Afya na Jamii

Mbinu ya ‘kufyonza mtoto’ imeokoa kina mama wengi wakati wa kujifungua

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA NURU ABDULAZIZ

SHIRIKA la afya ya uzazi na idadi ya watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) limeashiria kuwa idadi ya wanawake wajawazito wanaofariki kutokana na matatizo yanayojitokeza wakati wa ujauzito ni 355 kati ya wanawake 1,000 wanaojifungua nchini Kenya.

Hii ina maana kuwa kuna karibu wanawake na wasichana 5000 wanaofariki kila mwaka.

Ili kupunguza idadi hii, wahudumu wa afya nchini wanatumia mbinu tofauti tofauti za kuwasaidia kina mama wajawazito kujifungua salama, moja ya mbinu hizi ni mbinu ya kufyonza mtoto almaarufu kwa lugha ya Kimombo Vacuum delivery.

Njia hii hutumiwa wakati mwanamke mja mzito anajifungua kwa njia ya kawaida na wakati huo kifaa maalum cha plastiki kinatumiwa kwa kuweka kichwani mwa mtoto na kwa kutumia presha kinasaidia kumvuta mtoto huyo.

Kifaa cha kumsaidia mwanamke kujifungua ‘Kiwi cup’. PICHA|MPIGA PICHA WETU

Kulingana na daktari Felix Oindi, mtaalamu wa afya ya uzazi katika hospitali ya Aga Khan, mbinu hii inatumika sana ili kuzuia kina mama kufanyiwa upasuaji usiohitajika.

“Katika mbinu hii ya kumsaidia mama mjamzito kujifungua, kifaa kama kikombe almaarufu Kiwi cup kinatumika. Kichwa cha mtoto kina sehemu mbili laini sana mbele ya kichwa na nyuma ya kichwa, kama sentimita sita kutoka mbele na kama sentimita tatu kutoka nyuma, hivyo basi kifaa hicho kinawekwa katikati ya sehemu hizi mbili yaani katikati ya kichwa, ili kuzuia kumjeruhi mtoto kichwani. Iwapo kifaa hicho kitawekwa katika sehemu iliyo laini huenda kikaathiri ubongo wake kwa kuufyonza,” asema Dkt Oindi.

Wakati wa kutumia kifaa hicho, wahudumu wa afya huhakikisha kuwa mwanamke amefunguka kikamilifu hadi sentimita kumi, kisha kifaa hicho kinawekwa kichwani mwa mtoto na kuanza kutumika kwa kuhakikisha kuwa presha inayotumika haipiti alama iliyo na rangi ya majani katika kifaa hicho.

Presha salama

Alama hiyo huashiria presha iliyo salama kwa kichwa cha mtoto imeafikiwa, kisha pale mama mjamzito anapopata msukumo wa mtoto basi mhudumu wa afya atakitumia kumvuta.

“Wakati wa kutumia kifaa hichi cha ‘kiwi cup’, utahitajika kuvuta mara tatu tu na zoezi zima lisiwe zaidi ya dakika 20. Iwapo presha ya kifaa hicho itapita alama ya rangi nyekundu basi hii ina maana presha hiyo ni ya juu sana kwa kichwa cha mtoto na huenda kikasababisha madhara kwake. Ni vyema kuandaa chumba cha upasuaji mapema iwapo mbinu hii itafeli baada ya dakika hizo 20,” alieleza Dkt Oindi.

Mambo ambayo yanachochea wahudumu wa afya kutumia mbinu hii na pamoja na pale mama mjamzito anapochoka kumsukuma mtoto , iwapo mtoto amechoka akiwa tumboni na anahitaji kutolewa haraka, na iwapo mama ana matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la damu, matatizo ya moyo na akili ambayo hayawezi kumruhusu kumsukuma mtoto kwa muda mrefu.

“Mbinu hii haiwezi ikatumika iwapo mhudumu wa afya hana ujuzi wa kukitumia kifaa hicho cha kufyonza mtoto, pia iwapo mtoto ameanza kutoka na miguu kwanza au sehemu nyingine yoyote isipokuwa kichwa, na iwapo mtoto ana matatizo ya kiafya haswa kwa wale wana tatizo la kuwa na maji kichwani almaarufu Hydrocephalus, ” Dkt Oindi alieleza.

Pia iwapo kichwa cha mtoto hakijulikani kilipo na iwapo mtoto ni mkubwa sana basi mbinu hii haiwezi ikatumika.

Dkt Felix Oindi akieleza jinsi ya kutumia kifaa cha ‘Kiwi’ cha kumsaidia mwanamke kujifungua. PICHA|MPIGA PICHA WETU

Kuna hatari ambazo hujitokeza kutokana na mbinu hii ya mwanamke kusaidiwa kujifungua kwa kutumia ‘kiwi cup’, kama vile, maumivu zaidi katika sehemu kati ya tupu ya mbele ya nyuma, kupata jeraha katika sehemu ya siri, kuvuja damu, tatizo wakati wa kuenda haja ndogo, kutokwa kwa haja kubwa bila kujua.

Matatizo haya mara nyingi huwa yachukua muda kidogo na baadaye huisha.

Matatizo yanayojitokeza kwa mtoto ni kuwa huenda akapata uvimbe kichwani pale kifaa hicho kilitumika, ila uvimbe huo hupungua baada ya muda, kifaa hicho huenda kikaathiri fuvu la kichwa lakini jeraha kama hili sio jambo ambalo hujitokeza sana wakati wa kutumiwa kwa mbinu hii, kuvuja damu ndani ya kichwa, na pia kuna uwezekano wa mabega ya mtoto kukwama baada ya kichwa chake kutoka.

Sindano ya maumivu

Kabla ya mwanamke mjamzito kufanyiwa mbinu hii, daktari huzungumza naye na kumueleza madhara yake, faida yake na jinsi itakavyo fanywa ili kupata idhini yake.

Kisha huwa mwanamke mjamzito anadungwa sindano ya kupunguza maumivu.

Mbinu hii ya kufyonza mtoto inasaidia sana katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na pia kupunguza idadi ya wale wanaofanyiwa upasuaji usiohitajika kwa wakati huo.

Idadi ya wanawake wajawazito wanaofanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua imeongezeka maradufu kutoka asilimia tisa(9) mwaka 2014 hadi asilimia 17 mwaka 2022.