Wanasayansi waonya hatari ya kula chakula baada ya saa tatu usiku
NA CECIL ODONGO
WANASAYANSI wamebaini kuwa kula chakula hasa baada ya saa tatu usiku unachangia hatari ya kupata maradhi ya moyo na unene kupitia kiasi.
Watafiti kutoka Uingereza waligundua kuwa kula staftahi, chamcha na chajio kwa wakati wake husaidia katika kufanikisha mchakato wa mmeng’enyo tumboni.
Pia, husaidia katika mchakato wa chakula kusagwa na kemikali mbalimbali ndani na kuishia kupatia mwili nguvu zinazohitajika kufanya kazi mbalimbali.
Hata hivyo, Wanasayansi hao wamependekeza kuwa kula chajio mapema hasaidia mwili kutulia na kumaliza saa 12 kabla ya kula staftahi, husaidia kupunguza uzani mwilini, shinikizo la damu na kutanuka kwa mishipa ya damu.
Kula chajio kuchelewa pia huathiri usingizi na hili hutokea sana kwa wale ambao wanabugia pombe kiholela kisha kukesha au kulala kwa kuchelewa.
Kwa kifupi, kula kuchelewa kunachangia hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kupata unene kupita kiasi.
Watafiti hao waligundua kuwa nyakati za asubuhi mwili huwa na kiwango cha juu cha sukari.
Hilo hutokana na kula mapema kwa muda unaostahili nyakati za usiku na mchakato wa mmeng’enyo kumalizika kwa wakati. Hii ndiyo maana, kula kuchelewa usiku huathiri hata muda wa kula staftahi kwa kuwa mwili huwa haujajiandaa vyema.
Masuala mengine ambayo huvuruga mwili na kuuweka katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo ni kunywa pombe au kutumia mihadarati, na pia mtindo ambao usingizi huvurugwa na mtu kukosa kulala vizuri.
Watafiti vilevile, waligundua kuwa mwili huongezeka uzani nyakati za jioni na kiwango cha sukari hupanda wakati ambapo chakula cha jioni hucheleweshwa.
Hii wanaelezea hutokana na hali kuwa mwili hutulia na hutoa kemikali aina ya melatonin kwa wingi. Pia kula wakati ambao kemikali hiyo imeongezeka huchangia kupanda kwa kiwango cha sukari.