Afya na Jamii

Miji ya Afrika ingali nyuma katika kupambana na maradhi sugu

Na PAULINE ONGAJI March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ZAIDI ya watu 4.2 bilioni wanaishi mijini kote duniani kwa sasa huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka hadi takriban theluthi tatu ya watu wote kufikia mwaka 2050.

Miji inapoendelea kustawi kumeibuka hatari ya ongezeko la maradhi sugu yasiyoambukiza (non-communicable diseases kwa Kimombo) katika miaka ya hivi karibuni.

“Ongezeko la idadi ya watu, ujenzi wa majumba na barabara pamoja na ongezeko la magari barabarani ni baadhi ya masuala ambayo yamechangia kupanda maradufu kwa maradhi haya,” atanguliza Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Kijamii katika Shirika la Afya Duniani (WHO) , Bw Etienne Krug.

Wananchi katika soko la Gikomba mjini Nairobi mnamo Desemba 2024. PICHA | BONFACE BOGITA

Maradhi haya ni kama vile matatizo ya kupumua kama ugonjwa wa pumu, maradhi ya moyo, presha, uzito kupindukia, kansa na kisukari.

Athari zake hulemaza zaidi mataifa yenye pato la chini na wastani, ambapo tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya maradhi sugu hutokea.

Bara la Afrika limeathirika pakubwa na shida hii. Kulingana na Krug, miji mingi Afrika inakumbana na vizingiti vizito katika jitihada za kukabiliana na masuala ya afya ya umma.

“Miji hii inazidi kukabiliwa na matatizo ya uchafuzi wa hewa, uhaba wa vyakula vyenye virutubishi, ukosefu wa maeneo salama ya waendao kwa miguu barabarani, na uhaba wa viwanja vya umma ambavyo wakazi wanaweza kujihusisha katika mazoezi na michezo”

Bw Krug asema changamoto hizi zinazidishwa na viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa huduma bora za afya.

Hali hii ilifanya ndiposa hakuna jiji lolote Afrika lililotambuliwa kwenye tuzo za kongamano la ushirikiano wa miji yenye afya (Partnership for Healthy Cities Summit).

Tuzo hizo ziliandaliwa jijini Paris, Ufaransa, wiki iliyopita kutambua miji inayotia fora katika vita dhidi ya maradhi yasiyoambukizwa (NCDs) na majeraha.

Kulingana na Meya Erias Lukwago wa jiji la Kampala, Uganda, kukosekana kwa miji ya Afrika katika orodha ya utambuzi kunaashiria jinsi bara hili lingali nyuma katika masuala ya ustawi, na pia kuibua maswali kuhusu huduma za afya katika miji yake.

Meya wa jiji la Kampala nchini Uganda, Bw Erias Lukwago, wakati wa mahojiano kando ya Kongamano la Ushirikiano kwa Miji Yenye Afya (Partnership for Healthy Cities Summit) lililoandaliwa jijini Paris, Ufaransa, mnamo Machi 20, 2025. PICHA | PAULINE ONGAJI

Katika kongamano hilo miji mitatu kutoka Amerika Kusini na Ulaya ilitambuliwa kutokana na ubunifu wao wa kustawisha afya kwa wanamiji.

Miji ya Cordoba nchini Argentina, Fortaleza nchini Brazil na Greater Manchester nchini Uingereza, ilitambuliwa kwa sera zao za kipekee.

Cordoba ilitambuliwa katika jitihada zake za kuondoa vinywaji vyote vya sukari na vitamutamu shuleni kufikia mwaka 2026, ambapo zaidi ya watoto 15,000 wanatarajiwa kunufaika.

Nalo jiji la Fortaleza limeanzisha mfumo thabiti wa kukagua viwango vya ubora wa hewa, ili kukabiliana na uchafuzi na madhara yake kwa wakazi.

Jiji la Greater Manchester nalo limeongeza idadi ya maeneo kusikoruhusiwa uvutaji sigara, ikiwa ni pamoja na kuzindua bustani ya kwanza isiyoruhusu uvutaji sigara.

Sehemu za jiji la Paris, Ufaransa, mnamo Machi 20, 2025. Paris ni kati ya miji inayotambulika duniani kwa miundo mbinu ya kisasa inayosaidia kukabiliana na maradhi sugu yasiyoambukizwa (NCDs). PICHA | PAULINE ONGAJI

Pia, kuna miji mingine ambayo pia imechukua hatua kabambe katika kukabiliana na maradhi sugu ya NCDs.

Kwa mfano, miji ya New York City nchini Amerika na London nchii Uingereza imezindua kampeni za kuhamasisha umma kuhusu hatari za matumizi ya vinywaji vya sukari na manufaa ya kufanya mazoezi.

Aidha, miji kama vile Paris nchini Ufaransa na Copenhagen nchini Denmark imewekeza katika miradi safi ya mazingira kama vile mabasi ya usafiri wa umma yanayotumia kawi ya umeme badala ya petroli inayotoa moshi unaochafua hewa.

Kwa upnde mwingine, miji kama vile Vancouver nchini Canada na Melbourne nchini Australia imetilia maanani utengaji wa nafasi salama za wapita njia kutembea na hivyo kuwapa kichochea cha kufanya tizi ya matembezi wanapoenda kazi au kurudi nyumbani, na kupunguzia wakazi hitaji la kutegemea magari kwa usafiri.

Nayo miji kama vile Singapore katika taifa la kisiwani la Singapore na Oslo nchini Norway imeongeza ushuru wa tumbaku na bidhaa zake katika juhudi za kukatiza uraibu huu.

Lakini mambo ni tofauti kabisa barani Afrika ambapo miji mingi inazidi kuachwa nyuma katika upanuzi wa miundo misingi, na utekelezaji wa sera na kanuni za kupambana na mambo yanayochangia maradhi ya NCDs.

Hii ni licha ya bara hilo kuendelea kulemewa zaidi na mzigo mzito wa maradhi hayo.

Kulingana na shirika la WHO, maradhi kama vile kansa, matatizo ya moyo na magonjwa ya kupumua husababisha asilimia 74 ya vifo duniani huku Afrika likirekodi asilimia 37 ya vifo vyote.

Nchini Kenya takwimu za WHO zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wanakabiliwa na aina moja au zaidi ya NCDs, huku takriban asilimia 40 ya vifo hospitalini vikitokana na maradhi hayo.

Watu wawili wakiendesha baiskeli mjini. PICHA | MAKTABA

Yote tisa, kuna matumaini kwani tayari kuna miji Afrika ambayo imeanza kuweka mikakati muhimu kuangazia changamoto za kiafya zinazoikumba.

“Miji kama vile Cape Town (Afrika Kusini), Lagos nchini Nigeria na Kigali nchini Rwanda inatekeleza mikakati ya kuimarisha usalama barabarani na kudhibiti matumizi ya tumbaku,” alieleza Bw Krug.

Kwa mfano, Cape Town imekuwa ikiweka mipangilio mipya ili kupunguza ajali za barabarani.

Nalo jiji la Kigali kando na utekelezaji wa sheria za barabarani kama vile kuhakikisha waendesha boda boda wanatii sheria za trafiki, pia limepanua maeneo ya wapita njia kutembelea ili kupunguza hitaji la usafiri wa magari.

Jiji la Lagos limewekeza katika magari ya usafiri ya umma yanayotumia umeme ili kupunguza uchafuzi wa hewa unaosababishwa na moshi wa petroli.