Wanaume waacha chupi za ‘polyester’ kunusuru mbegu za uzazi – Utafiti
IMEBAINIKA kuwa wanaume wanaacha kuvalia chupi na kaptula zilizotengenezwa kwa kitambaa cha ‘polyester’ kutokana na sababu za afya na uzazi.
Sasa wanakumbatia kaptula au chupi ambazo zimetengenezwa kwa pamba au manyoya ambazo zinaonekana kutokuwa na hatari kwao kiafya.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la The Wall Street, ulisema kuwa chupi zilizoundwa kwa vitambaa vya polyester (vyenye plastiki), vina kemikali ambazo zinahusishwa na athari hasi kwenye mbegu zao za uzazi.
Wanasayansi kwenye tafiti mbalimbali wamekuwa wakisema plastiki ndogo zisizoonekana kwa urahisi mara nyingi hupatikana kwenye hewa, chakula na maji.
Kemikali hizo hubeba uchafu ambao huathiri viungo vya binadamu na husababisha magonjwa kama kansa, kutanuka kwa mishipa, magonjwa ya moyo na huharibu seli za mwili.
Chupi ambazo zinabana lakini zinapanuka au kujivuta na zimeundwa kwa vitambaa vya polyester, zimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa wanaume hasa vijana.
“Iwapo ni chupi ya plastiki ambayo imeshika sana korodani, basi hupunguza ubora wa mbegu za kiume, kiwango cha mbegu hizo na kuathiri uzazi wa wanaume,” akasema Mtaalamu wa masuala ya afya Jaime Knopman.
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia Alex Robles, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uzazi, alisema utafiti zaidi unastahili kufanywa kubaini ni aina gani ya vitambaa vinavyotumika kutengeneza chupi na athari zao katika uzazi wa mwanaume.
“Kuvalia chupi ambayo imekushika, kuketi kwa kipindi kirefu au kuendesha baiskeli huongeza kiwango cha joto na kumehusishwa na kupunguza ubora wa mbegu za kiume katika tafiti za awali,” akasema Robles.
Watafiti hao hata hivyo wanashikilia kuwa baadhi ya wanaume wamebaini kuwa ubora wa mbegu za kiume huongezeka wakikosa kuvaa chupi au kaptula zilizowabana.
Kwa hivyo, wamewashauri wavalie chupi ambazo hazijawabana, wazuie kuwa penye joto jingi, wale vyakula vyenye madini na waache uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi.