Namna ya kuepuka ugonjwa wa macho mekundu
ALEX KALAMA Na HASSAN WANZALA
VISA vya ugonjwa wa macho mekundu almaarufu red eyes vimeripotiwa kwa wingi katika eneo la ukanda wa Pwani nchini Kenya.
Wakazi wa eneobunge la Malindi, Kaunti ya Kilifi, wameshauriwa kudumisha usafi wa mwili na mazingira ili kukabiliana na mkurupuko wa ugonjwa huo wa macho, ambao umeanza kushuhudiwa katika eneo hilo.
Hali sawa na hiyo imeripotiwa katika taifa jirani la Tanzania ambapo Wizara ya Afya nchini humo iliwataka raia kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa wa macho mekundu husababishwa na maambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho.
Hali hiyo hujulikana kitaalamu kama ‘Viral Keratoconjunctivitis’ na hufanya jicho kuonekana jekundu.
Kabla ya visa vya ugonjwa huo kuripotiwa kwa wingi na raia wa maeneo ya Pwani nchini Kenya, mnamo Januari 15, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya nchini Tanzania Prof Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu, alitoa taarifa ya uchunguzi wa awali kuhusu ugonjwa huo.
Prof Ruggajo alisema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi, na kutoa matongo ya manjano.
Taifa Leo ilimtembelea Daktari Mkuu wa Hospitali Kuu ya Malindi David Mang’ongo, kutaka kufahamu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Dkt Mang’ongo alieleza kuwa, kwa muda wa wiki mbili sasa, hospitali hiyo imepokea visa zaidi ya 70, macho ya wagonjwa hao yakigeuka kuwa mekundu na kutoa uchafu mwingi, na kuwasha.
“Hivi sasa ugonjwa wa macho umesambaa katika mji wa Malindi. Nawahimiza wakazi na Wakenya kwa ujumla kwamba wadumishe usafi kama kuosha mikono mara kwa mara na pia waepuke kutumia vitu pamoja, na hata ikiwezekana waepuke kusalimiana kwa kupatiana mikono,” alitahadharisha Dkt Mang’ongo.
Alieleza kuwa ugonjwa huo unaweza kukabiliwa, akiwahimiza waathiriwa kutafuta matibabu na kujitenga kando na wengine kwa muda wa wiki moja, ili kurejelea hali zao za kawaida za kiafya.
“Huu ugongwa unaweza kudhibitiwa kwa urahisi sana endapo wakazi watazingatia usafi na pia endapo mmoja wao ambaye atakuwa ameambukizwa maradhi haya atajitenga kando na wale ambao hawajaambukizwa,” akasema.
Alitoa mfano akisema ikiwa mwanafunzi shuleni anaugua ugonjwa huu, inapaswa aruhisiwe kuenda nyumbani akapumzike kwa muda wa wiki moja, kisha baada ya wiki moja akiwa amepona, ndipo anaweza kuruhusiwa kurudi shuleni.
Aidha afisa huyo wa afya alidokeza kuwa eneo la Barani ndiyo sehemu ambayo imeathiriwa sana na visa vya ugonjwa huo katika mji wa Malindi. Baadhi ya shule katika eneo hilo pia zimeathirika ambapo wanafunzi na walimu wameonyesha dalili za ugonjwa huo.
Mbali na hayo, daktari huyo aliongeza kuwa ugonjwa huo umeathiri watoto, watu wazima na hata wazee.