Afya na Jamii

Wasiwasi kaunti 17 zikikosa madaktari wa kutibu matatizo ya kiakili

June 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LEON LIDIGU

KAUNTI 17 nchini hazina madaktari wa akili wanaoshughulikia matatizo ya kiakili hivyo kuwanyima maelfu ya wagonjwa Wakenya matibabu wanayohitaji, wataalam wamesema.

Rais wa Muungano wa Madaktari wa Matatizo ya Kiakili Nchini, Chitayi Murabula, amesema kaunti za Tana River, Lamu, Taita Taveta, Garissa, Marsabit, Isiolo, Nyandarua, Kirinyaga, Turkana, Samburu, Uasin Gishu, Nandi, Narok, Busia, Homa Bay, Migori na Nyamira, hazina daktari hata mmoja wa akili wa kuwahudumia Wakenya.

Alisema kaunti nyinginezo zina daktari mmoja au wawili wa kutibu akili wanaohudumia watu zaidi ya 1.3, akizungumza jana katika Kituo cha Kongamano cha Nairobi Hospital wakati wa Kongamano la pili kuhusu Afya.

Kongamano hilo lenye kaulimbiu “Kuimarisha Afya ya Akili Kenya na Afrika” liliandaliwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG).

“Ninatoka Kaunti ya Kakamega na tuna daktari mmoja tu wa kutibu akili,” Dkt Murabula.

Alisema visa vya maradhi ya akili vimeongezeka huku vikichochewa na upungufu wa wataalam wa kukabiliana na matatizo hayo.

“Tunataka kukumbuka kuwa afya ya akili ni haki ya kiafya kwa mujibu wa katiba. Maradhi ya akili husababisha ufukara na ufukara ni kiini kimojawapo kinachosababisha maradhi ya akili,” akafafanua.

Jopokazi kuhusu Afya ya Akili Nchini lililobuniwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta lakini likasitisha oparesheni zake 2020 lilitoa mapendekezo 15 na kutoa wito kwa serikali kupatia kipaumbele mafunzo ya kushughulikia masuala ya afya ya akili.

Jopokazi hilo lilitaja maradhi ya akili kuwa janga linaloibuka kutokana na kuongezeka kwa visa vya kujitia kitanzi, dhuluma za kijinsia na matatizo mengineyo yanayohusu afya ya akili, likisema yanaashiria mahitaji katika jamii ambayo yamekosa kutimizwa.

Kulingana na Sera kuhusu Afya ya Akili 2015-2030, Kenya ni miongoni mwa asilimia 28 ya mataifa wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) yasiyo na bajeti mahsusi ya kushughulikia afya ya akili.

“Afya ya akili ni sehemu inayozua wasiwasi mwingi duniani kote na washiriki walisema wazi kwamba Kenya imeathirika vilevile. Mtu mmoja kwa kila watu wanne anayetafuta huduma ya matibabu nchini ana matatizo yanayohusu afya ya akili,” inaeleza WHO.

Ripoti mpya kuhusu utoaji huduma za afya ya akili nchini iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilidadisi iwapo Wizara ya Afya (MoH) na serikali za kaunti zimeweka mikakati inayofaa kwa utoaji huduma za afya, inaafikiana na Dkt Chitayi.

“Ni kaunti 25 pekee miongoni mwa kaunti 47 zilizo na vituo vya kushugulikia afya ya akili kuashiria kuwa kaunti 22 hazina vituo vya kutoa huduma ya afya ya akili. Wagonjwa katika kaunti hizo 22 ambazo hazina vituo vya afya ya kiakili wanalazimika kulipa gharama ya kusaka matibabu katika kaunti jirani.