Afya na Jamii

Tambua kwa nini nyama chemsha ina madhara licha ya kupendwa na walinda afya

Na  JACKSON NGARI November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATAALAMU wa masuala ya lishe sasa wanasema kuwa ulaji wa mara kwa mara wa nyama chemsha una maadhara ya kiafya.

Wataalamu hao sasa wanasema kuwa nyama ya ng’ombe iliyochemshwa inayopendwa na wengi ina kiwango kikubwa cha mafuta.

Joy Ouma, mtaalamu wa lishe aliyesajiliwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, anasema nyama ya ng’ombe, kwa jumla, ina viwango vya juu vya mafuta ambayo yanaweza kusababisha ongezeko la kolesterol.

“Japo nyama ya ng’ombe ina protini na madini, wasiwasi hutokea inapotumiwa kupita kiasi, kwani nyama hiyo inapochemshwa, basi watu wanaikula sana,” akasema mtaalamu Ouma.

Kepha Nyanumba, mtaalamu wa lishe aliyeidhinishwa kutoka Nairobi, anaongeza kuwa mara nyingi watu hudharau madhara ya kiafya ya kula kiasi kikubwa cha nyama, bila kujali jinsi inavyopikwa.

“Nyama ya ng’ombe ya kuchemsha inaweza kuonekana kama chaguo bora zaidi ikilinganishwa na kukaanga au kuchomwa, lakini bado ina kiasi kikubwa cha mafuta, hasa katika sehemu ndogo kama vile mbavu. Mafuta haya yanaweza kujilimbikiza mwilini baada ya muda na kuchangia kiwango cha juu cha kolesterol jambo ambalo huongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu,” anasema.

Bi Ouma anaonya kwamba ulaji wa mara kwa mara wa nyama kama hiyo inaweza kuongeza kolesterol ambayo ni hatari sana kwa mwili. Viwango vya juu vya mafuta mwilini huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo.

“Watu wengi wanadhani kuwa nyama ya ng’ombe ya kuchemsha ni bora kwa sababu haijakaangwa, lakini kiwango cha mafuta kinabaki kuwa wasiwasi. Kula nyama ya ng’ombe mara kwa mara au kwa sehemu kubwa kunaweza kusababisha maadhara makubwa ya kiafya ya muda mrefu,” anasema.

Hatari nyingine iliyopuuzwa ni uwezekano wa kupata kuwa mfugo ulikuwa ukiugua kabla ya kuchinjwa kwani inaathiri watu walio na matatizo ya figo.

Nyama ya ng’ombe ina protini nyingi, na ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi kwa wingi unaweza kusumbua figo, na kufanya figo kufura au hata ugonjwa sugu wa figo.

“Unapokula nyama ya ng’ombe kupita kiasi, figo zako hufanya kazi kwa muda wa ziada ili kuondoa sumu hizi, ambazo baada ya muda zinaweza kusababisha uharibifu, haswa kwa watu ambao tayari wana matatizo ya figo,” asema Bi Ouma.

Bw Nyanumba anaongeza kuwa wale walio na historia ya familia ya ugonjwa wa figo au matatizo mengine ya msingi wanapaswa kuwa waangalifu Zaidi.

“Ulaji wa nyama mara kwa mara unaweza kuathiri utendakazi wa figo kwa watu ambao tayari wako katika hatari. Ni muhimu kula aina vingine vya chakula vilivyo nap rotini ili kuzuia ugonjwa wa figo,” anasema.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO