Ageukia kilimo cha penino baada ya matundadamu kumpiga chenga
Na PETER CHANGTOEK
BEI duni na maajenti wanaowapunja wakulima wanaoshughulika na ukuzaji wa viazi, ni kati ya sababu ambazo zilimsukuma kujitosa kwa bahari ya ukuzaji wa mimea aina ‘pepino melons’, ufugaji wa nyuki na ukuzaji wa miche ya mimea aina ainati.
Japo Zakayo Kipkorir alijaribu kufanya shughuli ya ukuzaji wa mimea aina ya matundadamu (tree tomatoes) mwanzoni, maradhi fulani ya mmea huo yalimshurutisha kukatiza shughuli hiyo, na kuanza kuikuza mimea aina ya ‘pepino’ na kuwafuga nyuki.
Mkulima huyo, ambaye ana umri wa miaka 46, pia huiuza miche ya ‘pepino’ na mingine mingineyo ya mimea mbalimbali, anayoikuza katika shamba lake lililoko katika eneo la Seguton, umbali wa kilomita takriban 19, kutoka mjini Molo, karibu na barabara ya Molo-Olenguruone.
Anadokeza kuwa alijitosa katika ukuzaji wa mimea aina ya matundadamu takriban miaka saba iliyopita, na ugonjwa huo ulipozuka, ukamshurutisha kufikiria kuhusu mbinu nyingine.
“Nilianza kufanya shughuli hii mnamo mwaka 2013, kwa kuikuza mimea aina ya matundadamu, ambayo iliathiriwa na maradhi baadaye, katikati ya mwaka 2015,’’ afichua.
Baada ya kilimo hicho cha mimea aina ya matundadamu kusambaratishwa na ugonjwa, aliamua kuubadilisha mkondo.
Anafichua kwamba baadaye mnamo mwaka 2016, alianzisha shughuli ya ukuzaji wa mimea aina ya ‘pepino’ mnamo mwaka 2016, akiutumia mtaji wa Sh700, baada ya kusoma katika jarida la Seeds of Gold kuhusu mmea huo.
Kwa wakati huu, anashughulika na ukuzaji na uuzaji wa miche ya ‘pepino melon’, anayosema kuwa huiuza kwa Sh100 kwa mche mmoja.
Miche hiyo hutoka kwa mimea ambayo imekomaa, ambapo yeye huikata na kuikuza kwa kitalu, kisha kuwauzia wateja wake. “Mwezi mmoja unatosha kwa miche kuwa tayari kuuzwa,’’ adokeza mkulima huyo, ambaye ni mzazi wa watoto wawili.
Anaongeza kuwa, watu wameanza kupata ufahamu kuhusu matunda aina ya ‘pepino melon’ kwa sababu ya manufaa ya afya ambayo matunda hayo yanayo. Hata hivyo, anafichua kuwa ndege huyaharibu matunda hayo yanapoiva shambani. Pia, mkulima huyo anadokeza kuwa usafirishaji wa matunda hayo sokoni ni mojawapo ya changamoto.
Mbali na shughuli ya ukuzaji na uuzaji wa miche pamoja na matunda ya ‘pepino’, mkulima huyo pia, anajihusisha na ufugaji wa nyuki. Alianza kufanya shughuli hiyo mnamo mwezi Aprili mwaka 2016, ambapo anasema alianza kwa kuutumia mtaji wa Sh12,000.
“Nilianza (kufanya) ufugaji wa nyuki mwezi Aprili mwaka 2016, kwa kuitumia mizinga mitatu na mtaji wa Sh12,000, na kwa sasa nina mizinga ishirini,’’ afichua mkulima huyo mwenye umri wa miaka.
Anadokeza kuwa ufugaji wa nyuki hauna kazi ya kubwa mno. Pia, anesema kwamba asali huhitajika sana. Hata hivyo, anasikitika kuwa waja wengi hupenda asali lakini hawawapendi nyuki!
Ili kurina asali, mja hana budi kuwa na mavazi maalum ya kujikinga dhidi ya nyuki. Aidha, mrindaji wa asali anafaa kuwa na kifaa cha kutumia kuupulizia moshi mzingani ili kuwazubaisha nyuki na kuwafanya wasiwe wakali sana. Hali kadhalika, anafaa kuwa na kisu cha kukata au kuibandua asali kutoka kwa mbao za mzinga. Isitoshe, awe na kifaa cha kutia asali, kama vile ndoo.
Zakayo, ambaye hukiendeleza kilimo hicho katika shamba lake ekari moja nukta nane (1.8), anasema kuwa hurina asali mara mbili kwa mwaka, na huuza kilo moja ya asali kwa Sh450.
Aidha, huuza miche ya matundadamu kwa Sh50, pepino kwa Sh100, mikalatusi kwa Sh100.