Afya na Jamii

‘Matatizo ya moyo yalivyonihangaisha Kenya na ng’ambo’

June 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA PAULINE ONGAJI

TANGU utotoni, Bi Ruth Ngwaro, 34, kutoka kijiji cha Gathanje, Kaunti ya Kiambu, amekuwa akiishi na maradhi ya moyo.

Ni ugonjwa ambao ulimlazimu kukaa hospitalini kila mara. Anasimulia kisa chake cha jinsi alivyopambana na maradhi haya sio tu hapa nchini, bali pia ng’ambo.

Hii hapa simulizi yake:

“Nilizaliwa na shimo kubwa katikati ya moyo ambapo damu ilikuwa inavuja katika mojawapo ya valvu. Shida hii ilisababisha moyo wangu kuwa mkubwa.

Wazazi wangu waligundua kwamba nilikuwa na shida nikiwa na miezi minane pekee. Wakati huo, sikuweza kufanya mambo ya kawaida kama watoto wengine wachanga, kama vile kunyonya, ambapo kila mara madaktari walinitibu maradhi ya nimonia.

Ni hapa ndipo baada ya kupelekwa hospitalini, madaktari waligundua kuwa nilikuwa na matatizo ya moyo, na kwamba ningehitaji upasuaji kurekebisha shida hiyo.

Tokea hapo, sasa kazi ilikuwa kudhibiti hali hii huku azma ya madaktari ikiwa kuhakikisha kwamba naishi maisha bora.

Wakati huo, hakukuwa na huduma ya upasuaji wa kutatua shida yangu humu nchini.

Mwaka wa 1993 nikiwa na miaka mitatu, nilibahatika kuchaguliwa miongoni mwa mamia ya watoto wenye matatizo ya moyo, kupitia mpango wa Heart to Heart programme kutoka nchini Amerika. Mradi huu ulikuwa ukisaidia watoto kutoka mataifa yanayostawi walio na matatizo ya kiafya yaliyohitaji upasuaji, ilhali wazazi wao walikuwa maskini.

Nilisafirishwa hadi kituo cha Chuo Kikuu cha University of Maryland Medical centre ambapo nilifanyiwa upasuaji.

Lakini sikupata nafuu ambapo nilikumbwa na shida ya kutembea, kila mara nilikuwa mchovu, na vidole vyangu viligeuka na kuwa rangi ya samawati.

Madaktari walilazimika kufanya ukaguzi zaidi ambapo waligundua kwamba moyo wangu ulikuwa na mashimo manne, na hivyo nikalazimika kufanyiwa taratibu mbili za upasuaji katika kipindi cha wiki mbili.

Baadaye nilianza kupata nafuu na kurejea nchini Kenya na hata kuendelea na maisha.

Badilisha

Lakini huo haukuwa mwisho wa masaibu yangu.

Nilipokuwa nchini Amerika, madaktari hawakurekebisha mojawapo ya vali moyoni mwangu, ambayo ilikuwa ikivuja.

Walikuwa wanafaa kuibadilisha na ile bandia, lakini waligundua kwamba iwapo wangefanya hivyo, basi ningehitaji upasuaji mwingine baadaye maishani ili kuibadilisha, na hivyo, suluhu ilikuwa kudhibiti tatizo la vali kwa kutumia dawa.

Hii iliendelea hadi mwaka wa 2001, ambapo nilianza kushuhudia ishara zilizonikumba awali. Kwa mfano, ningekumbwa na maumivu sehemu ya kushoto ya moyo, na singeweza kufanya mambo ya kawaida.

Nilikuwa mchovu ambapo hata singeweza kutembea kwenda shuleni.

Nilirejeshwa kwa daktari wa moyo hapa nchini na kufanyiwa chunguzi kadhaa, ambapo waligundua kwamba vali yangu ingine ilikuwa na uvimbe ambao ulikuwa ukiziba njia ya damu kuelekea moyoni. Pia, vali ile ya mwanzo bado ilikuwa inavuja.

Ushauri

Wakati huu ilikuwa ngumu kupata daktari ambaye angekubali kunifanyia upasuaji, sio tu humu nchini, bali pia ng’ambo.

Wazazi wangu walijaribu kutafuta ushauri kutoka kwa madaktari hadi India, lakini bado haikuwezekana.

Lakini mwaka wa 2001 nilifanyiwa upasuaji mwingine hapa nchini ambapo waliondoa uvimbe katika vali iliyokuwa imeathirika, na ile iliyokuwa ikivuja ikaondolewa na nikawekewa ya bandia.

Mwaka wa 2019, familia yangu ilihamia nchini Amerika ambapo mwaka mmoja baadaye, nilienda hospitalini kufanyiwa ukaguzi wa kawaida.

Kwa kawaida, ukiwasili nchini humo lazima ufanyiwe uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kuingizwa katika mfumo wao wa afya.

Hapa ndipo wahudumu wa afya waligundua tatizo langu na mara moja wakanituma kwa daktari wa moyo ili kufanyiwa chunguzi zaidi.

Waligundua kwamba nilikuwa na hali inayofahamika kama atrial fibrillation, ambapo moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi sana.

Nilipelekwa mara moja katika hospitali ya watoto ambapo baada ya uchunguzi zaidi, madaktari walipendekeza nifanyiwe upasuaji mwingine.

Lakini baada ya upasuaji, madaktari waligundua kwamba nilikuwa na tatizo lingine kwa jina, complete heart block, au mpigo usio wa kawaida wa moyo.

Ilibidi niwekewe kidhibiti kasi ya moyo (pacemaker), na wakabadilisha vali bandia niliyokuwa nayo, na ingine mpya.

Nilianza kuhisi vyema lakini miezi sita baada ya upasuaji, nikaanza kukumbwa na hali inayofahamika kama arrhythmia, au mpigo usio wa kawaida wa moyo.

Hali hii ilinifanya kuhisi dhaifu na kukumbwa na kisunzi kila mara ambapo kuna wakati ningeshindwa kupumua na kukumbwa na maumivu ya moyo.

Madakatari walilazimika kufanya utaratibu unaofahamika kama ablation,ambao husaidia kuvunja mawimbi yasiyo ya kawaida ya kieletroniki yanayosababisha mpigo usio wa kawaida wa moyo.

Miezi mitatu

Kwa miaka mitatu nilikuwa nikifanyiwa utaratibu wa ablation kila baada ya miezi mitatu.

Hii iliendelea hadi Machi mwaka jana ambapo madaktari waliamua kufanya utaratibu wa kudumu wa ablation, na tangu wakati huo hali yangu imeimarika.

Kwa sasa, naweza kufanya shughuli za kawaida. Pia, tofauti na awali ambapo nililazimika kutumia dawa nyingi, sasa natumia tu dawa za kuyeyusha damu.

Hii ni muhimu kwa sababu ukitumia vali bandia, damu haipaswi kuwa nzito sana kwani yaweza kuganda, na hivyo ili kudhibiti hali hii lazima niendelee kutumia hizi dawa.

Japo kwa sasa hali yangu imeimarika, ugonjwa huu umegharimu familia yangu pesa nyingi, na mara nyingi tulishindwa. Hii ndio hali inayokumba Wakenya wengi wanaougua maradhi ya moyo.

Ndiposa nimekuwa nikipaza sauti kutetea haki za wagonjwa wa maradhi ya moyo nchini Kenya.

Mimi ni mwanzilishi mshiriki wa Kenyan Mended Heart Patients’ Association, muungano unaotoa usaidizi kwa wagonjwa wa moyo, vile vile wazazi walio na watoto wanaokumbwa na hali hii.

Pia, nimekuwa mwanaharakati wa kushinikiza mabadiliko ya sera na ufikiaji huduma za matibabu mapema, miongoni mwa mambo mengine.

Nafanya kazi na NCDI Poverty Network kama mwanachama wa sauti za PEN-Plus.

Kwa sasa, mpango huu una kliniki mbili za moyo nchini kote; moja katika Kaunti ya Vihiga na ingine Kaunti ya Isiolo.”