Afya na Jamii

Muda mwingi kwenye skrini waongeza hatari za matatizo ya moyo kwa watoto

Na PAULINE ONGAJI November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UTAFITI mpya umeonya kwamba mtoto anapotumia sana vifaa vya kielektroniki, hasa pale shida hii inapoambatana na kiwango kidogo cha usingizi, kunaweza kuongeza hatari ya kupata matatizo ya moyo na kimetaboli baadaye maishani.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Journal of the American Heart Association, ulionyesha kwamba matumizi ya muda mrefu ya vifaa vya kielektroniki kama vile televisheni, simu, kompyuta, na michezo ya video, miongoni mwa vijana, yanahusiana sana na ongezeko la hatari za magonjwa ya moyo na kimetaboli ikiwa ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kiwango kisicho salama cha kolesteroli, na upinzani wa insulini.

Wanasayansi hawa kutoka Chuo Kikuu cha University of Copenhagen’s Copenhagen Prospective Studies on Asthma in Childhood (COPSAC) walichambua data kutoka kwa washiriki zaidi ya 1,000 waliotokana na tafiti mbili za muda mrefu nchini Denmark, kundi moja la watoto wa miaka 10 na jingine la vijana wa miaka 18, ili kuelewa vizuri jinsi tabia za kutumia skrini zinavyoathiri afya ya moyo na metaboli.

Waligundua kuwa kila saa ya ziada ya kutumia skrini kwa burudani, ilihusiana na ongezeko la hatari ya kimetaboli ya moyo. Miongoni mwa watoto wa miaka 10, kila saa ya ziada ya kutumia skrini iliongeza alama za hatari kwa takriban mkengeuko wa kawaida wa 0.08, huku miiongoni mwa vijana wa miaka 18 ongezeko hili likiongeza alama za hatari kwa takriban mkengeuko wa kawaida wa 0.13.

“Hii inamaanisha mtoto anayekaa mbele ya skrini kwa saa tatu zaidi kila siku, anaweza kuwa na hatari takriban robo hadi nusu ya mkengeuko wa kawaida zaidi kuliko wenzao,” alisema mwandishi mkuu Dkt. David Horner, mtafiti wa COPSAC. “Inaweza kuonekana kidogo kwa kila saa, lakini kwa muda mrefu, na kwa idadi kubwa ya watu, inaonyesha mabadiliko makubwa katika hatari za afya mapema ambazo zinaweza kuendelea hadi utu uzima.”

Wanasayansi hao walitengeneza alama ya jumla ya kimetaboli ya moyo iliyojumuisha viashirio kadhaa vya afya, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa kiuno, shinikizo la damu, HDL (“nzuri”) kolesteroli, trigliseridi, na viwango vya sukari ya damu. Pia walitumia mfumo wa machine learning kubaini mifumo maalum ya kimetaboli za damu inayohusiana na muda wa skrini.

Alama hizi za kemikali zinapendekeza kuwa tabia za kutumia skrini zinaweza kusababisha mabadiliko ya kibiolojia hata wakati mtoto bado mdogo. Utafiti huo pia uligundua uhusiano kati ya muda wa skrini na hatari inayokadiriwa ya moyo na mishipa ya damu katika utu uzima, hasa kwa vijana.

Aidha, usingizi mchache ulionekana kuongeza madhara ya muda mrefu wa skrini. Watoto na vijana waliotumia muda mrefu mbele ya skrini na kulala kwa muda mfupi walikuwa na alama za hatari za juu zaidi.

“Kwa watoto, muda wa usingizi haukuathiri tu uhusiano huu bali pia ulichangia takriban asilimia 12 ya athari hiyo,” alisema Horner. “Hii inaonyesha kwamba usingizi mfupi unachangia sehemu ya jinsi muda wa skrini unavyosababisha mabadiliko ya metaboli.”

Wanasayansi waonya kwamba matumizi mengi ya skrini, ambapo siku hizi hufikia kati ya saa 5 hadi 6 kwa siku kwa vijana, yanaweza kuwa yakibadilisha matokeo ya afya kwa muda mrefu bila mtu kuutambua.

“Kupunguza muda wa burudani mbele ya skrini wakati wa utoto na ujana kunaweza kulinda afya ya moyo na kimetaboli kwa muda mrefu,” Horner alisisitiza. “Utafiti wetu unaonyesha kuwa uhusiano huu unaanza mapema na unasisitiza haja ya ratiba za kila siku zilizo na usawa.”

Wataalamu pia wanasema kuwa kuzingatia tabia za skrini kunapaswa kuwa sehemu ya ukaguzi wa watoto, pamoja na majadiliano kuhusu lishe na mazoezi.

Dkt Amanda Marma Perak, mwenyekiti wa kamatii ya udhibiti maradhi ya moyo miongoni mwa vijana katika Muungano wa kupambana na maradhi ya moyo nchini Amerika (AHA), anashauri wazazi na walezi kuanza polepole wanapotaka kupunguza muda wa skrini miongoni mwa watoto wao.

“Iwapo kupunguza muda wa skrini kunahisi ni kazi kubwa, anza kwa kuhamisha muda huo mapema mchana na kulenga kulala mapema na kwa muda mrefu,” alisema.

Anaongeza kuwa wazazi wana jukumu muhimu katika kuweka mfano: “Sote tunatumia skrini, kwa hivyo ni muhimu kuwaelekeza watoto na vijana kutumia kwa njia ya afya na kwa makini. Onyesha tabia nzuri, weka vifaa mbali wakati wa chakula, eleza sababu, na himiza muda wa familia bila skrini.”