na hivyo kuzuia matatizo hatari ya kiafya,” aeleza Dkt Hankins.
Barani Afrika, kati ya asilimia 50- 90 ya watoto wanaozaliwa na maradhi haya, hufa kabla ya kutimu miaka mitano, sababu kuu ikiwa kwamba mataifa husika hayana uwezo wa kutibu maradhi haya.
Hapa nchini, asilimia 90 ya watoto wengi wanaougua maradhi haya hufa kabla ya kutimu umri huu.
Ndiposa mwaka wa 2021, Chama cha Himatolojia nchini Amerika (ASH) kilianzisha ushirikiano na wanahimatolojia barani Afrika, pamoja na wataalamu wengine wa afya, kuanzisha ASH Consortium on Newborn Screening in Africa (CONSA), muungano wa kimataifa unaonuia kuonyesha umuhimu wa kupima selimundu miongoni mwa watoto wachanga, kama mbinu ya kukabili maradhi haya.
Lakini pia, hata miongoni mwa watu wakomavu, suala la kupima ili kujua hali yao, limekuwa changamoto licha ya kuwa ni hatua muhimu sana katika kukabiliana na ongezeko la watoto wanaozaliwa wakiwa na maradhi haya.
“Ni muhimu kujua ikiwa mwili wako unazalisha seli nyekundu za damu zinazochochea selimundu. Unaweza kujua hali yako kwa kufanyiwa uchunguzi wa damu. Aidha, unaweza kufanyiwa uchunguzi wa kijenetiki kwenye damu. Hatua hii itasaidia kugundua ikiwa una jeni za selimundu ambazo pia unaweza kupitisha kwa mtoto wako,” aongeza Dkt Angela Munoko, mwanapatholojia jijini Nairobi.
Kulingana naye, kunapaswa kuwa na mikakati dhabiti ya mwongozo kamili kuhusu udhibiti wa ugonjwa huu ili kupunguza mzigo wa maradhi ya selimundu miongoni mwa Wakenya.
Dkt Munoko asema kwamba kunapaswa kuwa na kampeni dhabiti za uhamasishaji kuhusu maradhi haya.
“Watu wanafaa kuelimishwa kuhusu maradhi haya, umuhimu wa matibabu ya mapema, vilevile umuhimu wa ushauri wa kijenetiki wakati wa kuchumbiana, kabla ya watu kufunga ndoa,” aeleza.
Lakini zaidi ya yote, wataalamu wa maradhi haya wanasisitiza umuhimu wa serikali za Afrika kuchukulia suala la maradhi ya selimundu kwa uzito.
Kwa mujibu wa Prof Jenifer Knight-Madden, Profesa wa kitengo cha utafiti wa maradhi ya selimundu katika Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Caribbean, katika Chuo Kikuu cha West Indies, ili mataifa ya Afrika yashinde vita dhidi ya maradhi haya, lazima matibabu ya maradhi haya yajumuishwe kwenye mfumo msingi wa afya katika nchi hizi.