Mfumo wa kidijitali ‘eCHIS’ unavyoimarisha huduma za afya Kaunti ya Kisumu
NI saa kumi na mbili unusu asubuhi katika kijiji cha Kitare, eneo la Seme, Kaunti ya Kisumu, ambapo Bi Rose Apondi, mhudumu wa afya wa kijamii (CHP), anajiandaa kwa siku nyingine kazini.
Mkononi mwake amebeba simu yake—kifaa muhimu ambacho kwa miaka kadhaa sasa kimebadilisha jinsi anavyohudumia jamii yake.
Bi Apondi anashughulikia masuala ya afya kwa zaidi ya nyumba 100, ambazo zinajumlisha takriban watu 400, na hii leo, kama siku nyingine ile, yuko tayari kusaidia kuimarisha siha na afya yao.
Bi Apondi ambaye anahudumu kupitia hospitali ya kaunti ndogo ya Manyunda, ni mojawapo ya takriban wahudumu 3,000 wa afya ya kijamii katika Kaunti ya Kisumu, wanaoongoza mabadilikko ya kidijitali katika huduma za kiafya.
Bi Apondi amepokea mafunzo ya kutumia eCHIS- jukwaa la kidijitali. Ala hii imebadilisha kazi yake na kumwezesha kuunganisha wagonjw na vituo vya afya kwa urahisi.
Kazi yake Bi Apondi inahusisha kutoa elimu ya masuala ya kiafya, kupima maradhi ya kudumu kama vile kisukari na shinikizo la damu, na kuhakikisha kwamba watu walio katika hatari kiafya kama vile akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, wanapokea huduma wanayohitaji.
Kuwatembelea akina mama
Majukumu yake ya kila siku yanahusisha pamoja na kuwatembelea akina mama wajawazito na waliojifungua, kupima maradhi kama vile malaria, na kutoa ushauri kuhusu lishe bora, ambapo anasema kwamba tangu kujumuisha ala hii katika kazi yake, uwezo wake wa kuhudumia wagonjwa umeimarika pakubwa.
“Awali ningelazimika kusafiri kwa mwendo mrefu ili kufikia kila mgonjwa moja kwa moja, suala lililonipotezea muda na kunisabababishia uchovu,” aeleza Bi Apondi.
“Kwa sasa, naweza kuhudumia kufikia wagonjwa 20 kila siku.”
Kulingana na Bi Apondi, mfumo huu wa kidijitali unampangia kila kitu ambapo haina haja kwake kutegemea rekodi za makaratasi. Rekodi hizi za kidijitali zinafanya iwe rahisi kwake kuwafuatilia wagonjwa na pia tofauti na zile za makaratasi, apu hii inahifadhi data ya wagonjwa kwenye mfumo wa cloud.
“Hii imefanya iwe rahisi kufikia maelezo ya wagonjwa kila yanapohitajika. Hii imepunguza makosa na pia kuhakikisha kwamba hali ya mgonjwa inafuatiliwa kwani sitegemei faili za makaratasi ambazo zaweza kupotea au kuharibiwa,” aongeza.
Kabla ya kuanza kutumia apu hii, sawa na wahudumu wengine wa kijamii hasa katika maeneo ya mashambani, Bi Apondi anasema kwamba walihangaika kutokana na changamoto kama vile uhaba wa rasilimali na kufikia taarifa mpya za kiafya kuhusu wagonjwa wao.
Ilikuwa kibarua kwake kuwashughulikia wagonjwa wote, na pia alilazimika kutumia muda mwingi kukagua rekodi za wagonjwa ambazo zilikuwa kwenye makaratasi.
“Matumizi ya mfumo huu yamebadilisha kabisa kazi yangu kwani mbali na kupima magonjwa, naweza kudhibiti vizuri maelezo kuhusu matumizi ya dawa, na hata kumuelekeza mgonjwa kwenda hospitalini kwa kutumia simu yangu,” aeleza.
Bi Apondi alipokea mafunzo kuhusu jinsi ya kutumia apu hii mwaka 2022, na tangu wakati huo, mambo yamekuwa shwari kwake.
Maradhi ya kudumu
“Kwa wagonjwa walio na maradhi ya kudumu kama vile kisukari au shinikizo la damu, naweza kuwajazia dawa pasipo mgonjwa kuhitajika kwenda hospitalini, na ikiwa mgonjwa atasahau kutumia dawa zake, naweza kumkumbusha kupitia apu hii,” aongeza.
Ikiwa mgonjwa anahitaji huduma zaidi, jukwaa hili linamwezesha Bi Apondi kumwelekeza kwa daktari moja kwa moja, na hivyo kumsaidia kupokea matibabu kwa wakati unaofaa.
Mfumo huu umebadilisha kabisa ufikiaji wa huduma za afya katika jamii yake Bi Apondi, hasa ikizingatiwa kwamba wengi huishi mbali na vituo vya afya ambapo wanalazimika kutumia muda na nauli nyingi kufika hapo.
“Wagonjwa wengi wangu ni wazee ambao hukumbwa na changamoto za usafiri,” asema Bi Apondi.
“Watu saasa hawaoni aibu kuzungumzia hali yao ya kiafya na wanaweza kumuona daktari pasipo kwenda hospitalini,” aeleza.
Lakini kumekuwa na changamoto ambapo mojawapo ya vizingiti vikuu ni tatizo la kimtandao hasa ikizingatiwa kwamba sehemu hii ni ya mashambani.
“Kuna wakati ambapo mtandao ni dhaifu na tumekumbwa na tatizo la kuweka data za wagonjwa au kuwasiliana na madaktari kuhusu hali ya wagonjwa.
Lakini licha ya haya, faida za jukwaa hili ni dhahiri.
Bw Fredrick Oluoch, mkurugenzi wa huduma ya afya ya umma na usafi katika Kaunti ya Kisumu, anasema kwamba jukwaa hili limebadilisha jinsi wahudumu wa afya ya kijamii wanavyotekeleza kazi zao.
“Sasa wanaweza kukamilisha kazi zao haraka na kikamilifu, suala linalowaachia nafasi ya kushughulikia masuala mengine ya kiafya,” aeleza.
Aidha, Bw Oluoch anasema kwamba, kutokana na sababu kuwa mfumo huu umewawezesha wahudumu kuhifadhi maelezo kuhusu wagonjwa vyema, kama kaunti wanaweza kukagua hali ya kiafya ya wakazi wa eneo hili na hivyo kusaidia kufanya maamuzi na bajeti.
“Kwa mfano tumeweza kujua viwango vya maradhi yasiyoambukiza, suala ambalo lilitupa mwongozo wa kufungua kliniki za kukabiliana na maradhi haya katika maeneo ya Kombewa Seme na katika hospitali ya kaunti ndogo ya Nyakach.”
Kulingana na Bw Oluoch, jukwaa hili limeimarisha huduma za kimatibabu katika vitengo 274 vya kiafya katika Kaunti ya Kisumu.