Afya na Jamii

Tunda la peazi ni nadra sokoni lakini ukilipata, kutakuboreshea afya barabara

April 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA PETER CHANGTOEK

MATUNDA ya mapeazi ni nadra sana kupatikana sokoni. Si wakulima wengi wanoikuza mipea nchini Kenya.

Hata hivyo, kuna maeneo kama vile Limuru, katika Kaunti ya Kiambu, ambapo mipea hupatikana.

Kwa sasa, huu ni msimu wa matunda ya mapeazi na yanapatikana kwa wauzaji mboga na matunda katika sehemu tofauti tofauti nchini, hasa jijini Nairobi.

Lakini je, wafahamu manufaa ya tunda hilo? Ni muhimu kufahamu manufaa ya mapeazi kwa mwili, na ni muhimu kula angaa peazi moja kwa siku.

Mojawapo ya manufaa ya matunda ya mapeazi ni Vitamini A, iliyoko kwa matunda yenyewe.

Vitamini A husaidia ngozi kuwa na afya na kuimarisha nywele. Pia, vitamini hiyo husaidia macho kuona vizuri.

Mapeazi pia, yana Vitamini C, ambayo husaidia kuimarisha kinga dhidi ya maradhi, na hufanya vidonda kupona haraka kwa ngozi.

Aidha, matunda ya mapeazi yana madini muhimu kama vile shaba nyekundu, ambayo huimarisha kinga dhidi ya maradhi kwenye mwili.

Husaidia pia kupunguza kolestero na kuimarisha jinsi neva inavyofanya kazi.

Vile vile, matunda ya mapeazi yana madini aina ya potasiamu na huimarisha misuli kwa mwili na kusaidia kuimarisha afya ya moyo.

Mepeazi pia, yana nyuzinyuzi zinazosaidia kwenye shughuli ya kumeng’enya chakula katika tumbo.

Isitoshe, matunda hayo yana anthocyanin na chlorogenic ambazo husaidia kuzuia ugonjwa wa saratani.

Matunda hayo pia, yana uwezo wa kusaidia mwili kuzuia kupata ugonjwa wa kisukari na husaidia kupunguza uzito kwa mwili.

Aidha, matunda ya mapeazi pia, husaidia kuimarisha mifupa.