Upele kwenye mashavu kila ninaponyoa huletwa na nini?
Mpendwa Daktari,
Nitakabiliana vipi na upele unaojitokeza kwenye mashavu na nyuma ya kichwa changu kila baada ya kunyolewa ndevu na nywele?
Harrison, Nairobi
Mpendwa Harrison,
Baada ya kunyoa, nywele huanza kuota na kupenyeza tena kwenye vinyweleo. Ncha kali za nywele hudunga vinyweleo kabla ya kuonekana nje ya ngozi.
Hii yaweza sababisha sehemu iliyoathirika kuvimba, kuasha na kubadilisha rangi na kuwa nyekundu. Wakati mwingine sehemu hii yaweza pata maambukizi. Hii yaweza tokea mahali popote ambapo nywele zimenyolewa au kung’olewa.
Tiba sahili ni kuacha nywele ziendelee kuota au kuzichenga tu badala ya kuzinyoa kabisa. Nywele zilizoota ndani ya uvimbe zaweza tolewa kwa utaratibu kwa kutumia kikoleo.
Kuna baadhi ya krimu ambazo zaweza saidia kupunguza uvimbe kama vile steroid cream, dawa za kuabilina na chunusi, krimu za viua vijasumu ikiwa kuna maambukizi, au tembe za viua vijasumu, ikihitajika.
Unapoendelea kupokea matibabu, waweza pimwa kubaini ikiwa una maambukizi mengine.
Ningependa kujua kiini cha kuumwa na shingo kila mara
Mpendwa Daktari,
Kuumwa na shingo ni dalili ya ugonjwa upi?
Jane, Nairobi
Mpendwa Jane,
Wakati mwingi maumivu ya shingo hutokana na shida za kawaida, lakini unashauriwa kutafuta ushauri wa daktari unaposhuku kuwa umezidiwa. Maumivu haya huzuia mzunguko wa shingo wa kawaida.
Ishara za maumivu ya shingo
· Shingo kuwa gumu kiwango cha kuzuia mwendo wake wa kawaida
· Uchungu mabegani na kwenye mikono
· Kushindwa kugusisha kidevu kwenye kifua
· Maumivu ya kichwa yanayosababisha kisunzi
· Maumivu katika sehemu ya shingo na ugumu unapomeza chakula
· Macho kuathirika unapotazama mwangaza
· Udhaifu miguuni
· Vilevile maumiviu haya yanaweza fuatwa na ishara kali kama vile kutapika, homa na maumivu makali ya kichwa.
Haya yanapojiri sharti utafute ushauri wa kimatibabu.