Afya na Jamii

Menyu mpya ya vyakula vilivyotokana na wadudu yazinduliwa kusaidia kukabili njaa

Na PAULINE ONGAJI April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAASISI ya kimataifa ya utafiti wa wadudu na ikolojia ICIPE, muungano wa kimataifa wa viumbe-hai pamoja na kituo cha kimataifa cha kilimo cha kitropiki CIAT, juma lililopita walishirikiana kuandaa hafla ya maonyesho ya vyakula vya kipekee vinavyotokana na mazao maalum ya shambani, vilevile wadudu.

Hafla hiyo ya maankuli kwa jina “Biodiversity Bites: A Culinary Journey into Agricultural Research in Africa” iliandaliwa ili kuangazia mbinu bunifu za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya ardhi.

Menyu iliyoandaliwa jioni hiyo ilikuwa ya kipekee iliyochochewa na mazao yanayotokana na utafiti wa mazao ya shambani kama vile maharagwe, mchele, mboga, ndizi, na hata wadudu wanaoliwa, ambapo kila mlo uliambatana na maelezo kutoka kwa wanasayansi.

Dkt Abdou Tenkouano, Mkurugenzi Mkuu wa ICIPE, alizungumza kuhusu dhamira ya shirika hilo akisema, “Tunajumuisha wadudu kwa manufaa ya binadamu na mazingira. Wadudu wanasaidia kuzalisha chakula safi, kusafisha mazingira, na kuunda nafasi za ajira kwa vijana.”

Duniani kote, zaidi ya aina 2,000 za wadudu huliwa kama chakula, huku Afrika ikiwa na takriban aina 500 ya wadudu. Panzi, viwavi aina ya mopane, na vizinga ni chakula cha kawaida katika jamii nyingi.

Supu ya nyenje (cricket). Picha|Hisani

Hata hivyo, Dkt Margaret Kababu, anayeongoza mpango wa ‘Wadudu kwa Chakula na Matumizi Mengine’, alihimiza kupanua matumizi ya wadudu kama chakula.

Alieleza kuwa, “Wadudu wana hadi asilimia 70 ya protini, wakizidi maharagwe na kuweza kushindana na nyama ya ng’ombe. Wana madini kama chuma, zinki, mafuta ya omega, na virutubisho hai vinavyofaa kwa dawa.”

Wadudu wanazidi kutambuliwa kama chanzo endelevu cha lishe.

Uwezo wa ufugaji wa wadudu nchini Kenya pia ni mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa ufugaji wa wadudu unahitaji kiwango kidogo cha ardhi, uwekezaji mdogo wa mtaji, na gharama ya chini ya utunzaji.

Aidha, soko la vyakula vilivyosindikwa kwa kutumia wadudu kama vizinga na mchwa pia linaendelea kukua, na hivyo kufanya aina hii ya kilimo kuwa njia bora ya kuendesha kilimo endelevu.

Kwa mfano, mdudu anayejulikana kama nzi mweusi au black soldier fly kwa Kiingereza, alitolewa kama mfano mzuri wa wadudu wenye manufaa kutokana na uwezo wake wa kubadilisha taka na kuwa chakula cha wanyama na mbolea, na hivyo kuwaletea wakulima manufaa.

Dkt Kababu alisema kwamba majaribio yaliyofanyiwa kwenye mimea 25 yalionyesha kuwa mbolea kutoka kwa wadudu huimarisha afya ya udongo na kasi ya ukuaji.

Lakini licha ya faida hizo nyingi, bado kuna upinzani hasa wa kitamaduni dhidi ya ulaji wa wadudu. Dkt. Abdou alikiri kuwa hali hii inatokana na ukosefu wa maarifa na uelewa, akihimiza watu “fumba macho, onja, na utarudi tena.”

Ili kurahisisha mabadiliko haya, Dkt Kababu alipendekeza kusaga waduduna kuwa unga ili wachanganywe kwa urahisi kwenye vyakula vya kila siku kama mkate au uji.

Bi Céline Termote, Mwanasayansi Mkuu kutoka Muungano wa Biodiversity International na CIAT, pia alizungumzia juhudi za kufufua ulaji wa mboga za kienyeji zenye virutubisho vingi.

Mimea hii hustawi kwenye udongo hafifu na hustahimili changamoto zinazotokana na wadudu na mabadiliko ya tabianchi.

“Mboga hizi zina virutubisho ambavyo bado hatujavigundua,” alisema Bi Termote.

Utafiti unaonyesha kuwa mboga hizi zina manufaa mengi ya kiafya zaidi ya aina ya virutubisho vya vitamini tunavyovitambua, ilhali bado havitumiwi sana.

Kwa mfano, nchini Kenya, kila Mkenya hula kilo 63 pekee za mboga za kienyeji, kinyume na pendekezo la kilo 90 kila mwaka.

Shirika la ICIPE linaongoza mpango wa kujumuisha wadudu wanaoliwa kwenye mlo wa Waafrika, kama suluhisho endelevu la kuongeza virutubishi na kukabiliana na uhaba wa chakula.

Mbali na wadudu, tukio hilo liliangazia umuhimu wa kukuza mazao ya kienyeji hasa yale yanayoweza kustahimili mabadiliko ya mabadiliko ya tabianchi.

[email protected]