• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wakenya washauriwa kutumia tiba mbadala kupunguza gharama

Wakenya washauriwa kutumia tiba mbadala kupunguza gharama

NA MARY WANGARI

WAKENYA wameshauriwa kukumbatia tiba za kiasilia na matibabu mbadala.

Hii inaweza kufanikishwa kupitia serikali na wadau husika kuwekeza kwa mbinu hizi mbadala.

Mabilioni ya pesa zinazotumika kila mwaka na raia kusaka matibabu katika mataifa ya kigeni yataweza kuokolewa.

Hata hivyo, ukosefu wa sheria na sera madhubuti za kudhibiti uundaji, usambazaji na matumizi ya tiba mbadala na tiba za kiasilia bado ni kikwazo kikuu, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Vituo vya Matibabu vya Iran, Dkt Mahmoudreza Faghihi.

Kwenye mahajiano na Taifa Leo, Dkt Faghihi alisema kuwekeza katika matibabu mbadala kutasaidia kupunguzia mzigo familia zinazolazimika kusaka matibabu katika mataifa ya kigeni na kuvutia fedha za kigeni kupitia utalii na utafiti wa kimatibabu.

Alisema kuna mipango ya kushiriki mazungumzo na Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kuhusu matibabu mbadala yanayojumuisha tiba za kiasilia katika juhudi za kupunguza gharama za matibabu na kuimarisha afya ya umma nchini.

Kulingana naye, Wakenya hutumia takriban Sh26.2 bilioni kila mwaka kusaka matibabu katika mataifa ya kigeni ambayo yametilia maanani tiba mbadala.

India na Iran ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa utalii wa kimatibabu duniani.

Ingawa Kenya na bara la Afrika kwa ujumla limejaaliwa rasilimali na malighafi asilia tele yanayoweza kutumika kuunda na kuendeleza tiba za kiasilia, bado tiba mbadala haijatiliwa maanani eneo hili.

“Kenya na Afrika kwa jumla ina raslimali chungunzima kama vile miti, viungo mbalimbali zinazoweza kutumika. Lakini kuna pengo kubwa kuhusu tiba mbadala ambayo inaweza kuwasaida wanajamii kutibu magonjwa sugu na kuwapunguzia mzigo wa matibabu,” alisema Dkt Faghihi ambaye ni Mtaalam kuhusu Tiba za Kiasilia.

Utafiti uliofanywa kuhusu tiba za kiasili nchini mnamo mwaka 2020, unaashiria kuwa Kenya ina karibu aina 1,200 za mimea inayoaminika kuwa na manufaa ya tiba kwa binadamu na wanyama.

“Huku viwango vya ufukara vikizidi kupanda barani Afrika na uzalishaji wa chakula, mapato na misaada ya kimataifa kuendelea kupungua, huduma ya afya kiasilia imezidi kuwapa riziki madaktari wa kiasili, wavunaji, wachuuzi na wanaouza bidhaa hizo katika mataifa ya kigeni,” inasema ripoti hiyo.

“Mimea huvunwa ili kutumiwa nchini na pia kama malighafi ya kuanzia uundaji wa tiba za kisasa nchini na ulaya. Kando na manufaa ya kimatibabu, mimea hutumika kama lishe bora (supu na rojo inayotiwa kwenye maziwa ya watoto) na kama viungo kwa chai.”

Shirika la Afya Duniani (WHO) linafafanua Tiba za Kiasilia kuwa maarifa, ujuzi na ufundi unaojikita kwenye dhana, imani na tajriba za kiasili kwa tamaduni mbalimbali na zinazotumika kudumisha afya, kuzuia, kugundua, kuboresha au kutibu afya ya mwili na akili.

China ni moja kati ya mataifa ambayo yamejipatia umaarufu kupitia tiba zake za kiasili kama vile Unani, Ayurveda, na Siddha.

Dkt Faghihi alizungumza katika hafla ya matibabu bila malipo kwa wakazi wa vitongoji duni vya Kibra, Kaunti ya Nairobi, yaliyofadhiliwa na Ubalozi wa Iran kuadhimisha Sikukuu ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu na Red Cresent inayosherehekewa kote duniani Mei 8 kila mwaka.

  • Tags

You can share this post!

Raia wa Congo asukumwa gerezani kwa kashfa ya dhahabu ya...

Sita walioangamia kwenye maporomoko Murang’a wazikwa

T L