Afya na Jamii

Utaratibu wa kuchoma nyama kudhibiti hatari ya kuchangia saratani

Na PAULINE ONGAJI January 15th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KWA mujibu wa wataalamu, ulaji wa nyama iliyochomwa umehusishwa na kuongezeka kwa hatari ya kansa.

Ili kupunguza hatari hiyo, wataalam wanahimiza hatua hizi rahisi unapochoma nyama:

Chagua nyama yenye mafuta kidogo

Tumia nyama isiyo na mafuta mengi, na kama yapo yaondoe kabla ya kuchoma. Mafuta na majimaji yanapodondoka motoni husababisha moto na moshi mwingi unaochangia uzalishaji wa kemikali hatari.

Epuka nyama zilizohifadhiwa

Nyama zilizohifadhiwa kwa kemikali zinaweza kuongeza hatari ya kansa ya utumbo, hivyo ni vyema kutumia nyama mbichi isiyoongezwa vihifadhi.

Pika kwa moto wa wastani

Epuka kuchoma nyama kwa moto mkali sana. Tafiti zinaonyesha kuwa joto la juu huzalisha kemikali hatari ambazo huhusishwa na kansa, hususan ya kongosho.

Punguza muda wa kuchoma

Kuchoma nyama kwa muda mrefu huongeza uzalishaji wa kemikali zinazosababisha kansa (carcinogens). Badilisha upande wa nyama mara kwa mara ili kupunguza kukaa muda mrefu kwenye moto na moshi.

Dumisha usafi wa vifaa

Safisha waya au kifaa cha kuchomea nyama mara baada ya matumizi ili kuondoa masalio ya kemikali hatari. Kutumia kifaa kichafu kunaweza kuhamisha kemikali hizo kwenye chakula chako wakati wa matumizi yajayo.

Tumia marinadi

Kulainisha nyama kwa marinadi kabla ya kuchoma husaidia kupunguza uzalishaji wa kemikali hatarishi, kwani huunda kinga kati ya nyama na moto.