Afya na Jamii

Sababu zinazofanya wanawake kuhisi maumivu ukeni wakati wa unyumba

January 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya wanawake wataungama kwamba kuna wakati ambapo wamekuwa na tatizo la uchungu wakati wa tendo la ndoa.   

Kwa lugha ya kitaalam, shida hii inafahamika kama dyspareunia, ambapo hutokea sana katika sehemu ya ndani ya uke.

Utafiti unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wanawake, huripoti visa vya aina hii. Visa hivi vinasemekana kuongezeka kutokana na sababu zifuatazo:

• Mabadiliko ya mbinu zinazotumika wakati wa tendo la ndoa

• Kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa

Uchungu unaoshuhudiwa wakati wa tendo la ndoa huchunguzwa na daktari wa kawaida au mwanajinakolojia.

Wataalamu wengine wanaoweza husishwa ni pamoja na daktari wa akili, mwanasaikolojia au mtaalamu wa mfumo wa viungo vya uzazi kwa wanaume na wanawake, na yule wa mfumo wa mkojo kama vile figo, kibofu na viungo vya uzazi.

Ingawa wakati mwingi uchungu huu haupaswi kuzua wasiwasi, unashauriwa kutafuta usaidizi wa kimatibabu kila unaposhuhudia ishara zifuatazo:

• Uchungu mwingi unaosababisha damu kuvuja kutoka sehemu ya uke.

• Kichefuchefu, kutapika au uchungu katika sehemu ya rektamu hasa baada ya kushiriki tendo la ndoa.

• Kutokwa na majimaji yasiyo ya kawaida baada ya kushiriki tendo la ndoa.

Nini hasa kinachosababisha hali hii?

• Kutolainisha vyema sehemu ya uke vyema kabla ya kushiriki tendo la ndoa, hali ambayo hutokana na mabadiliko ya kihomoni au matumizi ya dawa fulani.

• Uvimbe katika lango la uke

• Mkazo au mshtuko wa ghafla katika sehemu ya ndani ya uke

Uchungu katika sehemu yote ya uke, unaashiria kuharibika kwa misuli ya sehemu hii, hali nyingine isiyo ya kawaida au maambukizi ukeni.

Uchungu unaotokea wakati wa kushiriki tendo la ndoa ambapo mwanamume atahisi kana kwamba amejigonga kwa kitu, unashiria chupa ya uzazi iko katika sehemu mbaya au kulegea kwa mayai ya uzazi.

Ikiwa baada ya uchunguzi wa kimatibabu itabainika kwamba hakuna tatizo la kiafya, mbinu rahisi ya kukabiliana na mamumivu haya itakuwa kupaka mafuta maalum yanayotumika kulainisha sehemu ya ndani ya uke wakati wa tendo la ndoa.