Afya na Jamii

Sehemu ya uke inahitaji kutunzwa vilivyo kuepuka matatizo mbalimbali

Na PAULINE ONGAJI July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UKE ni kiungo chenye uwezo wa kujisafisha chenyewe kupitia utoaji wa majimaji ya asili.

Hata hivyo, kuna hatua muhimu unazoweza kuchukua ili kusaidia katika kudumisha afya ya uke.

Ili kudumisha usafi wa kawaida, osha eneo la nje la uke kwa maji safi ya uvuguvugu kila siku. Pia, unashauriwa kutumia nguo za ndani za pamba ambazo huruhusu hewa kupita.

Kando na hayo, badilisha chupi kila siku au mara kadhaa kwa siku ikiwa kuna unyevunyevu mwingi.

Aidha, baada ya haja ndogo au kubwa, jisafishe kutoka mbele kwenda nyuma ili kuzuia bakteria kuingia ukeni kutoka sehemu ya haja kubwa.

Unapofanya hivi, epuka sabuni zenye harufu kali, au kemikali ambazo husababisha mwasho na kuvuruga bakteria asili katika sehemu hii.

Pia, usisafishe ndani ya uke kwa maji au dawa.

Unapochanganua dalili za maambukizi katika sehemu hii, unapaswa kujua kwamba kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida.

Unapaswa kutambua dalili kama vile harufu kali au isiyo ya kawaida, majimaji ya rangi isiyo ya kawaida (kijani, manjano, au yenye povu), mwasho usio wa kawaida na vidonda, na maumivu wakati wa kukojoa au tendo la ndoa.

Ikiwa utashuhudia mojawapo ya dalili hizi, tembelea kliniki au mwanajinalokojia kwa uchunguzi.

Hedhi na jinsi ya kujitunza wakati huu

Unashauriwa kubadilisha visodo kila baada ya kati ya saa 4 na 6 au hata kabla ya muda huu kukamilika, kuambatana na kiwango cha damu inayotiririka.

Kando na hayo, unashauriwa kutumia bidhaa za hedhi salama na zinazokufaa. Aidha, osha uke mara kwa mara kwa maji safi.

Epuka kuweka bidhaa yoyote ndani ya uke kwa muda mrefu (kama vile tampuni), kwani hii huongeza hatari ya kukumbwa na Toxic Shock Syndrome (TSS).

Ili kujikinga kutokana na magonjwa ya zinaa

Tumia kondomu wakati wa tendo la ndoa hasa ikiwa huna mpenzi wa kudumu au ikiwa mpenzi wako hajapimwa.

Pia ni jambo la busara kupima mara kwa mara magonjwa ya zinaa, hata bila dalili. Kando na hayo, elimika kuhusu HPV (Human Papilloma Virus), ili kufahamu mengi kuhusiana na maradhi ya kansa ya lango la uzazi.

Mlo na mtindo wa maisha kwa afya ya uke

Unashauriwa kunywa mtindi, (yoghurt) isiyo na sukari) – kwani hii huimarisha bakteria wazuri.

Pia, kunywa maji mengi ili kusaidia mwili kujisafisha. Epuka sukari nyingi kwani inaweza kuchangia kuongezeka kwa ukuvu.

Kando na hayo, kabiliana na tatizo la uzani mzito na uepuke matumizi ya sigara na pombe kupindukia.